Tafuta

Papa Leo XIV anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wafiadini na mashupavu wa Injili, walioteswa na kuuwawa kwa sababu ya kukaa karibu na watu wao Papa Leo XIV anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wafiadini na mashupavu wa Injili, walioteswa na kuuwawa kwa sababu ya kukaa karibu na watu wao  

Papa Leo XIV: Mashuhuda wa Imani Kutoka Ufaransa na Hispania: Walifia Ukweli na Haki

Papa Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wafiadini na mashupavu wa Injili, walioteswa na kuuwawa kwa sababu ya kukaa karibu na watu wao na wakawa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni wenyeheri waliosadaka maisha na wakafa kutokana na chuki za kidini: Odium Fidei!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Wakristo wapya: “Sanguis martyrum semen Christianorum.” Waamini wanakumbushwa kwamba, hapa duniani ni wasafiri na wala hawana makazi ya kudumu, changamoto na mwaliko ni kujitahidi kujiandalia maisha ya uzima wa milele, watakapounganika na Mwenyezi Mungu. Kristo Yesu aligeuza mateso na kifo cha Msalaba kuwa ni ufunuo wa chemchemi ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa binadamu. Kumbe, mateso na kifo cha Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na ufuasi wa Kristo Yesu. Kwani ni kwa njia ya mateso na kifo, wafiadini wanashiriki pia Fumbo la Pasaka ya Kristo Yesu. Jambo la msingi kwa wafiadini ni kujitahidi kusamehe kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Ushuhuda wa imani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.Huu ni ushindi dhidi ya utamaduni wa kifo, chuki na uhasama. Ni ushuhuda wa upendo kwa Mungu na jirani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe. Tangu mwanzo wa Kanisa, kuna Wakristo ambao wameyamimina maisha yao kama ushuhuda wa imani. “Kifodini kinathaminiwa na Kanisa kuwa karama bora na uhakikisho mkuu wa upendo. Ingawa ni wachache wanaojaliwa neema hii ya kifodini, lakini wote wanapaswa wawe tayari kumkiri Kristo mbele ya watu, na kumfuata katika Njia ya Msalaba kati ya madhulumu ambayo hayakosekani kamwe katika Kanisa”. LG. 42.

Jipeni moyo kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu
Jipeni moyo kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu   (AFP or licensors)

Kardinali Jean-Claude Hollerich, S.J., Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Luxembourg, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 13 Desemba 2025 amewatangaza watumishi wa Mungu 54 kutoka nchini Ufaransa kuwa ni wenyeheri, Ibada ambayo imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Notre-Dame de Paris, nchini Ufaransa. Hawa ni mashuhuda wa imani kutoka katika Majimbo thelathini ya Kanisa Katoliki nchini Ufaransa, waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake kutokana na chuki za kidini “Odium fidei” nchini Ujerumani wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, yaani kati ya Mwaka 1944 hadi mwaka 1945. Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 14 Desemba 2025 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wafiadini na mashupavu wa Injili, walioteswa na kuuwawa kwa sababu ya kukaa karibu na watu wao na wakawa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mchakato wa kuwatangaza kuwa Wenyeheri, ulianzishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kunako mwaka 1988 na hatimaye kufikia hatima yake tarehe 22 Februari 2018 na Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 20 Juni 2025 akaridhia na kutambua ushuhuda wa imani ya wale walioteseka na hatimaye, wakasadaka maisha yao kama kielelezo cha imani na upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kujikita katika ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika haki na amani.

Ni mashuhuda waliofia ukweli na haki
Ni mashuhuda waliofia ukweli na haki   (ANSA)

Wakati huo huo Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Jumamosi tarehe 13 Desemba 2025 kwenye Jimbo Katoliki la Jaèn nchini Hispania, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Leo XIV amewatangaza watumishi wa Mungu 124 kuwa ni Wenyeheri! Hawa ni mashuhuda wa imani waliokuwa na ujasiri wa kuteseka hadi kufa kwa ajili ya upendo kwa ukweli na haki. Ni mashuhuda wa imani waliouwawa kutokana na chuki za kidini “Odium fidei” kati ya mwaka 1936 hadi mwaka 1938. Mashuhuda hawa wa imani wanaweza kugawanywa katika makundi makuu mawili.   Kundi la kwanza ni lile lililokuwa likiongozwa na Padre Emanuele Izquierdo, akiwa na wenzake 58 na kundi la pili lilikuwa chini ya uongozi wa Padre Antonio Montañés Chiquero akiwa ameandamana na wenzake 64, waliothubutu kukabiliana na mateso, wakawa tayari kusadaka maisha yao kwa ajili ya upendo kwa ukweli na haki, kwa ajili ya Kristo Yesu pamoja na ndugu zao. Hawa ni mashuhuda wa Injili kutoka Hispania, wanaodhihirisha kwamba, kwa hakika damu yao ni mbegu ya uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Fadhila ya nguvu iliwawezesha wafuasi wa Kristo Yesu nguvu ya kushinda kishawishi cha woga, huku wakitiwa moyo na maneno ya Kristo Yesu anayesema, “jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.” Yn 16:33. Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 14 Desemba 2025 amesema kwamba, anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa mapigano mapya yaliyoibuka hivi karibuni Mashariki wa DRC. Baba Mtakatifu ameonesha ukaribu wake kwa wale wote wanaoteseka, ametoa wito kwa wahusika katika vita hii kusitisha aina zote za vurugu, kinzani na vita na kuanza kujikita katika mazungumzo yanayojenga na kuheshimu mchakato wa amani unaondelea nchini DRC.

Papa Leo XIV: Kifo Dini
15 Desemba 2025, 14:12