Ujumbe wa Papa Leo XIV Kwa Mapadre na Watawa Kutoka Amerika ya Kusini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Nifuate ni neno ambalo Kristo Yesu alilitumia kutoa mwaliko wa ndani kabisa kwa wafuasi wake kama: waseminari, mapadre, au watawa. Huu ni mpango mkakati wa Yesu anayewaita pasipo kuwa na sifa yoyote ya awali kwa upande wao (rej. Mt 9:9; Yn 1:43), na badala yake kwa nia ya kwamba, wito anaowaitia utakuwa fursa ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kwa wenye dhambi na wanyonge. Rej Mt 9:12-13. Tayari kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yao. Wakati huo huo Injili inawataka wafuasi wa Kristo Yesu kufahamu dhamira inayohusika katika kuitikia wito huu. Anazungumzia juu ya madai ambayo wanaweza kutambua katika wito uliokatishwa tamaa kwa kijana tajiri: Mt 19:21): hitaji la ukuu kamili wa Mungu, aliye mwema pekee (mstari 17); hitaji la lazima la maarifa ya kinadharia na ya vitendo ya sheria ya Kimungu (Mst. 18-19) na hitaji la kujitenga na usalama wote wa kibinadamu, pamoja na utoaji wa matokeo ya yale yote waliyo nayo (mstari 21). Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa: Mapadre, Watawa na Majandokasisi kutoka Amerika ya Kusini wanaoishi na kusoma mjini Roma, kama sehemu ya Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, Ijumaa tarehe 12 Desemba 2025. Kardinali Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ndiye aliyeongoza mkutano huu na katika tafakari yake amekazia umuhimu wa Bikira Maria Mama wa Uinjilishaji mpya, chemchemi ya Kristo Yesu na Roho Mtakatifu. Bikira Maria ni Mama aliyejaa neema, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwilisha Injili katika uhalisia wa maisha yao, tayari kuinjilisha kwa kujikita katika sura ya Bikira Maria kwa kuwa karibu na Fumbo la Utakatifu Mtakatifu. Kwa hakika Bikira Maria ni Mama wa neema, mshiriki katika kazi ya ukombozi sanjari na uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mtakatifu Ambrose, katika ufafanuzi wake wa kifungu cha kustaajabisha cha kijana ambaye Yesu hakumruhusu kwenda kumzika baba yake (Lk 9:59), anachukulia kwamba katika dai hili la kuacha kila kitu, Kristo Yesu anapenda kufungua macho ya waja wake ili kuangalia maisha mapya, ili kuweza kuwa wamoja na Mwenyezi Mungu ili hatimaye kumwona vyema Mwanaye wa pekee. Kwa Mtakatifu Ambrose, muungano huu wa lazima na Kristo Yesu, mbali na kuwatenganisha na jamaa zao unawaongoza kujenga ushirika na wengine, walionunulia kwa bei ya thamani ya Damu yake Azizi. Rej. 1 Pet 1:18-19). Huu ni muungano unaowapeleka kwenye thamani ya kieskatolojia katika kuiga: “umoja wa amani ya milele na mapatano yasiyoweza kuvunjwa ya nafsi na katika agano lisilo na mwisho” na kutimiza “kile Mwana wa Mungu aliwahidia waja wake wakati alipoinua sala hii kwa Baba yake: ‘Ili wote wawe kitu kimoja, kama sisi tulivyo umoja’ (Yn 17:21.) Hatimaye, katika Injili ya Yohane, Yesu anarudia maneno “nifuate” kwa mtume Petro mara mbili. Anafanya hivyo katika muktadha tofauti sana, Ufufuo, mara tu baada ya ungamo la upendo mara tatu la Petro ili kulipia dhambi yake. Hata kukiri upendo wake, Mtume hakuelewa kikamilifu siri ya Fumbo la Msalaba, lakini Kristo Yesu akilini mwake alitambua juu ya dhabihu ambayo Mtakatifu Petro angempatia Mungu utukufu na kurudia kwake: "Nifuate" (Yn 21:19). Wakati, katika maisha yote, maono ya wafuasi wa Kristo yanapotiwa mawingu, kama yale ya Petro, katikati ya usiku au kupitia dhoruba (Mt 14:25, 31), itakuwa sauti ya Yesu ambayo, kwa subira ya upendo, huwategemeza.
Mara ya pili Yesu anamwambia Petro, “Nifuate,” ili kuwahakikishia wafuasi wake kwamba Kristo Yesu anatambua fika udhaifu wao na kwamba, mara nyingi, si Msalaba uliowekwa juu yao, bali ubinafsi wao wenyewe, ambao unakuwa kikwazo katika hamu yao ya kumfuata Kikristo Yesu. Mazungumzo na Mtume Petro yanaonesha jinsi wafuasi wa Kristo Yesu wanavyo wahukumu kwa urahisi ndugu zao na hata Mwenyezi Mungu, bila kukubali kwa upole mapenzi yake katika maisha yao. Hapa pia Bwana anarudia mara kwa mara kwao akisema: "Una nini kwako? Unifuate" (Yn 21:22). Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema kwa kuwa mapadre na watawa wanaishi katika jamii ya kelele za kutatanisha, leo kuliko wakati mwingine wowote wanahitaji watumishi na wanafunzi wanaotangaza na kushuhudia ukuu kamili wa Kristo Yesu na wanaosikia sauti yake waziwazi masikioni na mioyoni mwao. Ujuzi huu wa kinadharia na wa vitendo wa Sheria ya Mungu hupatikana zaidi ya yote kwa: Kusoma Maandiko Matakatifu, kutafakari katika ukimya wa sala ya kina; Kwa kutii kwa uchaji sauti ya wachungaji halali, na kujifunza kwa makini hazina nyingi za hekima ambazo Kanisa linawakirimia.
Katikati ya furaha na katikati ya matatizo, kauli mbiu yao lazima iwe: ikiwa Kristo alitembea njia hii, basi ni zamu yetu kuishi kile alichoishi. Hatupaswi kung'ang'ania kupiga makofi, kwa maana mwangwi wake ni wa kupita; wala si jambo la afya kukaa tu juu ya kumbukumbu ya siku ya msiba au nyakati za kukatishwa tamaa kwa uchungu. Badala yake, hebu tuone kwamba haya yote ni sehemu ya malezi yetu na kusema: ikiwa Mungu amenipenda, nitafanya hivyo pia (taz. Zab 40:8). Uhusiano wa kina unaowaunganisha na Kristo Yesu, iwe kama makuhani, watu waliowekwa wakfu, au waseminari, ni sawa na kile kinachosemwa kwa wenzi wa ndoa Wakristo katika siku yao ya arusi: “katika ugonjwa na afya, katika utajiri na umaskini” (Rite of Marriage, 66.) Mwishoni Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Bikira Maria wa Guadalupe, Mama wa Mungu wa kweli wanaoishi kwa ajili yake, awafundishe kuitikia kwa ujasiri, wakiweka mioyoni mwao maajabu ambayo Kristo Yesu ametenda ndani yao, ili wao bila kukawia watoke na kwenda kutangaza furaha ya kumpata, ya kuwa wamoja katika Mmoja, na mawe hai ya hekalu kwa utukufu wake. Bikira Maria aangalie muda wa uwepo wao huko Roma na awaombee, ili wote anaowasimamia hapa Roma wapate kuzaa matunda katika utume wa Bikira Maria.
