Papa Leo XIV kwa vijana:Jengeni ulimwengu bora zaidi ya mlivyoukuta
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa huko Lebanon katika Ziara yake ya kwanza ya Kitume, Siku yake ya Pili nchini Lebanon ilikuwa na mikutano kadhaa ambapo Jumatatu jioni tarehe Mosi Desemba 2025 alikutana na kuwasalimu karibia vijana 15,000 kutoka si Lebano tu bali pia nchi za Siria na Iraq. Ni katika eneo la jukwaani lililowekwa katika Uwanja mbele ya Upatriaki wa Maronite wa Antiokia, alifurahi na, wakiwa wamevaa bendera za nchi yao huku wakipunga mkono pia na zile nyeupe na njano za Jiji la Vatican. Awali ya yote aliwasikiliza na hatimaye akajibu maswali yao, na pamoja nao akatoa ahadi ya amani, ambayo inafanana na nuru ya alfajiri inaoyoonekana katika usiku mweusi ambao ubinadamu unapitia.
Hata hivyo kabla ya Hotuba Kardinali Patriaki wa Antiokia wa Wamaroniti, Béchara Boutros Raï, alitoa hotuba ya kumkaribisha Papa Leo. Kanisa la Wamaroniti, lililopewa jina la mwanzilishi wake, Mtakatifu Maroun wa kujinyima, limekuwa katika ushirika kamili na Kiti cha Kitume. Uhusiano huu unafanywa upya katika maneno ya Kardinali: "Heri wapatanishi."Usemi huu wa kiinjili unasikika katika nchi, Lebanon ambapo Mashariki na Magharibi huingiliana katika mazungumzo ya tamaduni, imani, na ustaarabu. Nchi inawakaribisha wote, na hivyo kumkumbatia Papa Leo XIV, "Papa wa amani": kupitia "upole wa majeraha yake" badala ya "utukufu wa majumba yake," ikitoa kama zawadi "machozi ambayo yamekuwa lulu za matumaini" na milima yake "iliyobadilishwa kuwa madhabahu za maombi," mwisho huo unashughulikiwa hasa na vijana, ili "wingi uweze kuwa chanzo cha utajiri, " alisema Kardinali huyo.
Hotuba ya Papa na kujibu maswali ya vijana
Assalamu lakum! Alianza salamu Papa Leo XIV na kuongeza Wapendwa vijana wa Lebanon, amani iwe nanyi! Assalamu lakum! Hii ni salamu ya Yesu Mfufuka (taz. Yh 20:19), na inadumisha furaha ya mkutano wetu. Shauku tunayohisi mioyoni mwetu inaonyesha ukaribu wa upendo wa Mungu, unaotuunganisha pamoja kama kakana dada ili kushiriki imani yetu kwake na ushirika wetu sisi kwa sisi. Ninawashukuru nyote kwa mapokezi yenu ya joto, pamoja na Patriaki kwa maneno yake ya ukarimu. Ninatoa salamu maalum kwa vijana kutoka Syria na Iraq, na kwa Walebanon ambao wamerudi nyumbani kutoka nje ya nchi. Sote tumekusanyika hapa kusikilizana, na kumwomba Bwana avuvie maamuzi yetu ya baadaye. Katika suala hili, ushuhuda ambao Anthony, Maria, Elie na Joelle wameshirikisha sisi unafungua mioyo na akili zetu kweli.
Historia zao zinazungumzia ujasiri katikati ya mateso. Zinazungumzia matumaini mbele ya kukata tamaa, na amani ya ndani wakati wa vita. Wao ni kama nyota zinazong'aa angani usiku, zikitupatia mwanga wa miale ya kwanza ya alfajiri. Katika migogoro hii yote, wengi wetu tunaweza kutambua uzoefu wetu wenyewe, mzuri na mbaya. Historia ya Lebanon imeunganishwa na nyakati tukufu, lakini pia ina alama ya majeraha makubwa ambayo hupona polepole. Majeraha haya yana sababu zinazovuka mipaka ya kitaifa na yameunganishwa na mienendo tata sana ya kijamii na kisiasa.
