Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Loreto: Shule ya Bikira Maria!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto yaliyoko nchini Italia, ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa familia ya Mungu! Watu wanataka kuona matendo kama kielelezo cha imani tendaji! Sala, toba na wongofu wa ndani pamoja na tafakari ya kina ya Neno la Mungu ni nyenzo muhimu sana katika uinjilishaji mpya, ili kuwawezesha waamini kugundua na kuonja uwepo fungamani wa Mungu katika historia, maisha na matukio mbalimbali wanayokumbana nayo katika safari ya maisha ya hapa duniani. Kwa njia hii, waamini watakuwa na ujasiri wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na jirani zao, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wanaohitaji msaada zaidi! Papa Benedikto XV tarehe 24 Machi 1920 alimtangaza Bikira Maria wa Loreto kuwa ni mlinzi na mwombezi wa marubani na wasafiri wanaotumia usafiri wa anga duniani, ili katika huduma yao, wawasaidie pia waamini kutamani kwenda mbinguni, ili kuungana na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Kumbe, viwanja vya ndege ni mahali muafaka pia kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji kutokana na ukweli kwamba, kuna umati mkubwa wa watu wanaosafiri kwenda sehemu mbalimbali za dunia. Itakumbukwa kwamba, kila mwaka ifikapo tarehe 10 Desemba Kanisa linaadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Loreto, nafasi adhimu ya kuendelea kulitafakari Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya watu wake. Baba Mtakatifu Leo XIV, wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 10 Desemba 2025 anawaalika waamini kuyaelekeza macho yao mbinguni na kwamba, katika Shule ya Bikira Maria waendelee kujifunza kutumaini na kupenda. Wagonjwa na wazee, wapate faraja na kwamba, wanandoa wapya wajiaminishe kwa tunza na maongozi ya Bikira Maria wa Loreto.
Ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni mapambano endelevu na fungamani yanayohitaji nguvu ya upendo na huruma ya Mungu. Ni mwaliko wa kukesha na kusali, ili wasitumbukie kwenye majaribu, kwa kuwa karibu na Kristo Yesu katika: Sala, Neno, Sakramenti na huduma makini kwa jirani. Waamini waendelee kumwomba Bikira Maria ili katika umaskini, unyonge na udhaifu wao wa kibinadamu, awaombee na kuwategemeza katika uvumilifu, utii, unyenyekevu na huduma makini kwa maskini na wahitaji zaidi. Awaombee neema ya kuendelea na hija hii ya maisha ya kiroho, kwa kutambua na kuhisi uwepo wa Kristo Yesu na Bikira Maria katika maisha na utume wao, ili waweze kushikamana katika umoja, ushiriki na utume wa Mama Kanisa. Baraza la Kipapa la Nidhamu na Sakramenti za Kanisa tarahe 31 Oktoba 2019 lilichapisha Hati juu Maandhimisho ya Sikukuu ya Bikira Maria wa Loreto iliyoaridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili iweze kuingizwa katika kalenda kuu ya madhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Hadi sasa kumbukumbu hiyo ilikuwa ikifanyika kwa ngazi ya Kanisa mahalia tu. Ibada kwa ajili ya Nyumba Takatifu ya Loreto ilianza kwa kipindi kirefu na asili ya Madhabahu hayo hadi leo hii, imefikiwa na mahujaji kutoka pande za dunia kwa ajili ya kuimarisha imani yao katika Neno aliyefanyika Mwili kwa ajili ya Ukombozi wa mwanadamu. Katika madhabahu hayo yanakumbusha Fumbo la Kristo Yesu aliyefanyika mwili na kutoa msukumo kwa wale ambao wanaitembelea na kufikiri utimilifu wa nyakati, wakati Mungu alipomtuma Mwanaye aliyezaliwa na mwanamke, pia kutafakari kwa kina juu ya maneno ya Malaika aliyompasha habari, hata majibu ya Bikira Maria aliyojibu wito wa Mungu. Kufunikwa na kivuli cha Roho Mtakatifu na kuwa mnyenyekevu wa Bwana, kwa maana hiyo eneo hili limegeuka kuwa nyumba ya Mungu, picha safi ya Kanisa Takatifu.
Madhabahu hayo yamewekwa pia moja kwa moja chini ya ulinzi na usimamizi wa Vatican na kwamba yamepewa sifa na viongozi wa Kanisa na kwamba, duniani yanajulikana sana kielelezo cha mji wa Nazaret katika nchi Takatifu; zile fadhila za kiinjili za Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Katika Nyumba Takatifu, mbele yake Picha ya Mama wa Mkombozi na wa Kanisa, Watakatifu na wenyeheri waliweza kujibu wito wake huo huo; wagonjwa wanaomba faraja katika mateso yao, watu wa Mungu walianza kusifu na kumwomba Bikira Maria kwa njia ya Litania ya Bikira Maria wa Loreto na nyimbo duniani kote. Kwa namna ya pekee, ni lazima kukumbuka ni watu wangapi wanasafiri kwa ndege na wameweza kumtembelea, Mama kikao cha ibada. Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Nidhamu na Sakramenti za Kanisa katika Hati hiyo anaandika kwamba: katika mwanga wa hayo yote, Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa limeamua kutekeleza uamuzi wa Baba Mtakatifu Francisko ambapo ametoa idhini kwamba, badala ya maadhimisho ya Bikira Maria wa Loreto kuadhimishwa katika Kanisa mahalia peke yake sasa itadhimishwa kwa ngazi ya Kanisa la ulimwengu. Kadhalika ili kuhakikisha kwamba, marekebisho haya yanaingizwa katika Kalenda ya Liturujia ya Kanisa, kila tarehe 10 Desemba siku ambayo ni sikukuu ya Bikira Maria wa Loreto ambayo imekuwa ikiadhimishwa kila Mwaka. Maadhimisho haya yatasaidia waamini wote hasa familia, vijana na watawa kuiga mfano wa fadhila timilifu za Mtume wa Injili, Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.
