Papa Leo XIV: Pango la Noeli: Kielelezo cha Fumbo la Umwilisho
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” anafafanua kwa kina kuhusu: Pango la Noeli, Asili yake, Mchango wa Mtakatifu Francisko wa Assisi kuhusu Pango kama ishara ya uinjilishaji pamoja na alama za Pango la Noeli. Pango la Noeli ni mchakato unaojikita katika kueneza na kurithisha imani katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kristo Yesu. Huu ni mwaliko wa kutafakari, kuhisi na kuonja uwepo endelevu wa Mungu kwa binadamu; kuhisi na kuonja uwepo angavu wa Mungu kati pamoja na waja wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pango la Noeli ni mahali ambapo panaonesha alipozaliwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, alama hai ya Injili, mwaliko wa kutafakari Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwanadamu, ili kukutana na watu wote, ili kuwaonjesha huruma na upendo wake na hatimaye, waweze kuunganika pamoja naye. Kwa Waraka huu wa Kitume, uliochapishwa tarehe 1 Desemba 2019, Papa Francisko anapenda kuwahamasisha waamini kuendeleza Mapokeo ya kuandaa Pango la Noeli kwenye familia, mahali pa kazi, shuleni, hospitalini, magerezani na kwenye maeneo ya wazi, kama kielelezo cha ibada katika Fumbo la Umwilisho. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pango la kwanza la Noeli lilitengenezwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kunako tarehe 29 Novemba 1223 baada ya Papa Honorius III kupitisha Katiba ya Shirika lake. Pango hili la Noeli ni matokeo ya hija ya kiroho iliyofanywa na Mtakatifu Francisko wa Assisi mjini Bethlehemu pamoja na picha alizowahi kuona kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Alilitengeneza Pango la Noeli, Siku 15 kabla ya Sherehe ya Noeli kama kumbukumbu endelevu ya Fumbo la Umwilisho.
Ilikuwa ni tarehe 25 Desemba 1223 watawa Wafranciskani kutoka sehemu mbalimbali za dunia walipofika kwenye Madhabahu ya Wafranciskani huko Greccio. Pango likapambwa kwa uwepo wa mahujaji na wanyama mbalimbali na Ibada ya Misa Takatifu ikaadhimishwa Pangoni humo, ili kuonesha uhusiano wa dhati kati ya Fumbo la Umwilisho na Fumbo la Ekaristi Takatifu. Huu ndio ukuu na utakatifu wa Fumbo la Umwilisho, mwaliko kwa waamini kuamsha tena mshangao kwa unyenyekevu wa Mungu aliyefanyika Mtoto! Mti wa Noeli unawarejesha waamini kwenye kumbukumbu ya Sherehe ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu, zawadi ambayo inamuunganisha Mungu na binadamu na matokeo yake, Mwenyezi Mungu anawakirimia maisha yake. Mwanga unaopamba mti wa Noeli, ni mwaliko wa kumtambua Kristo Yesu kuwa ni mwanga angafu wa upendo anayeendelea kuangaza usiku wa giza katika maisha ya walimwengu. Waamini wanaalikwa kukutana na kumhudumia Kristo Yesu anayejitambulisha na ndugu zake maskini, wanyonge na wahitaji zaidi. Uwepo wa Mungu kwenye Pango la Noeli ni chachu ya mabadiliko makubwa yanayoleta matumaini pamoja na kukuza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, kuna haja ya kushirikishana na maskini utajiri na karama mbalimbali ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake, ili kujikita zaidi katika ujenzi wa utu na udugu wa kibinadamu ambamo, hakuna mtu anayetengwa wala kusukumizwa pembezoni mwa jamii.
Ni katika muktadha wa Pango la Noeli, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 13 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na wasanii wanaoshiriki katika Pango Hai la Noeli kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma, mahali ambapo pamehifadhiwa “Masalia ya Pango Takatifu la Mtoto Yesu” kumbe, kuna uhusiano mkubwa kati ya Kanisa hili na Bethlehemu alikozaliwa Mtoto Yesu. Huyu ni Mungu anayekuja na kujifunua kama chombo na mjumbe wa haki na amani, ili kumwezesha mwanadamu kushinda kiburi, umiliki wa mwanadamu na hatimaye, kumwongoza mwanadamu huyu katika utambulisho wake wa kweli. Huu ni mwaliko anasema Baba Mtakatifu Leo XIV kujiweka katika hija ya unyenyekevu na kuanza safari ya maisha ya kiroho inayosimikwa katika unyenyekevu, ili kwenda kumwona na hatimaye, kukutana na Bikira Maria pamoja na Mtakatifu Yosefu, katika hali ya umaskini, tayari kuanza mchakato wa maisha mapya, kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu. Wasanii wanaoshiriki katika Pango Hai la Noeli kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu ni mashuhuda wa tukio hili litakalopitia katika mitaa na viunga mbalimbali vya Jimbo kuu la Roma, alama ya furaha, ili kuonesha ule umuhimu wa kuwa kweli ni wafuasi wa Kristo Yesu, Mungu aliyefanyika mwili, Jua la haki linalochomoza ili “kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.” Lk 1:79.
Hii inawafanya leo na daima katika maisha na utume wao ili kuwa ni mahujaji wa matumaini; wabebaji wa faraja na maongozi kwa wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao: Watambue kwamba wao ni kwa ajili ya vijana na wazee pamoja na familia na wanaokutana nao njiani; kwa wale wanaofurahi na wanaoteseka, kwa wale walio pweke; kwa wale wanaohisi hamu kubwa ya kupenda na kupendwa, na kwa wale ambao, licha ya mapambano yao, wanaendelea kufanya kazi kwa kujitolea na uvumilivu ili kujenga ulimwengu bora.Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema Tukio la Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, ni ishara muhimu: Inayowakumbusha binadamu kwamba wao ni sehemu ya safari ya ajabu ya ukombozi na kwamba, kamwe hawakosi peke yao na, kama Mtakatifu Augustino alisema, "Mungu alifanyika mwanadamu ili mwanadamu apate kuwa Mungu, [...] ili mwanadamu, mwenyeji wa dunia, apate makao mbinguni" (Sermo 371, 1). Huu ni wito wa kusambaza waraka huu sanjari na kudumisha mila hii hai. Watambue kwamba, wao ni zawadi ya nuru kwa ulimwengu, ambao unahitaji sana kuendelea kujikita katika fadhila ya matumaini kwa kuwa na matumaini.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru na kuwapongeza Wasanii wa Mfuko wa Kipapa wa Utamaduni wa Elimu “Fondazione Pontificia Gravissimum Educationis – Cultura per l’Educazione” na Shirika la Wasalesian wa Don Bosco kwa mara nyingine tena kwa kuandaa Tamasha la Noeli kwa mwaka 2025 linalohusisha nyimbo za zamani ambazo zimegeuzwa kuwa ni sehemu ya sala za waamini na ambazo ziliimbwa kwa kichwa, kielelezo cha uwepo na ukaribu wao katika kugharimia mradi wa ujenzi wa shule nchini DRC, utakaowahudumia wanafunzi 350. Hiki ni kielelezo kwamba, utamaduni unaweza kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi, lakini zaidi maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kielelezo cha upendo wa Kimungu.