![]()
Papa Leo XIV akiwapungia vijana mikono (@Vatican Media)
Papa leo XIV kadhalika alisema kwa vijana kuwa labda wanajuta kurithi ulimwengu uliogawanyika na vita na kuharibiwa na ukosefu wa haki wa kijamii. Lakini kuna tumaini, na kuna tumaini ndani yenu! Mna kipawa ambacho mara nyingi sisi watu wazima tunaonekana kupoteza. Mna tumaini! Mna muda! Mna muda zaidi wa kuota, kupanga na kutenda mema. Ninyi ni wakati uliopo, na wakati ujao tayari unaanza kuonekana mikononi mwenu. Mna shauku ya kubadilisha mkondo wa historia! Upinzani wa kweli dhidi ya uovu si uovu, bali upendo - upendo unaoweza kuponya majeraha ya mtu mwenyewe huku pia ukitunza majeraha ya wengine. Kujitolea kwa Anthony na Maria kwa wale wanaohitaji, uvumilivu wa Elie na ukarimu wa Joelle ni unabii wa mustakabali mpya utakaoletwa kupitia upatanisho na usaidizi wa pande zote.
Maneno ya Yesu yanatimizwa hivyo: “Heri walio wapole, maana hao watairithi nchi”; “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mt 5:5,9). Papa aliwaomba vijana kuishi katika nuru ya Injili, nanyi mtabarikiwa machoni pa Bwana! Nchi yenu, Lebanon, itastawi tena, ikiwa nzuri na imara kama mwerezi, ishara ya umoja na uzaaji wa watu. Mnajua vyema kwamba nguvu ya mwerezi iko katika mizizi yake, ambayo kwa kawaida huwa na ukubwa sawa na matawi yake. Idadi na nguvu ya matawi inalingana na idadi na nguvu ya mizizi yake.
Papa alisisitiza vile vile, kuwa mambo mengi mazuri tunayoyaona katika jamii ya Lebanon leo ni matokeo ya kazi ya unyenyekevu, iliyofichwa na ya uaminifu ya watu wengi wenye mapenzi mema, wa mizizi mingi mizuri, ambao hawataki kufanya tawi moja tu la mwerezi wa Lebanon likue, bali mti mzima, katika uzuri wake wote. Chukueni kutoka katika mizizi mizuri ya wale waliojitolea kuitumikia jamii bila kuitumia kwa maslahi yao wenyewe. Kwa kujitolea kwa ukarimu kwa haki, panga pamoja kwa ajili ya mustakabali wa amani na maendeleo. Kuwa chanzo cha matumaini ambacho nchi inakisubiri!
![]()
Kijana na vijana wengine wakishiriki Mkutano na Papa(@Vatican Media)
Katika suala hili, Papa alisema kuwa maswali yao yanaturuhusu kupanga njia ya kutenda ambayo hakika ni changamoto, lakini pia ya kusisimua. Papa alibainisha jinsi alivyoulizwa ni wapi pa kupata msingi imara wa kudumu katika kujitolea kwa amani. Akijibu Papa aliongeza, "msingi huu imara hauwezi kuwa wazo, mkataba au kanuni ya maadili tu. Kanuni ya kweli ya maisha mapya ni tumaini linalotoka juu: ni Kristo mwenyewe! Yesu alikufa na kufufuka tena kwa ajili ya wokovu wa wote. Yeye, Aliye Hai, ndiye msingi wa imani yetu; yeye ndiye shahidi wa huruma inayokomboa ulimwengu kutoka kwa kila uovu. Kama Mtakatifu Agostino alivyokumbuka, akimkumbusha Mtume Paulo, "ndani yake kuna amani yetu; kwake tunapata amani yetu" (Maelezo kuhusu Injili ya Yohane, LXXVII, 3). Amani si ya kweli ikiwa ni matokeo ya maslahi ya vyama. Ni ya dhati kabisa ninapowatendea wengine kile ambacho ningependa wanitendee (taz. Mt. 7:12). Kwa msukumo wa kweli, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema hakuna "amani bila haki, hakuna haki bila msamaha" (Ujumbe wa Siku ya 35 ya Amani Duniani, 1 Januari 2002). Hili ni kweli kabisa: msamaha husababisha haki, ambayo ndiyo msingi wa amani.
