Tafuta

Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede" kwa Mwaka 2026 kinaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 155 tangu kuanzishwa kwake. Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede" kwa Mwaka 2026 kinaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 155 tangu kuanzishwa kwake.  (@Vatican Media)

Chama Cha Kitume Cha Mtakatifu Petro: Huduma Kwa Papa na Kanisa

Ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa kuzama zaidi katika karama, ushuhuda wa uaminifu wao katika kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na majukumu yake ya kuliongoza Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu amewapongeza kwani wao wako mbali sana na “Zuavi Pontefici” yaani Kikosi cha Wanajeshi kutoka Ufaransa, Ubelgiji, Netherland, na baadhi za nchi za Ulaya na Marekani, wanajeshi waliojisadaka kwa ajili ya Khalifa wa Mt. Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kufanya toba na kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa: mapendo, imani na matumaini zaidi. Ni katika muktadha huu, Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede", tarehe 27 Novemba 2021 kimefanya kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwake Jimbo kuu la Brussels nchini Ubelgiji. Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa Kardinali Dominique Mamberti, Mwenyekiti wa Mahakama Kuu ya Kitume ya Kanisa Katoliki kuwa mwakilishi wake maalum katika maadhimisho haya yaliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu Koekelberg, Jimbo kuu la Brussels, nchini Ubelgiji.

Papa Leo XIV amewapongeza wanachama wa "Pro Petri Sede kwa msaada wao
Papa Leo XIV amewapongeza wanachama wa "Pro Petri Sede kwa msaada wao   (@Vatican Media)

Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede" kwa Mwaka 2026 kinaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 155 tangu kuanzishwa kwake, kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican, Jumatano tarehe 18 Februari 2026. Ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa kuzama zaidi katika karama, ushuhuda wa uaminifu wao katika kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na majukumu yake ya kuliongoza Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu amewapongeza kwani wao wako mbali sana na “Zuavi Pontefici” yaani Kikosi cha Wanajeshi kutoka Ufaransa, Ubelgiji, Netherland, na baadhi za nchi za Ulaya na Marekani, wanajeshi waliojisadaka kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hiki ni kikosi kilichokuwa kinatumia silaha kutekeleza dhamana na majukumu yake, leo hii mambo yamebadilika.

Chama cha Pro Petri Sede: Huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro
Chama cha Pro Petri Sede: Huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro   (@Vatican Media)

Leo hii wanachama Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede" kinajikita katika maisha ya sala, kwa kuendelea kuragibisha dhamana na mchango wa Khalifa wa Mtakatifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila kusahau sadaka na majitoleo yao ya hali na mali. Baba Mtakatifu Leo XIV anawashukuru kwa kuamua kufadhili miradi ya maendeleo Jimbo Katoliki la Chiclayo, nchini Peru, mahali ambapo Baba Mtakatifu Leo XIV alipahudumia kama Askofu wake, kielelezo cha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu Jimboni humo kwa mawazo na matendo ya huruma. Anawashukuru kwa niaba ya Askofu Edinson Farfan, wa Jimbo la Chiclayo. Baba Mtakatifu Leo XIV amewasihi wajumbe hawa kuendelea kujikita katika maisha na utume wao wa kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na majukumu yake ya kuwaunganisha watu waaminifu wa Mungu; kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Karama yao inaonesha uhuru kamili wa kuweza kuutekeleza, bila ya vikwazo.

Amewapongeza wanachaka kwa kutoa huduma kwa Kanisa
Amewapongeza wanachaka kwa kutoa huduma kwa Kanisa   (@Vatican Media)

Kwa hakika Khalifa wa Mtakatifu Petro anaweza kutekeleza vyema dhamana yake ya kutangaza na kushuhudia ukweli; kukemea ukosefu wa haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa hakika, kwa njia ya uhuru huu, Khalifa wa Mtakatifu Petro anaweza kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za wanyonge na watu wasiokuwa na sauti; ni jukumu lake akuza na kuendeleza haki na amani, lakini zaidi kwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; kielelezo cha binadamu waliopatanishwa. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa sala na majitoleo yao, kwani haya ni mambo yanayomkirimia amani, faraja na matumaini, katika utekelezaji wa majukumu yake. Mwishoni, amewaweka wanachama wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa pamoja na chini ya Ulinzi wa Mtakatifu Petro Mtume na hatimaye akawapatia baraka zake za Kitume.

Pro Petri Sede
18 Februari 2026, 15:51