Hotuba ya Papa Leo XIV Kwa Wanadiplomasia Wapya Mjini Vatican 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Umuhimu wa diplomasia ya Vatican unakita mizizi yake katika: Amani, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa na umaskini duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote kwani kuna mamilioni ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo endelevu! Vatican inawataka waamini pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu, ili kuweza kukabiliana na changamoto katika ulimwengu mamboleo. Mataifa yatambue kwamba, yanategemeana na kukamilishana na kwamba, binadamu ni kiumbe jamii. Kwa njia, hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa ni alama ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo kutokana na sababu mbalimbali. Vatican inakazia pamoja na mambo mengine: Mosi, umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbalimbali za dunia. Jambo la pili, ni uhamasishaji wa familia ya binadamu kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, ili kujenga na kuimarisha: haki, umoja na udugu ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Vatican inakazia: ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kutatua migogoro ya kivita na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia! Lengo la tatu la diplomasia ya Vatican ni kukuza na kudumisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani.
Katika sehemu hii, Vatican imekuwa ni sauti ya kinabii na hasa zaidi sauti ya watu wasiokuwa na sauti! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu wote bila ubaguzi. Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata maendeleo ya kweli na endelevu, basi binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu! Kanisa linapenda kudumisha mchakato wa haki, amani na utulivu, kwa kuzimisha moto wa machafuko, kinzani na vita kwa maji ya baraka, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.Ni mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia unaojikita katika kubainisha mbinu mkakati wa mawasiliano, vikwazo na vizingiziti vinavyoweza kujitokeza pamoja na kuunda mazingira ya kuaminiana na kuthaminiana, ili kuendeleza majadiliano. Diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbalimbali za dunia inajikita kwa namna ya pekee, katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ni diplomasia inayojipambanua kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!
Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 6 Desemba 2025 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi 13 wanaoziwakilisha nchi za: Uzbekistan, Liberia, Lesotho, Afrika ya Kusini, Fiji, Lithuania, Finland, Micronesia, Thailand, Bahrein, Sri Lanka, Pakistan, na Moldova. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amejikita zaidi katika umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza katika kutafuta, kulinda na kudumisha amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu sehemu mbalimbali za dunia, maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza. Diplomasia ya Vatican inachota amana na utajiri wake kutoka katika tunu msingi za Kiinjili, ili kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, utume wa wanadiplomasia unapaswa kufumbatwa katika kudumisha ushirikiano ili kudumisha misingi ya haki, udugu, haki na amani.
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” na yanalenga pamoja na mambo mengine: Kuwahamasisha waamini kuishi kwa matumaini na hivyo kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa fadhila ya matumaini inayokita mizizi yake katika imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili sanjari na kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kukuza na kudumisha amani ambayo kimsingi si kukosekana kwa vita, kinzani na misigano, bali amani inayopata chimbuko lake katika sakafu ya moyo wa mwanadamu, kwa kuondokana na kiburi, moyo wa kutaka kulipiza kisasi pamoja na matumizi mabaya ya maneno kama silaha ya vita. Vita inaendelea kuhatarisha na kugumisha mahusiano ya familia ya binadamu na kwamba waathirika wakuu ni maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.” Kumbe, maskini wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya teknolojia sanjari na maendeleo fungamani ya binadamu. Vatican haitaweza kukaa kimya na kufumbia macho ukosefu wa usawa, haki, amani pamoja na uvunjaji wa haki msingi za binadamu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, diplomasia ya Vatican kimsingi, inachota amana na utajiri wake kutoka katika tunu msingi za Kiinjili, ili kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili; kusimama kidete kudumisha utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi, kwa kuzingatia dhamiri nyofu, mahali patakatifu ambapo Mwenyezi Mungu anaongea na mja wake; sanjari na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Utume wa wanadiplomasia unapaswa kufumbatwa katika ujenzi wa ushirikiano ili kudumisha misingi ya haki, amani na udugu wa kijamii. Huu ni mwaliko kwa wanadiplomasia hawa, kufungua milango mipya ya majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujenga umoja na ushirikiano, utakaosimamia ujenzi wa haki na amani katika ulimwengu mamboleo.