![]()
Papa Leo XIV kati ya vijana (@Vatican Media)
Ikiwa upendo una kikomo cha muda si upendo wa kweli
Swali la la pili linaweza pia kujibiwa kwa njia ile ile. Ni kweli kwamba tunaishi katika enzi ambapo mahusiano ya kibinafsi ni dhaifu na yanatumiwa kana kwamba ni vitu. Hata miongoni mwa vijana, maslahi binafsi wakati mwingine yanaweza kuchukua nafasi ya kuwaamini wengine, na kuwajali wengine hubadilishwa na faida ya mtu mwenyewe. Mitazamo kama hiyo hubadilisha hata ukweli mzuri kama urafiki na upendo kuwa kitu cha juu juu, na kuwachanganya na hisia ya kuridhika kwa ubinafsi. Ikiwa ubinafsi wetu uko katikati ya urafiki au uhusiano wa upendo, hauwezi kuzaa matunda. Vile vile, si upendo wa kweli ikiwa tunapenda kwa muda tu, mradi tu hisia hiyo hudumu. Ikiwa upendo una kikomo cha muda, si upendo wa kweli. Kinyume chake, urafiki ni wa kweli unapoweka "wewe" kabla ya "Mimi." Njia hii ya heshima na ya kukaribisha ya kuwaangalia wengine hutuwezesha kujenga "sisi" zaidi, iliyo wazi kwa jamii nzima na kwa wanadamu wote. Upendo ni wa kweli na unaweza kudumu milele tu unapoakisi utukufu wa milele wa Mungu - Mungu ambaye ni upendo (taz. 1 Yh 4:8). Mahusiano imara na yenye matunda hujengwa pamoja juu ya uaminifu wa pande zote, juu ya "milele" hii ambayo ni moyo inyaodunda kwa kila wito wa maisha ya familia na utakaso wa kidini.
Wapendwa vijana, ni nini kinachoonesha uwepo wa Mungu duniani kuliko kitu kingine chochote? Upendo, upendo! Upendo huzungumza lugha ya ulimwengu wote, kwa sababu huzungumza na kila moyo wa mwanadamu. Sio dhana tu, bali ni haistoria iliyofunuliwa katika maisha ya Yesu na watakatifu, wanaotusindikiza katika majaribu ya maisha. Fikiria vijana wengi ambao, kama nyinyi, hawajajiruhusu kukata tamaa na dhuluma na mifano hasi, hata ile inayopatikana ndani ya Kanisa. Badala yake, wamejaribu kutengeneza njia mpya katika kutafuta Ufalme wa Mungu na haki yake. Kwa kutumia nguvu mnayopokea kutoka kwa Kristo, jenga ulimwengu bora kuliko ule mliourithi! Kama vijana, mnaunda uhusiano na wengine kwa urahisi zaidi, hata wale kutoka asili tofauti za kitamaduni na kidini. Upyaishaji wa kweli ambao moyo wa kijana unatamani huanza na ishara za kila siku: kuwakaribisha wale walio karibu na mbali, kuwapa msaada marafiki na wakimbizi, na kuwasamehe maadui - kazi ngumu lakini muhimu.
Watakatifu wa Lebanon
Hebu tuangalie mifano mingi mizuri iliyowekwa na watakatifu! Fikirieni Pier Giorgio Frassati na Carlo Acutis, vijana wawili waliotangazwa kuwa watakatifu katika Mwaka huu wa Jubilei. Fikirieni watakatifu wengi wa Lebanon. Ni uzuri wa kipekee tunaouona katika maisha ya Mtakatifu Rafqa, alipovumilia miaka mingi ya mateso kutokana na magonjwa kwa nguvu na upole! Ni matendo mangapi ya huruma yaliyofanywa na Mwenyeheri Yakub El-Haddad alipowasaidia wale walioachwa na kusahaulika na kila mtu! Ni mwanga wenye nguvu gani unaotoka kwenye giza ambalo Mtakatifu Charbel alichagua kujiondoa, yeye ambaye amekuwa mmoja wa alama za Lebanon na ulimwenguni kote. Macho yake huoneshwa kila wakati kama yamefungwa, kana kwamba yanafunika fumbo kubwa zaidi. Kupitia macho ya Mtakatifu Charbel, ambayo yalifungwa ili kumwona Mungu wazi zaidi, tunaendelea kuona mwanga wa Mungu kwa uwazi zaidi. Wimbo uliowekwa kwake ni mzuri: "Enyi mlalao, na ambao macho yenu ni nuru kwa ajili yetu, kwenye kope zenu nafaka ya uvumba imechanua." Wapendwa vijana, mwanga wa Mungu na uwaangazie macho yenu na uvumba wa maombi uchanue.
