Papa Leo XIV: Bikira Maria wa Guadalupe: Mama wa Uinjilishaji Mpya: Haki na Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini inakumbusha kwamba, kwa mara ya kwanza Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, Mlinzi na Mwombezi wa Amerika ya Kusini pamoja na Ufilippin, iliadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 12 Desemba 2011 na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kama kumbukizi endelevu ya Jubilei ya uhuru kwa nchi nyingi za Amerika ya Kusini. Kunako mwaka 2014, Baba Mtakatifu Francisko akaonesha nia njema ya kutaka kuendeleza mapokeo ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumbukumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, kama kumbukumbu ya tukio hili miaka zaidi ya 50 iliyopita, wakati Mtakatifu Paulo VI alipoadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii ilipambwa na kuchukua mwelekeo wa utamadunisho kwa kuongozwa na vionjo vya watu wa Mungu kutoka Amerika ya Kusini, sehemu ya mchakato wa uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko akabahatika kutembelea Mexico kuanzia tarehe 12- 18 Februari 2016 pamoja na kutoa heshima zake kwa Bikira Maria, Mama Yetu wa Guadalupe. Aligusia kuhusu: Ibada ya Bikira Maria wa Guadalupe aliyokabidhiwa Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin kunako mwaka 1531 Fadhila zinazoujaza umaskini wa waamini; Utii na Madhabahu ya Bikira Maria wa Gudalupe. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin alikabidhiwa kazi ya kutangaza na kueneza Ibada ya Bikira Maria wa Guadalupe kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaopaswa kuzaa matunda, kwa kutia manukato katika maisha dhaifu ya binadamu, ili hatimaye, aweze kuzaa matendo mema, kukua katika wema na hivyo kuondokana na chuki pamoja na woga katika maisha. Bikira Maria akaweka picha yake kwenye kitambaa, matokeo na ishara iliyozaliwa kutokana na utii pamoja na imani. Mwenyezi Mungu akamkirimia Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin fadhila zinazoujaza umaskini wa binadamu, kwa njia ya matendo madogo madogo yanayosheheni upendo, kwa sura ya Mama Kanisa anayembeba Kristo Yesu tumboni mwake.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, tarehe 12 Desemba 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahubiri yake, alikazia sana dhamana na nafasi ya Ibada ya Bikira Maria wa Guadalupe, kuwa ni kiungo cha umoja na mshikamano wa udugu wa upendo unaofyekelea mbali chuki, kinzani na mipasuko ya kijamii. Kanisa limewakumbuka na kuwaombea watu wasiokuwa na makazi maalum; watu wanaoteseka na kusiginwa na baa la njaa na kwamba, Mwenyezi Mungu awajalie viongozi wa Serikali kujikita katika hekima, busara na haki. Kadiri ya Mapokeo, Bikira Maria anatambulikana kama “Mama wa fadhila ya upendo” anayesukumwa na Neno la Mungu kwenda kutangaza na kushuhudia ile furaha ya Injili, kama kielelezo cha zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hiki ndicho kiini cha utenzi wa Bikira Maria, maarufu kama “Magnificat.” Lk 1:43. Bikira Maria ni chemchemi ya furaha kama ilivyodhihirika kwenye ishara ya arusi ya Kana ya Galilaya, kielelezo cha upendo na uaminifu wa Mungu kwa watu wake. Mwinjili Yohane anamweka mbele ya macho ya waamini Bikira Maria anayeguswa na mahitaji ya wanandoa wapya waliotindikiwa na divai na hivyo kuomba huruma na upendo wa Yesu kwa niaba yao!
Divai ni ishara ya furaha na upendo, lakini wakati mwingine, mwanadamu anatindikiwa na divai, kumbe, katika muktadha huu, waamini wajifunze kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, atakayewaonesha uwepo wa Mungu katika safari ya maisha yao ishara ya: Imani, furaha, upendo na matumaini. Ujio wa Kristo Yesu ni chemchemi ya: Matumaini, upendo, furaha, huruma na utakaso katika maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Bikira Maria alikuwa ni mwaminifu kwa maisha na utume wake. Kumbe, wale wote wanaotaka kuwa ni watoto wa Bikira Maria hawana budi kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaofyekelea mbali chuki, uhasama na vita. Awafunde viongozi wa Serikali kwamba, uongozi ni huduma na kwamba, wanawajibika kulinda, kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.
Bikira Maria awasaidie vijana wa kizazi kipya, kuchota kutoka kwa Kristo Yesu nguvu na ujasiri wa kusimama kidete katika kutangaza na kushuhudia imani, wakiwa wamekita maisha yao katika kutekeleza mpango wa Mungu. Awasaidie kukita maisha yao katika kanuni maadili na utu wema; awaepushe ili wasitumbukie katika vitendo vya jinai, matumizi haramu ya dawa za kulevya; waendelee kuwa karibu na Mama Kanisa, ili awasaidie kupata malezi na majiundo bora zaidi. Bikira Maria awasaidie waamini kujenga umoja, upendo na mshikamano na kwamba, wasiwepo watu wanaopandikiza “ndago” za chuki, uhasama na vita. Baba Mtakatifu ameziombea familia ili ziweze kuimarika na kudumu kwani: Familia ni Kanisa dogo la nyumbani: Ni shule ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii. Familia ni tabernakulo ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ni mahali pa kufundana kuhusu umuhimu wa kumwilisha: huduma, upendo, ukarimu, msamaha na kuvumiliana. Hapa ni madhabahu ya sala, ibada, na tafakari ya kina ya Neno la Mungu; mambo msingi yanayowawezesha wanafamilia kujivika upendo, busara, rehema, utu wema, upole na unyenyekevu.
Tunu hizi msingi za maisha ya ndoa na familia kwa sasa ziko hatarini kutokana na taasisi ya familia kupigwa vita kana kwamba ni “Mbwa koko!! Lakini, Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa kusimama kidete kulinda, kudumisha na kushuhudia Injili ya familia! Huu wito na mwaliko wa kujizatiti katika ujenzi wa tunu msingi za familia kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa upendo, msamaha na maridhiano; mambo msingi katika maisha ya ndoa na familia. Waamini hawana budi kusimama kidete katika misingi ya imani, maadili na utu wema sanjari na kukataa kishawishi cha utengano na kinzani katika maisha ya ndoa na familia kwani waathirika wakuu ni watoto. Baba Mtakatifu Leo XIV alijikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe, ili wale anaowaongoza waweze kuzaa matunda mema; aweze kutumia vyema Ufunguo wa Ufalme wa Mungu aliokabidhiwa na Kristo Yesu katika kufungua na kufunga; aweze kusaidia kuwakomboa watu wa Mungu kutokana na mapungudu na udhaifu wa mwanadamu. Aendelee kuwa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, daima akiwa ameunganika na Kristo Yesu na kati ya watoto wa Kanisa, daima wakisafiri kwa pamoja kuelekea kwenye makao ya uzima wa milele, ambayo Kristo Yesu, amewaandalia waja wake.
