Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 12 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na washiriki wa Jubilei ya Wanadiplomasia wa Italia. Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 12 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na washiriki wa Jubilei ya Wanadiplomasia wa Italia.  (@Vatican Media)

Jubilei Miaka 2025 ya Ukristo: Wanadiplomasia Mahujaji wa Matumaini

Papa Leo amekutana na kuzungumza na washiriki wa Jubilei ya Wanadiplomasia wa Italia, kwa kupita katika Lango la Jubilei; kwa kushiriki matumaini yaliyomo ndani mwao sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Injili ya matumaini kwa jirani zao, daima wakijikita katika kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo, mafao ya wengi, haki na amani. Hii ni diplomasia inayokita mizizi yake katika majadiliano yanayofumbata ukweli na uwazi hata pale ambapo kuna kinzani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Diplomasia ya Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, inatoa kipaumbele cha pekee kwa uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Vatican katika medani mbalimbali za Kimataifa. Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni haki za wote zisizoweza kukiukwa wala kutenguliwa. Ni za binadamu wote bila kujali: wakati, mahali au mhusika. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Haki ya kwanza kabisa ni uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale anapofariki dunia kadiri ya mpango wa Mungu. Mkazo umewekwa katika haki ya uhuru wa kidini inayofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu. Hiki ni kiini cha haki msingi kinachofumbata haki nyingine zote. Kuheshimu na kuthamini haki hii ni alama ya maendeleo halisi ya binadamu katika medani mbalimbali za maisha. Haki inakwenda sanjari na wajibu! Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kuheshimu haki msingi za binadamu, kichocheo muhimu sana cha amani na utulivu miongoni mwa binadamu. Kanisa linapenda kusimama kidete: kulinda na kudumisha haki na amani sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mwanga na chachu ya tunu msingi za Kiinjili! Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948.

Jubilei ya Wanadiplomasia wa Italia
Jubilei ya Wanadiplomasia wa Italia   (ANSA)

Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yanayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa maisha na uzima wa milele. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ni muda muafaka wa kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu; kwa kuweka kando mizigo ya zamani, na kupyaisha msukumo kuelelea siku zijazo; ili kusherehekea uwezekano wa mabadiliko katika maisha, kwa waamini kujitahidi kupyaisha utambulisho wao na kuwa jinsi walivyo, kwa njia ya imani, tayari kushuhudia ubora wao katika maisha ya kila siku. Itakumbukwa kwamba, Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 12 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na washiriki wa Jubilei ya Wanadiplomasia wa Italia, kwa kupita katika Lango la Jubilei; kwa kushiriki matumaini yaliyomo ndani mwao sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Injili ya matumaini kwa jirani zao, daima wakijikita katika kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo, mafao ya wengi, haki na amani.

Diplomasia inayokita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi
Diplomasia inayokita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi   (@Vatican Media)

Hii ni diplomasia inayokita mizizi yake katika majadiliano yanayofumbata ukweli na uwazi hata pale ambapo kuna: matatizo na kinzani, ili hatimaye kuweza kufikia suluhu ya kudumu. Huu ndio utume wa diplomasia unaopania pamoja na mambo mengine, kuleta suluhu kati ya watu au pande zinazosigana. Kristo Yesu ni shuhuda na chemchemi ya upatanisho, haki, amani na matumaini kwa watu wote wa Mungu. Kwa neno la Mungu, Kristo Yesu na kwa nguvu za Roho Mtakatifu anatekeleza majadiliano kati ya Mungu na wanadamu na kwamba, watu wanaweza kupata tajiriba hii kwa njia ya majadiliano, kwa kusikiliza na kuzungumza, kwa kujenga na kudumisha mahusiano katika maisha yao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, utamaduni pamoja na lugha mama, inawawezesha watu kuufahamu ulimwengu, tunu msingi za kijamii, mila na desturi na kwamba, maneno ni urithi wa jamii, unaoiwezesha jamii kujadiliana na kwamba, hii ni alama ya ukarimu, ushirikishwaji na udugu na kwamba, katika ngazi ya Kimataifa, lugha inaiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuweza kuzaa matunda ya ushirikiano na amani, kumbe kuna haja ya kujielimisha jinsi ya kuzungumza vyema, kwa kuwa watu waaminifu kwa njia ya maneno. Kimsingi mwamini Mkristo ni mtu wa maneno na kwamba, wakati wa Ubatizo, mwamini anaandikwa Ishara ya Msalaba: “effata” maana yake “funguka.” Huu ni muujiza uliotendwa na Kristo Yesu, unaomwezesha mtu kuweza kuzungumza na kwamba, hii ni sehemu muhimu sana ya utamaduni unaoenzi maisha katika familia na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, kuna haja ya kuelimisha ulimi, kwa kujikita katika shule ya kusikiliza na kujadiliana; kwa kusimamia ukweli na haki, ili kujenga amani na utulivu. Kumbe, kama Mabalozi wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza katika majadiliano.

