Papa Leo XIV: Tamasha la Muziki Pamoja na Maskini 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV “Dilexi te” Yaani: “Nimekupenda” Kuhusu Upendo kwa Maskini. Ufu 3:9; unakazia upendo wa Kanisa kwa maskini, kama njia ya utakatifu inayowawezesha waamini kumtambua Kristo Yesu kati ya maskini na wanaoteseka, kiini cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambao watakatifu wengi walitamani kuuiga. Mtakatifu Francisko wa Assis alijisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, akawa ni chanzo cha mabadiliko katika historia mamboleo na kwamba, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wakachukua huduma kwa maskini kuwa ni sehemu ya tasaufi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kwamba, upendeleo kwa maskini ni kiini cha upyaisho wa Kanisa na jamii katika ujumla wake, changamoto na mwaliko kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini. Kuna mifumo mbalimbali ya umaskini: maskini wanaokosa mahitaji msingi; maskini wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii; maskini wa kiutu, kimaadili na kitamaduni; watu dhaifu na maskini wanaonyimwa haki, uhuru na fursa na kwamba, ndio maana Umoja Mataifa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu Ifikapo Mwaka 2030 umeelekeza kutokomeza umaskini wa aina zote kila mahali. Kwa hakika kiwango cha umaskini kinaendelea kuongezeka maradufu. Kuna itikadi ya maamuzi mbele inayodharirisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni changamoto kwa waamini kurejea tena katika Maandiko Matakatifu na kwamba, huduma kwa maskini ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu.
Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo na amejifunua kwa walimwengu kwa njia ya Mtoto mchanga aliyelazwa katika hori ya kulia wanyama. Upendeleo wa Mungu kwa maskini ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa maskini na binadamu dhaifu anayesubiri kufunguliwa kwa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, udugu wa kibinadamu na mshikamano na kwamba, maskini wanayo nafasi ya pekee katika moyo wa Mungu, mwaliko kwa Mama Kanisa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaonyanyaswa na kudhulumiwa. Kimsingi, historia nzima ya ukombozi inasimikwa katika uwepo wa maskini kama inavyojionesha kwenye historia ya Fumbo la Umwilisho, katika maisha. Ni Masiha maskini na kwa ajili ya maskini, aliyetumwa na Baba yake wa mbinguni kuwatangazia maskini Habari Njema. Katika Agano la Kale, umaskini ulifungamanishwa na dhambi binafsi, lakini Kristo Yesu katika Agano Jipya anaonesha kwamba, maskini wana nafasi ya pekee miongoni mwa watu wa Mungu. Kimsingi, huruma kwa maskini imeoneshwa kwa kina katika Maandiko Matakatifu na kwamba, Mungu ni upendo ndiyo maana Mama Kanisa anakazia matendo ya huruma: kiroho na kimwili na kama Kristo Yesu anavyobainisha kwenye Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu na kwamba, hiki ni kielelezo cha imani tendaji kama Mwinjili Luka anavyosimulia katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Upendo kwa maskini ni ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, mwaliko kwa waamini kuiga mfano huu mzuri, utakao zaa utajiri mkubwa.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitamani sana kuona Kanisa maskini na kwa ajili ya maskini; Kanisa linalojisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini: “Diakonia”, kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu, kiasi hata cha kuyamimina maisha, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Stefano, Shuhuda wa imani na huduma ya upendo kwa maskini. Mtakatifu Laurenti, Shemasi, ndiye aliyewaonesha maskini kuwa ni hazina na utajiri wa Kanisa. Ni kosa la jinai kwa watu kujitajirisha kutokana na umaskini wa watu. Katika maisha na utume wao, Mababa wa Kanisa daima wamekazia huduma ya upendo kwa maskini, kwa kuwatambua kwamba, wao ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili wa Kristo. Daima Kanisa limejipambanua kuwa ni Mama wa maskini, mahali pa ukarimu na haki. Tangu mwanzo, Kanisa lilijikita katika kutoa huduma makini kwa jamii, kama kielelezo cha imani tendaji, kwani imani bila matendo hiyo imekufa. Rej. Yak 2:17. Waamini wajibidiishe kukutana na Kristo Yesu kati ya maskini wanaosimama mlangoni mwa Kanisa na kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya upendo na haki, viwasukume waamini kuipenda Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na hivyo kuwa makini kwa maskini. Upendo ni kielelezo cha Ibada ya kweli na huduma kwa maskini na ndiyo maana ya haki jamii na kwamba huduma kwa maskini ni kuwarejeshea maskini haki yao na kwa Mtakatifu Augustino, maskini ni Sakramenti ya uwapo wa Kristo Yesu na kuwa upendo na ukarimu kwa maskini ni chemchemi ya baraka na neema kutoka kwa Mungu. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani unaofumbata huduma kwa maskini. Kanisa katika maisha na utume wake, halina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, ili kweli Kanisa liwe ni maskini kwa ajili ya maskini, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Injili.
Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali, mali na kipato; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wanapaswa kuwajali, kuwathamini na kuwapenda maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama afanyavyo mama mzazi kwa watoto wake. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV kama sehemu ya maandalizi ya Sherehe za Noeli, yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, anayejiweka kati ya waja wake na kujifanya mtoto na maskini, kielelezo cha upendo wa Kimungu unaomwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, amekutana na kuzungumza na waandaaji pamoja na wasanii wa Tamasha la Muziki Pamoja na Maskini kwa mwaka 2025. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema: “Mungu ni upendo.” 1Yn 4:16, mwaliko kwa waamini kujifunza jinsi Mungu anavyopenda na hivyo waamini kujitahidi kumwilisha Amri kuu ya upendo katika uhalisia wa maisha yao. Tamasha la Muziki Pamoja na Maskini kwa mwaka 2025, ni kielelezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu pamoja na maskini na wakumbuke daima maneno ya Kristo Yesu aliyesema: “Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.” Mt 25:40 na kwa kufanya hivi ni kuendelea kupandikiza mbegu ya upendo kwa wale wenye njaa na kiu; wasiokuwa na mavazi, wagonjwa, wageni na wafungwa wanaopendwa na kuthaminiwa na Kristo Yesu. Maskini ni shule ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Ni katika muktadha huu, Tamasha la Muziki Pamoja na Maskini ni tukio linalobeba uzito wa pekee na kwamba, muziki ni tajiriba ya maisha ya Kikristo, ni Sala na Zawadi maalum kutoka kwa Mungu kwa ajili ya mwanadamu. Wanamuziki wanapaswa kuimba kwa sanaa inayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, kwani muziki ni kielelezo pia cha upendo, utu na udugu wa kibinadamu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru viongozi, waandaaji, wasanii na wadhamini wanaowezesha kufanikisha kwa Tamasha la Muziki Pamoja na Maskini kwa Mwaka 2025.
