Tafuta

Papa Leo XIV: Mfumo wa Habari wa Ulinzi na Usalama Nchini Italia (SISR) kwanza kabisa, lazima utoe kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Papa Leo XIV: Mfumo wa Habari wa Ulinzi na Usalama Nchini Italia (SISR) kwanza kabisa, lazima utoe kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu.  (ANSA)

Papa Leo XIV: Vyombo vya Ulinzi na Usalama: Utu, Haki na Mafao ya Wengi

Papa Leo XIV, tarehe 12 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfumo wa Habari wa Ulinzi na Usalama Nchini Italia (SISR) na kukazia umuhimu wa kuheshimu utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kanuni madili ya mawasiliano. Mfumo wa Habari wa Ulinzi na Usalama Nchini Italia (SISR) kwanza kabisa, lazima utoe kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu bila kusahau kanuni maadili na utu wema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfumo wa Habari wa Ulinzi na Usalama Nchini Italia (SISR) ni muunganiko wa taasisi za Italia (kama vile DIS, AISE, AISI) zinazofanya kazi kulinda nchi dhidi ya vitisho vya ndani na nje, kwa kutoa habari muhimu kwa serikali ili kuweza kuchukua maamuzi ya kimkakati, kushughulika na ujasusi, vitendo vya kigaidi, usalama wa mtandao; ulinzi na usalama kwa masilahi ya kitaifa, kupitia mageuzi yaliyoletwa na Sheria namba: 1/20074. Mfumo wa Habari wa Ulinzi na Usalama Nchini Italia (SISR), ulianzishwa kunako mwaka 1925, miaka mia moja iliyopita, kwa kuweka mfumo bora wa ulinzi na usalama wa nchi ya Italia. Huu ni mfumo unaohitaji zaidi: umahiri, uwazi na usiri ili kuweza kufuatilia kila siku matukio yanayo hatarisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kujikita katika mchakato wa kulinda amani. Hii ni kazi inayodai usiri mkubwa, ni kazi ya hatari, lakini ni muhimu ili kuweza kubainisha vitisho vinavyoweza kuikumba jamii. Katika kipindi cha miaka mia hii, mengi yamebadilika: ujuzi na zana zimeboreshwa zaidi, ili kuweza kupambana na changamoto mambo leo. Baba Mtakatifu Leo XIV, Ijumaa tarehe 12 Desemba 2025 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfumo wa Habari wa Ulinzi na Usalama Nchini Italia (SISR) na kukazia umuhimu wa kuheshimu utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kanuni madili ya mawasiliano. Mfumo wa Habari wa Ulinzi na Usalama Nchini Italia (SISR) kwanza kabisa, lazima utoe kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Vyombo vya ulinzi na usalama: Vizingatie: Utu, heshima na haki msingi
Vyombo vya ulinzi na usalama: Vizingatie: Utu, heshima na haki msingi   (ANSA)

Wakati mwingine katika ulinzi na usalama kwa kutafuta ustawi na mafao ya wengi kuna hatari ya kusahau kanuni maadili na utu wema na hivyo inakuwa ni vigumu kuweza kupata usawa. Kama Tume ya Ulaya ya Demokrasia kupitia Sheria inasema, Taasisi na mashirika ya ulinzi na usalama mara nyingi yanahitaji kukusanya taarifa kuhusu watu binafsi na hivyo kuwa na athari kubwa kwa haki msingi za mtu binafsi. Kwa hiyo ni muhimu anasema Baba Mtakatifu Leo XIV kuweka mipaka, kwa kuzingatia hadhi ya mtu binafsi, na kubaki macho dhidi ya vishawishi ambavyo kazi kama yao inavyoweka wazi.  Wahakikishe kwamba, matendo yao yanalingana na kuzingatia mafao ya wengi kwa kuzingatia kwamba ulinzi na usalama wa taifa daima unahakikisha haki za watu binafsi, maisha yao ya kibinafsi na ya kifamilia; wazingatie uhuru wa dhamiri na habari pamoja na haki ya kuhukumiwa kwa haki. Katika suala hili, shughuli za Huduma lazima zidhibitiwe na sheria, zitangazwe na kuchapishwa ipasavyo, kwa kuzingatia uangalizi na uchunguzi wa mahakama, na bajeti lazima zichunguzwe kwa umma na kwa uwazi.

