Tafuta

Papa Leo XIV: Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa wafungwa, maaskari magereza pamoja na wahudumu mbalimbali magerezani. Papa Leo XIV: Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa wafungwa, maaskari magereza pamoja na wahudumu mbalimbali magerezani.  (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV Jubilei ya Wafungwa na Askari Magereza: Utu, Heshima na Haki Msingi

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa wafungwa, maaskari magereza pamoja na wahudumu mbalimbali magerezani katika Dominika ya furaha inayosimikwa katika imani, matumaini na furaha ya kungojea. Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia kuhusu: Umuhimu wa Jubilei, Changamoto za magereza, wajibu wa kinabii magerezani, msamaha na matumaini kwa wafungwa., huku wakishikilia nanga ya matumaini katika maisha, kwa kufungua nyoyo zao kwa upana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anatekeleza shughuli za kichungaji kwa ajili ya wafungwa na mahabusu magerezani, ili kuonesha wasiwasi na ukaribu wa Mama Kanisa kwa wafungwa wanaoteseka magerezani. Hii ni dhamana na wajibu wa Kanisa zima kama sehemu ya utekelezaji wa utume wake unaomwilisha matendo ya huruma katika uhalisia wa maisha ya watu. Wakati wa hukumu ya mwisho, watu watahukumiwa kadiri walivyowatendea ndugu zake Kristo Yesu walio wadogo, na kwa kufanya vile, walimtendea Kristo Yesu mwenyewe. (Rej. Mt. 25:40) Kristo Yesu anajitambulisha kuwa kati ya watu wenye njaa, kiu, wageni, watu walio uchi, wagonjwa na wale walioko kifungoni. Baba Mtakatifu Francisko anasema taswira inayotolewa na magereza sehemu mbalimbali za dunia inaonesha ukweli wa jamii ambamo uchoyo, ubinafsi na utandawazi wa kutoguswa na mahangaiko ya jirani vinatawala. Kuna maamuzi ambayo yamefanywa kisheria lakini yanakiuka utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kujidai kukuza na kutaka kudumisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Matokeo yake ni watu kutengwa na kutupwa magerezani kama suluhu ya matatizo mbalimbali yanayoisonga jamii. Lakini ikumbukwe kwamba, kuna kiasi kikubwa cha rasilimali na utajiri wa nchi unaotumika kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa magerezani, ikilinganishwa na kiasi cha fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuchochea kasi ya maendeleo fungamani ya binadamu, ambayo yangewezesha idadi kubwa ya wafungwa kupata kazi na kipato halali badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya jinai na uvunjaji wa sheria. Ni rahisi sana kufumbia macho umuhimu wa elimu na malezi makini kwa jamii, sanjari na kushindwa kuona ukweli halisi wa matatizo na ukosefu wa haki na hivyo suluhu ya haraka inayoweza kupatikana ni ujenzi wa magereza, ili “kuwashikisha adabu wale wote wanaovunja sheria za nchi.”

Ni wajibu  wa Mama Kanisa kutunga na kutekeleza sera za huduma kwa wafungwa
Ni wajibu wa Mama Kanisa kutunga na kutekeleza sera za huduma kwa wafungwa   (ANSA)

Umefika wakati wa kutoa msukumo wa pekee kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu kwa raia wote. Kwa bahati mbaya, magereza mengi yameshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuweza kutoa mafunzo bora zaidi, ili wafungwa wanapomaliza adhabu zao na kutoka magerezani waweze kuwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani. Ni ukweli usioweza kufumbiwa macho kwamba, kuna uhaba mkubwa wa rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na changamoto za kijamii, kisaikolojia na kifamilia wanazokabiliana nazo wafungwa magerezani. Magereza yamegeuka kuwa ni mahali hatari sana, ambapo: Haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu vinasiginwa. Mafunzo makini kwa wafungwa yanaanza pale ambapo wafungwa wanapewa fursa ya kushiriki katika mchakato wa maendeleo, wanapopewa elimu makini na kufanyishwa kazi zenye staha. Yote haya lazima pia yazingatie huduma bora za afya kwa wafungwa pamoja na kuunda mazingira ambayo, wafungwa wataweza pia kushirikiana kwa karibu na raia wengine. Jamii inapaswa kuwa na mwelekeo tofauti sana kwa wafungwa magerezani, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali, ili kuboresha maisha yao, kama sehemu ya faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa bahati mbaya sana, wafungwa wamekuwa wakiangaliwa kwa “jicho la kengeza” kiasi kwamba, si rahisi sana kuthamini utu na heshima yao.

Papa Leo XIV: Utu, heshima na haki msingi za wafungwa
Papa Leo XIV: Utu, heshima na haki msingi za wafungwa   (@VATICAN MEDIA)

Wafungwa waonjeshwe matumaini na kupewa tena fursa ya kufanya kazi, ili kujipatia mahitaji yao msingi. Pale ambapo wafungwa baada ya kumaliza adhabu yao wanashindwa kutambuliwa utu na heshima yao, wanajikuta wakiwa kwenye majaribu makubwa kati ya kutafuta fursa za kazi, kutenda uhalifu pamoja na kujenga mazingira yasiokuwa salama. Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.