Kardinali Parolin ameongoza Ibada ya Misa kwa Wanadiplomasia wa Italia
Kardinali Parolin ameongoza Ibada ya Misa kwa Wanadiplomasia wa Italia   (@Vatican Media)

Katika mazingira ya kimataifa yanayokumbwa na dhuluma na migogoro, Mabalozi hawa wanakumbushwa kwamba kinyume cha mazungumzo si kunyamaza, bali kukera. Ambapo ukimya huwafungua kusikiliza na kukaribisha sauti ya wale walio mbele yao, kosa kubwa ni mashambulizi ya maneno, vita vya maneno vilivyo na uwongo, propaganda, na unafiki mkubwa. Hii ni changamoto kwa Mabalozi hawa kuondokana na matangazo na hotuba zinazo chochea vita, vurugu na kinzani na hivyo kujikita zaidi na zaidi katika uaminifu na busara; kwa kutenda mema na hasa kwa kuchagua maneno yanayojenga ufahamu, kwa kushuhudia maneno yaliyo sawa, huku wakiwa tayari kusamehe makosa. Wale wanaochoshwa na mazungumzo wanachoka kutumainia amani.Mtakatifu Paulo VI katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, tarehe 4 Oktoba 1965, miaka 60 iliyopita alisema kinachounganisha ubinadamu, ni mkataba uliotiwa muhuri "na kiapo ambacho lazima kibadilishe historia ya siku zijazo ya ulimwengu: hakuna vita tena, hakuna vita tena! Amani, amani lazima iongoze hatima ya watu na wanadamu wote. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, amani ni wajibu unaowaunganisha wanadamu katika jitihada za pamoja za kutafuta haki. Amani ni fadhila inayo ambatana na maisha yote ya Kristo Yesu, tangu kuzaliwa kwake hadi, mateso, kifo na ufufuko wa wafu, yaani Fumbo la Pasaka. Amani ni wema wa uhakika na wa milele ambao watu wote wana utamani. Kwa hiyo, ili kulinda na kuendeleza amani ya kweli, Mabalozi hawa wanapaswa kujikita katika majadiliano na kuendelea kusoma alama za nyakati kulingana na kanuni hiyo ya utu wa Kikristo ambao ni msingi wa utamaduni wa Italia na Ulaya. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV aliwatakia mema katika huduma yao na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.

Jubilei ya Wanadiplomasia wa Italia: Majadiliano katika ukweli na uwazi
Jubilei ya Wanadiplomasia wa Italia: Majadiliano katika ukweli na uwazi   (ANSA)

Wakati huo huo, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahubiri yake kwa washiriki wa Jubilei ya Wanadiplomasia wa Italia, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumamosi tarehe 13 Desemba 2025, amekazia umuhimu wa Kipindi cha Majio katika maisha na utume wa Kanisa; kipindi mahusisi cha kupyaisha maisha ya kiroho, tayari kuambata na kutekeleza matamanio halali yanayopata chimbuko lake kutoka katika undani wa maisha, tayari kujitoa na kujisadaka kama moto unaofukuza giza katika maisha. Huu ni mwaliko wa kufuata mfano wa Yohane Mbatizaji, kwa kumwachia nafasi Mwenyezi Mungu ili aweze kutenda katika ukweli na haki na kwamba, ukweli unaangaza, unashauri, unafariji na wakati mwingine unauliza maswali, unahangaisha dhamiri nyofu, mambo ambayo walimwengu wanayatamani katika Ulimwengu mamboleo. Huu ni mwaliko kwa wanadiplomasia wa Italia kujikita katika majadiliano, ili kuleta haki na amani kwenye maeneo yenye vita, kinzani na migogoro; hali inayopelekea wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi zao wenyewe kama ilivyo katika Jimbo la Cabo Delgado, Msumbiji, DRC, Sudan ya Kusini na katika baadhi ya nchi zilizoko kwenye Ukanda wa Sahara. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete katika kulinda na kutetea ukweli, utu, heshima na haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika diplomasia, sheria za Kimataifa, Majadiliano katika ukweli na uwazi bila kusahau maisha ya sala, ili kutafuta na kujenga misingi ya haki, amani na maridhiano.

Wanadiplomasia wa Italia
13 Desemba 2025, 14:46