Tafuta

Maua yaliyowekwa  huko Bondi Beach nchini Australia kukumbuka wathirika wa shambulio la kigaidi. Maua yaliyowekwa huko Bondi Beach nchini Australia kukumbuka wathirika wa shambulio la kigaidi.  (AFP or licensors)

Papa analaani shambulio la Sydney:"ni kitendo kisicho na maana"

Katika telegramu iliyosainiwa na Kardinali Parolin,Katibu Mkuu wa Vatican na kuelekezwa kwa Askofu Mkuu Fisher,alionesha ukaribu wake wa kiroho na wale walioathirika na mkasa huo na kuwaombea wale wanaojaribiwa na vurugu wageuke na kutafuta njia ya amani na mshikamano."Papa aliwahakikishia maombi kwa ajili ya uponyaji wa waliojeruhiwa.

Vatican News.

Papa Leo XIV Jumatatu tarehe 15 Desemba 2025 alilaani shambulio la kutisha lililotokea Dominika 14 Desemba huko Sydney nchini Australia , ambalo lilisababisha vifo vya wanajumuiya wa Kiyahudi waliokusanyika kwa ajili ya sherehe ya Hanukkah kwenye Ufukwe wa Bondi. Papa alielezea tukio hilo kama"Kitendo cha vurugu kisicho na maana." Kufuatia kauli ya asubuhi Jumatatu 15 Desemba, wakati wa Mkutano na  wafadhili wa tukio la kupamba mti na Pango la  kuzaliwa kwa Yesu katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, alitoa  wito wa kukomesha aina zote za "vurugu dhidi ya Wayahudi."


Kwa njia hiyo Papa alituma telegramu yake kutoa  rambirambi iliyosainiwa na Katibu wa Mkuu wa Vatican,  Kardinali Pietro Parolin kwa Askofu Mkuu Anthony Fisher wa Jimbo Kuu Katoliki la Sydney, nchini Australia ambapo alionesha "huzuni yake kubwa" kuhusu mauaji haya yaliyotokea wakati wa likizo ya Kiyahudi ya siku kuu ya  Hanukkah. Shambulio hilo lilifanywa na washambuliaji wawili, baba na mtoto wake, ambapo mmoja wao alisimamishwa kishujaa na raia mmoja, mmiliki wa duka la matunda katika kitongoji cha Sutherland, ambaye alimpokonya silaha mtu huyo kwa mikono mitupu. Mmoja wa wahalifu baadaye aliuawa na polisi ambao walifika haraka ufukweni. Watu kumi na tano wameuawa hadi sasa, huku takriban thelathini wakijeruhiwa.

Maombi kwa ajili ya waliojeruhiwa

“Kwa wale walioguswa na kitendo hiki kisicho na maana cha vurugu, Papa Leo anaelezea ukaribu wake wa kiroho. Na kwa matumaini mapya, aliomba kwamba wale wanaojaribiwa na vurugu wageuke na kutafuta njia ya amani na mshikamano.” Katika telegramu, Papa aliwahakikishia maombi yake "kwa ajili ya uponyaji wa wale ambao bado wanaendelea kupona" na "kwa ajili ya faraja ya wale wanaoomboleza kufiwa na mpendwa wao." Hatimaye, alituma "baraka za kimungu za amani na nguvu kwa Waaustralian wote."

Ujumbe wa Askofu Mkuu Fisher

Askofu Mkuu Fisher mwenyewe, baada ya tukio la kupigwa risasi waathrika, alitoa taarifa huku akishutumu shambulio hili kama "kutojali maisha ya binadamu kwa ukali na bila huruma," akiita chuki ya baadhi ya watu kwa Wayahudi wote "uovu usioelezeka ambao lazima ukataliwe na kila Mwaaustralia."  Ni "dharau kwa mtindo wetu wa maisha kama Waaustralia" na "lazima ilaaniwe bila shaka," alisema mwakilishi wa maaskofu, wakitaka haki ifanyike haraka kwa waathiriwa. Shambulio hili, Askofu Mkuu Fisher alisisitiza, "lazima liongoze mabadiliko," kwa sababu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, hali ya chuki dhidi ya Wayahudi imeenea, na kusababisha vitisho, mgawanyiko, maandamano, na "kuhalalisha lugha ya uchochezi." Vitendo hivi "vimeongeza joto na labda kuchangia katika siasa kali." Yote haya, kulingana na Askofu Mkuu wa Sydney, "lazima yaishe.

Changamoto kwa Wakatoliki

Katikati ya mkasa huo, Askofu Mkuu hata hivyo alibainisha "athari za wema" katika "ujasiri wa ajabu wa polisi, wafanyakazi wa magari ya wagonjwa, na watoa huduma ya kwanza, pamoja na watazamaji; na katika ukarimu wa roho ya wale waliotoa msaada kwa walioathiriwa." Kisha alitoa rambirambi zake za dhati kwa jamii nzima ya Wayahudi na kuwahakikishia sala zake. "Tunawapenda majirani na marafiki zetu Wayahudi na lazima tufanye kila tuwezalo kuwalinda," Askofu Mkuu wa Sydney alihitimisha. Huku akihakikishia: "Jumuiya ya Wakatoliki itaongeza juhudi zake maradufu kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi kupitia elimu na mahubiri." Wakati huo huo, jumuiya ya Wakatoliki ya Sydney ilitoa huduma za kielimu na ushauri kwa majirani zake Wayahudi, ikiendelea kufanya ibada za kidini kwa ajili ya  wafu, waliojeruhiwa, na wale walioathiriwa na msiba huo.

Huzuni na Mshikamano kutoka Baraza la Maaskofu wa Italia

Jumatatu jioni, Desemba 2025 Baraza la  Maaskofu Italia (CEI) lilituma ujumbe ulioelezea rambirambi na kulaani shambulio la Sydney. “Tunaelezea huzuni na ghadhabu yetu kuhusu shambulio baya ambalo jana, kwenye Ufukwe wa Bondi, Australia, lilimwaga damu  katika siku kuu ya Hanukkah, na kusababisha vifo na majeraha mengi. Tunarudia kulaani kwetu vikali chuki dhidi ya Wayahudi, tukiwasihi Wakatoliki wa Italia kukataa aina zote za vurugu, za maneno na za kimwili.”

Kardinali Matteo Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Italia (CEI), na Askofu  Derio Olivero, Rais wa Tume ya Maaskofu kwa ajili ya  Uekumeni na Mazungumzo, katika ujumbe kwa Mkuu wa Kiyahudi  Arbib, Rais wa Bunge la Wakuu wa Kiyahudi wa Italia, na Noemi Di Segni, Rais wa Umoja wa Jumuiya za Wayahudi wa Italia. "Kwa kuwakabidhi waathiriwa wa shambulio hili lisilo na maana kwa upendo wa rehema wa Baba na kuomba uponyaji kwa wale wanaoteseka mwilini na rohoni, tunajiunga na jumuiya ya Wayahudi katika upendo na urafiki wetu," ujumbe unahitimisha.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Bonyeza hapa: Just click here

 

15 Desemba 2025, 16:30