Magereza yasaidie kurekebisha tabia za wafungwa kwa kuwapatia mafunzo
Magereza yasaidie kurekebisha tabia za wafungwa kwa kuwapatia mafunzo   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa wafungwa, maaskari magereza pamoja na wahudumu mbalimbali magerezani, Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 14 Desemba 2025, maarufu kama “Dominica Gaudete” Yaani “Dominika ya Furaha”; kama antifona ya mwanzo inavyohimiza kwa kusema: furahini katika Bwana siku zote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu. Rej Flp 4:4,5 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya hitimisho la Jubilei ya wafungwa, askari magereza na wahudumu mbalimbali magerezani, iliyozinduliwa tarehe 12 Desemba 2025. Hii ni Dominika inayosimikwa katika imani, matumaini na furaha ya kungojea. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia kuhusu: Umuhimu wa Jubilei, Changamoto za magereza, wajibu wa kinabii magerezani, msamaha na matumaini kwa wafungwa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwenye Gereza kuu la Rebibbia tarehe 26 Desemba 2024 Baba Mtakatifu aliwataka wafungwa kushikilia kamba ya nanga ya matumaini na kamwe wasiiachie.

Magereza yasimame kwenye utamaduni wa upendo
Magereza yasimame kwenye utamaduni wa upendo   (@Vatican Media)

Pili, wahakikishe kwamba wanafungua nyoyo zao kwa upana zaidi. Na hatimaye, wamwombe Kristo Yesu awasaidie kutimiza mambo haya mawili katika maisha yao kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, wakiwa na imani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, daima wakiwa ni vyombo na mashuhuda wa haki na upendo katika mazingira walimokuwa wanaishi. Mama Kanisa anapokaribia kufunga Maadhimisho haya, waamini wanakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayewafungua na kuwakomboa watu wake. Baba Mtakatifu Leo XIV anakiri uwepo wa shida, changamoto na fursa magerezani, lakini hakuna sababu ya kukata wala kukatishwa tamaa kiasi kwamba, hata wakiteleza na kuanguka wawe na ujasiri wa kusimama na kuendelea kujikita katika mchakato wa haki, ambao daima ni mchakato wa kuponya na kupatanisha. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika: kuheshimiana, huruma na msamaha na hivyo, kutoa nafasi ya watu kukutana. Maadhimisho ya Jubilei ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika: Toba, wongofu wa ndani na msamaha, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu amekuja kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika huruma, kuwajali watu, hekima sanjari na wajibu wa jumuiya na taasisi mbalimbali.

Msongamano wa wafungwa magerezani ni changamoto pevu
Msongamano wa wafungwa magerezani ni changamoto pevu   (ANSA)

Mama Kanisa hana budi kuwa ni sauti ya kinabii, ili magereza yaweze kusimama kwenye utamaduni wa upendo. Mwaka wa Jubilei iwe ni fursa kwa wafungwa kuachiwa huru kama si kuwapunguzia muda wa kutumikia vifungo vyao na hivyo kuwa na imani ya kuweza kurejea tena ndani ya jamii, wakiwa ni watu wapya. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, nchi mbalimbali duniani litaweza kutekeleza changamoto hii na kuifanyia kazi, ili wafungwa waweze kuanza tena upya, kwa kujikita katika toba, wongofu wa ndani na msamaha kama ilivyokuwa kwa yule mwanamke mzinifu aliyeambia na Kristo Yesu enenda zako, wala usitende dhambi tena. Rej Yn 8:10-11. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kuna matatizo, changamoto na fursa nyingi magerezani: Msongamano wa wafungwa magerezani ni kati ya changamoto changamani kwa wakati huu, hali ambayo inachangia pia kudhohofisha maisha ya Askari magereza, kiasi hata cha kukosa imani. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, wafanyakazi na wafungwa wanaishi maisha yenye hadhi na utu wa kibinadamu, vinginevyo magereza yatageuka kuwa nyumba za chuki, uhasama na hali ya kulipizana kisasi; badala ya kuwa ni mahali pa kurekebisha tabia na mwenendo wa wafungwa. Kuna upungufu mkubwa wa huduma msingi kwa wafungwa, hali inayochangia pia kudhorota kwa afya ya akili pamoja na changamoto za kisaikolojia.

Wafungwa wanabeba madonda na makovu mwilini na nyoni mwao
Wafungwa wanabeba madonda na makovu mwilini na nyoni mwao   (@Vatican Media)

Wafungwa ni watu wanaobeba madonda na makovu makubwa katika maisha yao, kumbe wanapaswa kusaidiwa kuganga na kuponya madonda na makovu haya. Kuna ongezeko kubwa la wafungwa kukata tamaa na hivyo kutema zawadi ya maisha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu katika Injili anataka watu wote waokoke. Rej 1Tim 2:4. Hata katika changamoto na matatizo makubwa, waamini watambue kwamba, Mwenyezi Mungu yuko karibu, anatembea pamoja na waja wake na kwamba, jambo jema na lenye furaha litaweza kutokea tu siku moja!

Papa Jubilei Wafungwa
14 Desemba 2025, 15:37