Papa Leo kwa vijana:“karibu na Bwana kuna nafasi kwa kila mtu"
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 19 Desemba 2025 alikutana na wawakilishi wa Vijana kutoka Chama cha matendo ya vijana katoliki nchini Italia. Katika hotuba yake alionesha furaha ya kuwakaribisha. “Ni vizuri sana kukutana nanyi siku chache tu kabla ya Kuzaliwa kwa Bwana Yesu! Ninawasalimu kwa uchangamfu nyote, Rais wa Kitaifa, na Msaidizi Mkuu wa Kanisa, pamoja na timu ya kitaifa ya ACR, waelimishaji, na washirika waliwasindikiza. Ninawashukuru kwa dhati kwa shauku mnayoonesha na kushiriki nasi vizuri kweli, mnaposhuhudia uzuri wa imani na uzuri wa Utendaji wa Kikatoliki. Jina la chama chenu linaonesha utambulisho wake vizuri: ninyi ni wanafunzi wa Yesu, mashuhuda wa Injili yake, na wasindikizaji katika safari pamoja na Kanisa lote.”
Papa Leo alisisitiza kwamba wakati wa Majilio, hakika wameandaa mapango ya kuzaliwa kwa Yesu katika nyumba zao, shule, na parokia. Wanapomtazama Mtakatifu Yosefu na Maria, wachungaji, punda, na ng'ombe, wanaona jina la safari ya chama chao mwaka huu likitimia: "Kuna nafasi kwa kila mtu." “Ndiyo, karibu na Bwana, ambaye alifanyika mwanadamu ili kutuokoa, kuna nafasi kwa kila mtu! Anaweka nafasi kwa kila mtu, kila mtoto, kila mvulana, kila kijana, na kila mzee. Mwana wa Mungu anapokuja ulimwenguni, hapati nafasi ndani ya nyumba; anagonga mioyo yetu kama vile anavyofungua yake ili kuwakaribisha kila mtu kwa upendo.”
Kwa hivyo, Papa alisisitiza wanapoomba mbele ya “Pango la kuzaliwa kwa Yesu, waomba wawe kama malaika wanaotangaza utukufu na amani ya Mungu kwa wote. Amani hii ni kujitolea kwa kila mtu mwenye mapenzi mema, na hasa kwetu Wakristo, ambao tumeitwa sio tu kuwa wema, bali kuwa bora kila siku.” Papa amewashauri wawe kama watakatifu, kama Pier Giorgio Frassati, ambaye alikuwa mwanachama wa Matendo ya Kikatoliki ya vijana na kama Carlo Acutis.
“Ninakutia moyo kuiga shauku yao kwa Injili na kazi zao, zikiongozwa na upendo kila wakati. Kwa kutenda kama wao, ujumbe wenu wa amani utakuwa mkali, kwa sababu katika ushirika wa Yesu mtakuwa huru na wenye furaha kweli, tayari kutoa msaada kwa wengine, hasa wale wanaohitaji.”
Papa alifafanua kwamba, “kuzaliwa kwa Mfalme wa Amani (taz. Isaya 9:6) kunatufunulia maana halisi ya neno hili, amani, ambalo si tu kutokuwepo kwa vita, bali pia urafiki kati ya watu unaotokana na haki. Sote tunatamani amani hii kwa mataifa yaliyojeruhiwa na migogoro, lakini tukumbuke kwamba maelewano na heshima huanza katika mahusiano yetu ya kila siku, katika ishara na maneno tunayobadilishana nyumbani, katika parokia, na wanafunzi wenzako, na katika michezo.”
Kwa hivyo, kabla ya usiku mtakatifu wa Nole, Papa aliwaomba wafikirie mtu ambaye unaweza kufanya amani naye: itakuwa zawadi ya thamani zaidi kuliko ile unayoweza kununua madukani, kwa sababu amani ni zawadi ambayo inaweza kupatikana tu moyoni. Kufanya amani ni "Hatua ya Kikatoliki" bora kabisa, kwa sababu ni ishara inayotufanya tuwe mashuhuda wa Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.” Kwa kuhitimisha Papa alisema “ Kwa jina lake, ninawatakia matashi mea ninyi na wapendwa wenu na ninawabariki kwa moyo wote, pamoja na wavulana na wasichana wote wa Chama cha Matendo ya Kikatoliki. Papa aliwabariki baada ya sala ya Baba Yetu na kuwaomba msamaha wa kumsubiri.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku, bofya hapa tu:Just click here
