Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo: Vikosi Vya Ulinzi na Usalama Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss, maarufu kama “Swiss Guards, Guardia Svizzera Pontificia” kina dhamana na utume unaojikita katika wito, uaminifu, umakini na sadaka inayotekelezwa kwa moyo wa unyenyekevu pasi na makuu. Kila mwaka ifikapo tarehe 6 Mei Wanajeshi wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswiss, wanafanya kumbukizi ya askari 147 kutoka Uswiss walioyamimina maisha yao mjini Roma kwa ajili ya kumtetea Papa Clement VII kunako mwaka 1527. Wanajeshi hawa katika maisha na utume wao waendelee kuimarishwa na imani kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Wawe ni mashuhuda na mitume wa upyaisho wa maisha binafsi na yale ya kijumuiya, kama kielelezo cha utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka katika huduma na maisha ya kijumuiya. Watu wanataka kuona utakatifu wa maisha kutoka kwa wafanyakazi wa Vatican! Kumbe, kambi ya kijeshi iwe ni mahali pa kujifunza kanuni maadili, utu wema na tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kukuza na kudumisha majadiliano, ukweli wa maisha, mahusiano mema pamoja na maelewano. Katika hali na mazingira kama haya, kutakuwepo na nyakati za furaha pamoja na nyakati za majonzi.
Kipindi hiki, kiwe ni fursa ya kujenga urafiki mwema, kwa kuheshimu na kuthamini mawazo yanayotolewa na wengine; kwa kuendelea kujifunza kuona kwa mwingine yule ndugu na jirani ambaye ni mwandani wa safari ya pamoja. Tabia hii itawawezesha kuishi katika jamii wakiwa na mwelekeo sahihi wa maisha, kwa kutambua na kuheshimu tofauti za kitamaduni, kidini na kijamii kama amana na utajiri na wala si tishio la maisha. Hii ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo kutokana na uwepo wa makundi makubwa ya watu wanaotafuta usalama na maisha bora zaidi. Wanajeshi hawa wanatakiwa kuungana na kudumisha maisha yao na Kristo Yesu, ili waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: toba, wongofu wa ndani na maisha ya sadaka yanayowang’oa kutoka katika uchoyo na ubinafsi; tayari kupambana na mapungufu yao ya kibinadamu; daima wakitafuta mafao ya wengi na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.
Wanajeshi hawa wanapaswa kushikamana na Kristo Yesu, ili kuendelea kufurahia maisha, kwani nje ya Kristo Yesu “watanyauka na kupotelea gizani,” mahali “kusikojulikana.” Katika maisha na utume, hata wao wamewahi kukutana na watu ambao “wanaelemewa na makaburi”; watu wasiokuwa na dira wala mwelekeo wa maisha; watu wenye shida na mahangaiko makubwa. Hawa ni wale wanaotarajia kuona mwanga utakaopyaisha maisha na hatimaye, kuzaliwa upya! Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawasihi wanajeshi hawa kuwaendea watu wote: kwa maneno ya faraja; wakutane nao katika alama ya udugu wa kibinadamu, ili kwa pamoja waweze kuwa kweli ni mashuhuda hai wa Kristo Yesu Mfufuka; Alfa na Omega, nyakati zote ni zake! Hii ndiyo njia muafaka ya kuishi kikamilifu wito wao wa Kikristo unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, chemchemi ya imani! Wakati wote wanapokuwa hapa Roma, wanahimizwa kushuhudia imani yao kwa furaha, ili mahujaji na wageni wanaotembelea mjini Vatican waweze kuonja na kuguswa na ari pamoja na sadaka ya maisha yao inayofumbatwa na upendo wa Mungu kwa kila binadamu. Huu ndio wito wa kwanza kabisa kwa kila mwamini! Wanajeshi hawa wawe ni mashuhuda na mitume wa upyaisho wa maisha binafsi na yale ya kijumuiya, kama kielelezo cha utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka katika huduma na maisha ya kijumuiya. Watu wanataka kuona utakatifu wa maisha kutoka kwa wafanyakazi wa Vatican!
Katika majiundo yao, wanapata katekesi ya kina na endelevu kuhusu: uaminifu, maana ya sadaka na zawadi ya maisha; ulinzi na usalama; dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika Kanisa la Kristo. Hiki pia ni kipindi kinachowawezesha askari hawa kujichotea amana na utajiri wa kitamaduni kwa kufanya hija katika maeneo muhimu ya kihistoria. Wanajeshi hawa wanajifunza kwa kina na mapana matendo ya huruma kiroho na kimwili, kwani ni sehemu ya vinasaba vya utume wao. Mara nyingi hawa ndio wanaomsindikiza mtunza sadaka mkuu wa Papa na kwa sasa katika nafsi ya Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo, katika kuwasaidia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii katika mitaa ya Roma nyakati za usiku, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” na yanalenga pamoja na mambo mengine kuwahamasisha waamini kuishi kwa matumaini na hivyo kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa fadhila ya matumaini inayokita mizizi yake katika imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni, ameadhimisha Jubilei kwa Askari wa Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswiss, maarufu kama “Swiss Guards, Kikosi cha Zima Moto kutoka Vatican pamoja na “Gendarmerie.” Katika mahubiri yake, amedokeza kuhusu maana ya Noeli, ambayo kwayo Kristo Yesu anaingia katika historia ya binadamu, chemchemi ya furaha, imani, matumaini na mapendo. Hii ni furaha inayopaswa kuwakumbatia na kuwaambata watu wote wa Mungu na hasa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.
Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani; ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Kristo Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi, chemchemi ya furaha na matumaini awaongoze waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la upendo na huruma ya Mungu. Kardinali Parolin amekazia sana umuhimu wa toba na wongofu wa ndani na kwamba, Mwenyezi Mungu anakuja kuwafariji watu wake.