![]()
Papa wakati anahutubia vijana(@Vatican Media)
“Kukuza urafiki wa kweli na Yesu na Maria"
Papa alisisitiza kuwa "Katika ulimwengu wa vikengeushi na majivuno, chukua muda kila siku kufumba macho na kumtazama Mungu pekee. Wakati mwingine anaonekana kimya au hayupo, lakini anajifunua kwa wale wanaomtafuta kimya kimya. Mnapojitahidi kutenda mema, ninawaomba muwe watafakari kama Mtakatifu Charbel kwa kuomba, kusoma Maandiko Matakatifu, kushiriki Misa Takatifu na kutumia muda katika ibada. Papa Benedikto XVI (mwaliko wa Benedetto XVI)aliwaambia Wakristo wa Mashariki ya Kati: “Ninawahimiza kukuza urafiki wa kweli na wa kudumu na Yesu kupitia nguvu ya sala” (Maombi ya Kitume ya Baada ya Sinodi ya Kikanisa ya Mashariki ya Kati, 63). Papa kwa njia hiyo alisema kwamba Maria, Mama wa Mungu na Mama yetu, hung’aa miongoni mwa watakatifu wote kama Mtakatifu sana. Vijana wengi hubeba rozari pamoja nao wakati wote, iwe mfukoni mwao, kwenye kifundo cha mkono au shingoni mwao. Ni vizuri sana kumtazama Yesu kupitia macho ya moyo wa Maria! Hata kutokea hapa, tulipo sasa hivi, ni vizuri sana kuinua macho yetu kwa Mama Yetu wa Lebanon kwa matumaini na uaminifu!"
![]()
Vijana walioshiriki Mkutano na Papa(@Vatican Media)
Papa Leo kwa kuhitimisha alisema “Wapendwa vijana, ningependa kuwaachieni sala rahisi na nzuri inayomhusu Mtakatifu Francis wa Assisi: Bwana, nifanyeni kuwa chombo cha amani yenu:palipo na chuki, niacheni nipande upendo; pale palipo na madhara, msamaha; pale palipo na ugomvi, umoja; pale palipo na shaka, imani; pale palipo na makosa, ukweli; pale palipo kukata tamaa, tumaini; pale palipo na huzuni, furaha; pale palipo na giza, nuru. Ombi hili na liwe hai kwa furaha ya Injili na shauku ya Kikristo mioyoni mwenu. “Shauku” inamaanisha “kuwa na Mungu katika nafsi yenu.” Bwana anapokaa ndani yetu, tumaini analotupatia huzaa matunda duniani. Kiukweli, tumaini ni fadhila “maskini”, kwa sababu linajitokeza mikono mitupu; mikono yake huwa huru kufungua milango inayoonekana imefungwa kutokana na uchovu, maumivu au kukata tamaa. Bwana atakuwa nanyi daima, na mnaweza kuwa na uhakika wa msaada wa Kanisa zima katika changamoto muhimu katika maisha yenu na katika historia ya nchi yenu pendwa. Ninawakabidhi kwa ulinzi wa Mama wa Mungu, Mama Yetu, ambaye kutoka kilele cha mlima huu anatazama maua haya mapya. Vijana wa Lebanon, kueni imara kama mierezi na mfanye dunia ichanue kwa matumaini! Papa alitoa baraka yake na kuongeza neno: “Grazie a tutti! Yaani Asante kwa Wote… Shukran!
Zawadi zilizotolewa kwa Papa Leo XIV(@Vatican Media)
Uwasilishaji wa 5D
Baada ya usomaji wa kifungu kutoka Injili ya Yohane, kulikuwa na uwasilishaji wa 5D: uzoefu wa kuzama unaopita mwelekeo rahisi wa pande tatu ili kuongeza msisimko mpya wa hisia kwenye onesho. Matukio ya furaha na uchangamfu kubadilishana na yale ya huzuni, yanayoakisiwa na dunia inayong'aa iliyobebwa na msichana mdogo, ambapo tawi la maua linatoka. Picha hii iliashiria mwanzo wa ushuhuda wa kwanza, ule wa Anthony na Maria, wanaojitolea baada ya mlipuko katika bandari ya Beirut. Walisimulia uharibifu uliojeruhi "sio mawe tu, bali pia mioyo." Hata hivyo, katikati ya kifusi, vijana wengi walitoa msaada bila kuuliza kuhusu utambulisho au asili ya wale waliowasaidia: "Tulikuwa wanadamu tu tukiwasaidia wanadamu wengine."
Yule anayechagua kubaki
Onesho lilipata uhai: njiwa anayeng'aa alipitishwa kutoka mkono hadi mkono miongoni mwa vijana jukwaani, huku mipira ya kung'aa kuanzia na mmoja ilianza kuongezeka mingine. Kisha mtumbwi yenye bendera ya Lebanon unaonekana: ni utangulizi wa ushuhuda wa Élie. "Ondoka, hamia, jiokoe": haya yalikuwa maneno yakirudia akilini mwake. Katika nchi ambayo hakuna siku moja ambayo mtu anajua kesho inaleta nini, matarajio ni machache. Kuporomoka kwa uchumi kumefuta akiba yake na ndoto zilizojengwa juu yake.
