Papa Leo XIV: Sala Kwa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema, kwa kuadhimisha katika mzunguko wa Mwaka wa Liturujia ya Kanisa, Kanisa linayaheshimu Mafumbo ya Kristo Yesu. Kanisa humheshimu kwa upendo wa pekee Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, ambaye ameunganika na Mwanaye wa pekee kwa namna isiyoweza kutengwa katika kazi ya wokovu. Tena ndani ya Bikira Maria, Kanisa hustahi na kutukuza tunda bora kabisa kuliko yote la ukombozi, na pia hutazama kwa fuaraha, kama katika mfano usio na doa yale anayoyatamani na kuyatumaini kwa ajili ya Kanisa zima. Rej. Lumen gentium, 103. Tangu mwaka 1953, viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki kila tarehe 8 Desemba, wamekuwa wakienda kutoa heshima zao kwa Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili iliyoko kati kati ya mji wa Roma. Bikira Maria alipata upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyemkirimia karama na neema nyingi ili aweze kuwa ni Mama wa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Karne kwa karne Mama Kanisa ametambua kwamba, Bikira Maria aliyejazwa neema na Mwenyezi Mungu, alikombolewa tangu mwanzo alipotungwa mimba! Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kuwasaidia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kielelezo cha imani tendaji! Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani, matumaini na mapendo, kwani amediriki kuwa ni mfuasi wa kwanza wa Kristo Yesu na chombo cha huduma makini kwa jirani zake; mtindo na mfumo wa maisha unaopaswa kutekelezwa na Mapadre kama sehemu ya majiundo yao ya awali na endelevu katika maisha na utume wa Kanisa.
Bikira Maria ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa watu wanaomkimbilia katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo Yesu ambaye pia ni: Njia, Ukweli na Uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma na upendo wa Mungu. Jumatatu tarehe 8 Desemba 2025 majira ya jioni, Baba Mtakatifu Leo XIV, amekwenda kutoa heshima yake kwa Sanamu ya Bikira Maria iliyoko kwenye “Uwanja wa Spagna” ulioko kati kati ya mji wa Roma na hatimaye, akasali mbele ya umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema akisema: Salamu, Ewe Bikira Maria, Furahi, kwani umejaa neema, katika neema ile ambayo, kama mwanga wa upole, huangaza wale ambao uwepo wa Mungu huwaangazia. Siri ilikuzingira tangu mwanzo, tangu tumboni mwa mama yako na ikaanza kutenda mambo makuu ndani yako, ambayo ilihitaji idhini yako hivi kwamba "ndiyo" ambayo iliongoza ndiyo nyingi katika maisha. Safi, Mama wa watu waaminifu, uwazi wako unamulika mji wa Roma kwa nuru ya milele, njia yako inatia manukato mitaa yake kuliko maua tunayokupa leo. Mahujaji wengi kutoka duniani kote, Ewe Mama Safi wametembea mitaa ya jiji hili la Roma katika historia na katika Maadhimisho ya Mwaka huu wa Jubilei. Ubinadamu uliojaribiwa, wakati mwingine kupondwa, mnyenyekevu kama nchi ambayo Mungu aliitengeneza kutoka kwayo, na ambayo Roho yake ya uzima haiachi kuvuma.
Tazama, Ee Bikira Maria, juu ya watoto wako wengi sana ambao tumaini ndani mwao halijafa bado! Alichokipanda Mwanao na kiote ndani yao, Yeye, Neno lililo hai ambaye katika kila mmoja anaomba kukua zaidi. Chukua mwili, uso, na sauti. Tumaini la Maadhimisho ya Jubilei na listawi Roma na kila pembe ya dunia, tumaini katika ulimwengu mpya ambao umetayarishwa na Mungu na ambayo wewe, Ee Bikira, ni kama chipukizi na mapambazuko yake. Sasa milango mitakatifu, na milango mingine ya nyumba ifunguke , ili chemchemi za amani ambapo utu unaweza kusitawi tena, elimu ya kutotumia nguvu na mabavu inaweza kufundishwa, na watu wanaweza kujifunza sanaa ya upatanisho. Ufalme wa Mungu uje, Ufalme mpya uliyotarajia na ambao ulijifungua kabisa, kama: mtoto, kama msichana, na kama Mama wa Kanisa changa. Hamasisha maarifa mapya katika Kanisa linalosafiri Roma na katika Makanisa ambayo katika kila muktadha hukusanyika kwa furaha na matumaini, huzuni na uchungu ya watu wa zama zetu, hasa maskini, na wale wote wanaoteseka. Ubatizo bado uzae watu watakatifu na safi, walioitwa kuwa viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo, Mwili unaotenda, kufariji, kupatanisha, na kubadilisha mji wa duniani ambamo Mji wa Mungu unatayarishwa. Utuombee, ukipambana na mabadiliko ambayo yanaonekana kutukuta hatujajiandaa na hatuna nguvu. Himiza ndoto, maono, na ujasiri, wewe ambaye unajua zaidi ya mtu mwingine yeyote kwamba, hakuna lisilowezekana mbele ya Mungu, na wakati huohuo Mwenyezi Mungu hafanyi chochote peke yake. Tuongoze tusonge mbele, kwa haraka ambayo iliwahi kusonga hatua zako kuelekea kwa binamu yako Elizabeth na hofu uliyo kuwa nayo kama mkimbizi na msafiri. Ndiyo umebarikiwa kubarikiwa, lakini kati ya wanawake wote, mfuasi wa kwanza wa Mwanao, Mama wa Mungu pamoja nasi. Utusaidie kuwa Kanisa daima na miongoni mwa watu, “chachu” katika unga wa ubinadamu unaolilia haki na matumaini. Safi kabisa, mwanamke wa uzuri usio na mwisho, tunza mji huu wa Roma, wa ubinadamu huu. Mwoneshe Yesu kwake, mlete kwa Yesu, mpeleke kwa Kristo Yesu. AMINA.
