Tafuta

Hija ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki imenogeshwa na kauli mbiu: Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja.” Hija ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki imenogeshwa na kauli mbiu: Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja.”  

Papa Leo XIV: Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana, Mwaka Wa Ukombozi 2033

Kristo Yesu amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele. Kaburi tupu na vitambaa vilivyolala ni ushuhuda wa Kristo Mfufuka. Kristo Yesu wa kwanza katika wafu ni msingi wa ufufuko wetu, tangu sasa kwa kufanywa haki roho yetu na baadaye kwa kuhuishwa miili yetu. Rej. KKK 638-658. Sherehe ya Pasaka ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na kifo, chemchemi ya maisha na mwanga wa imani na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele. Kaburi tupu na vitambaa vilivyolala ni ushuhuda wa Kristo Mfufuka. Kristo Yesu wa kwanza katika wafu ni msingi wa ufufuko wetu, tangu sasa kwa kufanywa haki roho yetu na baadaye kwa kuhuishwa miili yetu. Rej. KKK 638-658. Pasaka ya Bwana ni siku ya uumbaji mpya ambapo mwanadamu alirudishiwa sura na mfano wa Mungu alioupoteza kwa dhambi ya asili. Hali hii ndiyo inayoifanya Pasaka kuwa ni sikukuu ya sikukuu, sherehe ya sherehe. Mtakatifu Atanasi anaiita Dominika Kuu. Sio tena sikukuu ya Wayahudi ya kukumbuka kutolewa kwao utumwani Misri. Bali ni siku ya ulimwengu wote kukombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu ni kiini cha imani ya Kikristo, bila Fumbo hili, imani ya Kikristo ni utupu. Neno wa Mungu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amemkirimia mwanadamu ile sura na mfano wa Mungu baada ya kuchafuliwa na madoa ya dhambi na ukosefu wa utii.

Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana Kwa Wakristo Wote kila Mwaka
Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana Kwa Wakristo Wote kila Mwaka

Sherehe ya Pasaka ya Bwana ni ushindi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vita ya kidini na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Wakristo wanatangaza na kushuhudia Ufufuko wa Kristo dhidi ya kifo, kwani Neno wa Mungu ni chemchemi ya maisha na mwanga wa imani na matumaini yanayong’ara katika maisha na utume wa Kanisa na kwa namna ya pekee, katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini cha maisha, utume na tasaufi ya Kanisa la Kiorthodox. Fumbo la Ufufuko linaunganisha kwa namna ya pekee imani, maadili, ibada na sheria za Kanisa. Kutokana na imani hii, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa kwa furaha na imani timilifu, kwa kukumbuka Siku ya kwanza ya Juma, Yesu Kristo alipofufuka kutoka kwa wafu!

Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana kwa pamoja ni ushuhuda wenye mvuto
Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana kwa pamoja ni ushuhuda wenye mvuto   (ANSA)

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli anakaza kusema, Fumbo la Uumbaji linapata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kutangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka katika maisha yao ya kila siku hadi miisho ya dunia. Mama Kanisa anaendelea kuishi Fumbo la Msalaba ambalo linafumbatwa katika Ufufuko kwa kuwahamasisha waamini kuwa ni mwanga wa Kristo Mfufuka, ili kujenga na kuimarisha umoja, udugu, upendo na mshikamano kati ya watu, kwani kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Kristo amewaunganisha walimwengu kuwa wamoja! Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume linapaswa kujikita katika mchakato wa upatanisho, ili kupata maisha mapya yanayosimikwa katika ukweli, ili kuwa sehemu ya watu wa Mungu. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao kwani vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chchote kilichofanyika. Ndani mwake ndimo mlimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.

Utengano wa Wakristo unakwamisha ushuhuda wa Injili
Utengano wa Wakristo unakwamisha ushuhuda wa Injili   (AFP or licensors)

Hija ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki imenogeshwa na kauli mbiu: Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja.” Baba Mtakatifu leo XIV amekazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa uinjilishaji, Utangazaji na ushuhuda wa Injili yaani “Kerygma” kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya wokovu. Utengano kati ya Wakristo ni kikwazo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kutembea kwa pamoja katika hija kuelekea Maadhimisho ya Mwaka wa Ukombozi, 2033, huko mjini Yerusalemu, mahali ambapo Kristo Yesu aliadhimisha Karamu ya Mwisho, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, Siku ile ya Pentekoste, ili kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo huku akirejea kwenye kauli mbiu yake: "In illo Uno Unum" yaani "Ingawa Sisi Wakristo ni Wengi, Katika Kristo Mmoja Sisi ni Wamoja.”

Ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili ni kazi ya Roho Mtakatifu
Ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili ni kazi ya Roho Mtakatifu

Kumbukumbu ya Jubilei ya Miaka 1,700 ya Mtaguso Mkuu wa Nicea na Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana kwa Wakristo wote mwaka 2025 ni matendo makuu ya Mungu. Ni mwaliko hata kwa waamini wa dini mbalimbali duniani, kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu, chemchemi ya ujumbe wa matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo! Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia umuhimu wa Wakristo kujizatiti katika ujenzi wa umoja kamili. Kwa upande wake Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli amewataka Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kujikita kikamilifu katika mchakato wa haki na upatanisho ili kujenga na kudumisha amani ulimwenguni kote. “kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.” Efe 4:2-3.

Pasaka ya Bwana
01 Desemba 2025, 13:40