Licha ya uwezekano wa kuhamia Ufaransa, Élie alichagua kukaa: "Matatizo si sababu ya kukimbia, bali ni mwaliko wa kutafakari zaidi, kupenda zaidi, na kutenda ili kubadilisha kitu," hata kama mtu analazimika kuacha sehemu ya ustawi wake. "Ninawezaje kuondoka huku nchi yangu ikiteseka? Ninawezaje kuondoka huku nikiona kwamba Mungu anaendelea kutenda hapa duniani?" alijiuliza. Alipata jibu kwa imani: Lebanon haiwezi kuishi "bila kijana anayeamini." Na ndiyo maana yeye, kama wengine wengi, alichagua kubaki: "Kwa sababu, licha ya kila kitu, Lebanon bado inastahili kuota ndoto."
![]()
Mtumbwi na bendera ya Lebanon (@Vatican Media)
Marafiki wawili na familia inayokaribisha
Anayefuata ni Joelle, ambaye pia ni Mlebanoni. Hadithi yake inaanza katika msimu wa joto wa 2024, anapokaa miezi miwili nchini Ufaransa na jamii ya Taizé. Huko anakutana na Asil, mwenzake kijana Mwislamu ambaye anaendelea kuwasiliana naye hata baada ya kurudi nyumbani. Vita vinapozidi kuwa mbaya, simu ya Joelle inalia asubuhi moja: ni Asil, ambaye amebaki Ufaransa wakati huo, lakini anaogopa familia yake. "Mabomu ni ya vurugu... hawajui pa kwenda." Bila kusita, Joelle anajibu: "Waache waje nyumbani kwangu." Mama yake, ambaye alikuwa akinunua kitanda cha ziada, kwa bahati mbaya anakutana na familia ya Asil—"kana kwamba Mungu mwenyewe alikuwa amewaongoza hatua zao."
Kuanzia wakati huo, umbali hutoweka: tofauti za kidini si kikwazo tena. "Nilielewa ukweli muhimu: Mungu hakai tu katika makanisa au misikiti. Mungu hujidhihirisha wakati mioyo tofauti inapokutana na kupendana kama ndugu na dada," anasema Joelle. Roukaya, mama yake Asil, anapanda jukwaani pamoja naye na anasimulia vicheko na machozi walivyoshiriki kama familia moja. "Niligundua kwamba dini si kitu unachozungumzia: ni kitu unachoishi, katika upendo unaovuka mipaka yote."
Ahadi ya Amani na Vitendo
Maswali ya vijana kisha yalichochea hotuba ya Papa, ambayo ilifuatiwa na ibada ya "Ahadi ya Amani na Vitendo." Papa Leo XIV alianza: Wapendwa vijana wa Lebanon ninakuja kwenu na amani ya Kristo na nimeona mioyo yenu ikiwaka moto kwa imani. Je, mko tayari kuwa wapatanishi katika ulimwengu unaoteseka?
Vijana walijibu: Ee Bwana, tunaahidi kuwa wapatanishi vijana, wabebaji wa upatanisho mioyoni mwetu, tukipanda tumaini katika nchi yetu, tukiishi kama watoto wa nuru na tukishuhudia upendo wako kila mahali. Tusaidie kuwa chachu ya umoja, sauti ya haki, na wajenzi wa amani, katika Kanisa na katika taifa. Amina.
Baraka ya Papa na "asanteni nyote," iliyotamkwa kwa Kiitaliano, ilifunga mkutano, ambao ulimalizika kwa zawadi kwa Papa ya sanamu inayoonyesha Kristo Pantocrator, Bikira Maria na Mtakatifu Yohane Mbatizaji juu, na, chini, vijana waliojitolea kuzima ulimwengu kwa moto. Kukaa kwa Ppa Leo XIV nchini Lebanon kutaendelea hadi, Desemba 2. Kama ilivyopangwa na kRatiba ya Nyumba Kipapa, hakutakuwa Katekesi ya Jumatano, Desemba 3. Lakini Katekesi ya Jubilee itafanyika Jumamosi, tarehe 6 Desemba 2025.
![]()
Papa akutana na vijana wa Lebanon(@Vatican Media)
Asante kwa kusoma makala haya. Ukitaka kuendelea kupata taarifa mpya, tafadhali jiandikishe kwa jarida letu: cliccando qui
