Papa Leo XIV: Umuhimu wa Akiolojia ya Kikristo Katika Maisha na Utume wa Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Akiolojia ni ujuzi wa kuvutia unaohusisha uchunguzi wa kisayansi wa historia ya binadamu na historia ya awali kupitia uchimbaji na uchanganuzi wa mabaki, miundo, na mabaki mengine ya kimwili. Ni nyanja ya taaluma nyingi inayochanganya vipengele vya anthropolojia, jiolojia, kemia na historia ili kuunganisha fumbo la maisha yetu ya zamani. Katika nguvu kazi ya kisasa, akiolojia ina jukumu muhimu katika kuelewa na kuhifadhi urithi wetu wa kitamaduni. Umuhimu wa akiolojia unaenea zaidi ya taasisi za elimu na utafiti. Ina athari kubwa kwa kazi na tasnia mbalimbali. Katika usimamizi wa rasilimali za kitamaduni, wanaakiolojia huchangia miradi ya maendeleo ya ardhi kwa kutathmini maeneo yanayoweza kutokea ya kiakiolojia na kuhakikisha ulinzi wake. Makavazi na mashirika ya urithi hutegemea wanaakiolojia kuratibu na kufasiri mikusanyo yao, kutoa maarifa muhimu katika historia yetu iliyoshirikishwa. Katika taaluma, wanaakiolojia huchangia katika kukuza maarifa na uelewa wa ustaarabu wa kale. Kujua ujuzi wa akiolojia kunaweza kufungua milango kwa fursa za kazi zenye kusisimua na kuathiri vyema ukuaji wa kazi na mafanikio. Kwa ufupi kabisa, Akiolojia ya Kikristo ni utafiti wa kisayansi wa historia ya binadamu na historia ya awali kupitia uchimbaji na uchambuzi wa mabaki, miundo, na mabaki mengine ya kimwili. Inasaidia kuelewa tamaduni zilizopita, jamii, na maendeleo ya ustaarabu wa binadamu mintarafu sayansi ya historia, imani, maisha, utume na utambulisho wa Mama Kanisa.
Baba Mtakatifu Pio XI katika Barua yake Binafsi, “Motu Proprio” ya tarehe 11 Desemba 1925, alikumbusha kuhusu: umuhimu wa utunzaji wa Akiolojia ya Kikristo na kwamba, kulikuwa na haja ya kulinda na kutunza makaburi ya Wakristo; Makumbusho na Mambokale; Makanisa makuu pamoja na Liturujia. Aliwakumbuka waasisi wa Akiolojia ya Kikristo hawa ni: Giovanni Battista de Rossi na mtafiti nguri Antonio Bosio. Papa Pio XI akaunganisha Tume ya Akiolojia Takatifu pamoja na Taasisi ya Kipapa ya Akiolojia, ili kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya kujikita katika tafiti makini katika makumbusho ya Kikristo. Imekwisha gota miaka mia moja tangu Papa Pio XI alipoanzisha Taasisi ya Kipapa ya Akiolojia, ambayo imeweza kujikita katika tafiti za Sayansi ya historia, imani na utambulisho wa Kikristo. Kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Kipapa ya Akiolojia, Baba Mtakatifu Leo XVI Alhamisi tarehe 11 Desemba 2025 amechapisha Waraka wa Kitume ujulikanao kama: “On the Importance of Archaeology on the Occasion of the Centenary of The Pontifical Institute of Christian Archaeology” yaani “Umuhimu wa Akiolojia kwenye Maadhimisho ya Miaka mia moja ya Taasisi ya Kipapa ya Akiolojia ya Kikristo.” Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Taasisi ya Kipapa ya Akiolojia na hivyo kutumia fursa hii kufafanua mambo msingi yaliyomo kwenye Waraka huu wa Kitume.
Kwanza, fundisho la "Akiolojia ya Kikristo," ielewe kama somo la makaburi ya karne za kwanza za Ukristo, ina hali yake ya kielimu kwa sababu ya mwelekeo wake mahususi wa mpangilio wa matukio, kihistoria, na mada. Mafundisho haya yanajumuishwa ndani ya mawanda ya akiolojia ya zama za kati kwa kukazianidhamu pamoja kivumishi “Kikisto.” Hakikusudiwi kuelezea mtazamo wa kidini, lakini inastahili nidhamu yenyewe na hadhi yake ya kisayansi na kitaaluma. Zaidi ya hayo, akiolojia ya Kikristo ni fani ya masomo ambayo inahusu kipindi cha kihistoria cha Kanisa lililoungana, na kwa hiyo inaweza kuwa chombo muhimu cha majaribio ya kiekumene. Hakika, maungamo mbalimbali yanaweza kutambua asili yao ya kawaida kwa njia ya kujifunza mambo ya kale ya Kikristo na hivyo kukuza hamu ya ushirika kamili. Katika suala hili, anasema Baba Mtakatifu Leo XIV aliweza kupata tajiriba wakati wa hija yake ya kitume nchini Uturuki alipokuwa katika mji wa kale İznik, Nicea nchini Uturuki, kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 170 tangu Mababa wa Kanisa walipoandhimisha Mtaguso wa kwanza wa kiekumene, Nicea, kwa uwepo na ushiriki wa viongozi mbalimbali wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo. Uwepo wa mabaki ya majengo ya kale ya Kikristo ulikuwa unawatia moyo wote waliohudhuria. Katika mada hii, Baba Mtakatifu anasema alifurahi sana kushiriki katika semina iliyoandaliwa kwa pamoja na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawahimiza wasomi kuendelea kujikita katika “Diplomasia ya utamaduni” ili kuvuka mipaka ya nchi, maamuzi mbele na kuanza kujikita katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, ili kukuza haki, amani na utulivu. Hii ilikuwa nichangamoto pevu wakati ule wa Mwaka 1925 Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Jubilei ya amani na wakati huu katika maadhimisho ya Jubilei ya Matumaini. Kwa hakika walimwengu wana kiu ya utamaduni wa diplomasia ya utamaduni ili kuondokana na maamuzi mbele, ili kukuza na kudumisha amani na matumaini, kama wachungaji bora kwa kujikita katika sayansi, huku wakitambua kwamba, wao ni watangazaji na mashuhuda wa amani. Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, anasema: "Ulaya inamhitaji Kristo na Injili, kwa maana hii hapa ndio mizizi ya watu wake wote.” Hii pia ni changamoto kwa Taasisi hii kusikiliza na kuutekeleza ujumbe huu. Miongoni mwa mizizi ya jamii na Mataifa ya Ulaya ni hakika Ukristo, pamoja na vyanzo vyake vya fasihi na kumbukumbu; na kazi ya wanaakiolojia ni jibu kwa rufaa ambayo Baba Mtakatifu Leo XIV ameifanyia rejea hivi punde. Baba Mtakatifu Leo XIV anaitaka Taasisi ya Kipapa ya Akiolojia ya Kikristo iendeleze kwa nguvu mpya huduma yake yenye thamani kwa Kanisa na utamaduni na hatimaye akayakabidhi matumaini yake kwa maombezi ya Bikira Maria na kuwapatia baraka zake za kitume.