Kanisa pia ni muathirika wa vitendo vya kijasusi katika baadhi ya nchi
Kanisa pia ni muathirika wa vitendo vya kijasusi katika baadhi ya nchi   (ANSA)

Pili, Baba Mtakatifu anawataka wajumbe hawa kuheshimu na kuzingatia kanuni maadili na utu wema wa mawasiliano kwa kutambua kwamba, kumekuwepo na mabadiliko na mapinduzi makubwa kwenye Ulimwengu wa kidijitali na kwamba, hii sasa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu katika mchakato wa mabadilishano ya habari na mwingiliano wa kijamii. Maendeleo na mwingiliano wa habari umetoa mwanya mkubwa kwa watu kuweza kuwasiliana, lakini wakati huo huo huwaweka watu hatarini. Ubadilishanaji mkubwa na unaoendelea wa habari unatuhitaji kuwa macho na kukosoa masuala kadhaa muhimu: tofauti kati ya ukweli na habari za uwongo, ufichuzi usiofaa wa maisha ya kibinafsi, upotoshaji wa walio hatarini zaidi, mantiki ya usaliti, na uchochezi wa chuki na vurugu! Watu hawana budi kuwa waangalifu ili kuhakikisha kuwa taarifa za siri hazitumiwi kutisha, kudanganya, kukashifu, au kudharau huduma za wanasiasa, wanahabari, au watendaji wengine wa mashirika ya kiraia. Hali hii pia isitumike kwenye maisha na utume wa Kanisa. Hakika, katika nchi kadhaa, Kanisa ni mwathirika wa huduma za kijasusi zinazotendwa kwa makusudi maovu, zikikandamiza uhuru wake. Hatari hizi lazima zichunguzwe kila wakati na zinahitaji kuwekewa msimamo wa juu wa maadili kwa wale wanaojiandaa kufanya kazi kama yao na kwa wale ambao wamekuwa wakifanya kazi hii  kwa muda mrefu.

Kanisa pia ni muathirika wa vitendo vya kijasusi
Kanisa pia ni muathirika wa vitendo vya kijasusi   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anatambua dhamana na wajibu wao mbele ya umma, na kwamba, ametumia fursa hii kuwakumbuka na kuwaombea wafanyakazi wa Mfumo wa Habari wa Ulinzi na Usalama Nchini Italia wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika mazingira na maeneo tete sana; watu wanaosaidia kutatua changamoto zinazoendelea kulikumba Taifa la Italia. Amewashukuru wafanyakazi hawa wa “Intelijensia” wanaohakikisha pia ulinzi na usalama wa Vatican.Baba Mtakatifu Leo XIV, anawataka watekeleze dhamana na wajibu wao, huku wakilenga kukuza na kudumisha mafao ya wengi, wajifunze kuamua na kuhukumu kwa hekima na busara hali mbalimbali wanazokumbana nazo na hivyo kubaki wakiwa wamesimama katika misingi ya maadili na utu wema; heshima na haki msingi za binadamu. Amewapongeza kwa kuadhimisha kwa pamoja Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kama Jumuiya ya wafanyakazi. Neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu zitawawezesha kuzaa matunda bora katika ngazi ya mtu binafsi na katika shughuli zao kwa ujumla. Mwishoni amewatakia madhimisho mema ya Sherehe za Noeli kwa mwaka 2025.

Papa Ulinzi na Usalama

 

12 Desemba 2025, 15:51