Tafuta

Kituo cha Hija cha Pugu, kinapata tena umaarufu kwa kuwa ni mahali ambapo Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anazikwa. Kituo cha Hija cha Pugu, kinapata tena umaarufu kwa kuwa ni mahali ambapo Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anazikwa. 

Kardinali Pengo: Kituo cha Hija Pugu, Utoto Mtakatifu na Rasilimali Fedha!

Kituo cha Hija cha Pugu, kinapata tena umaarufu kwa kuwa ni mahali ambapo Kardinali Pengo, anazikwa kama alama ya ndoa ya maisha ya kiroho. Ni mahali ambapo alipapenda kwa sala na tafakari. Aliwapenda watoto wa Utoto Mtakatifu, akawekeza sana katika malezi na makuzi yao; aliyeleta mabadiliko makubwa katika: usimamizi wa rasilimali fedha ya Kanisa, akawataka waamini kujikita katika: Ukweli, uwazi na ushiriki wa waamini walei katika kudhibiti rasilimali fedha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Polycarp Pengo Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam alikemea sana udini, akakazia majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Itakumbukwa kwamba, Uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha adili na matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbalimbali za dunia ni mambo yanayowaunganisha wote bila ubaguzi hata kidogo. Damu ya Wakristo, itaendelea kuwa ni mbegu ya Ukristo na mchakato wa umoja wa Wakristo. Wakristo wote wanateseka na kudhulumiwa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kumbe, uekumene wa damu una nguvu sana kama kielelezo cha ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko. Umoja wa Kanisa upewe kipaumbele cha kwanza kuliko mafao mengine yote! Kwa njia hii, Wakristo wataweza kujenga na kudumisha ushirika na Kristo Yesu pamoja na Wakristo wenzao kwa kuumega na kushiriki Fumbo la Ekaristi, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kama ilivyokuwa kwa mahujaji wa Emau walivyoamua kurejea tena Yerusalemu ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, “ili ulimwengu upate kusadiki.” Yn 17:21.

Kardinali aliwapenda watoto wa Utoto Mtakatifu, akawekeza katika malezi
Kardinali aliwapenda watoto wa Utoto Mtakatifu, akawekeza katika malezi

Ni katika muktadha huu, Watawa 14 Wamisionari wa Shirika la Wabenediktini walifika nchini Tanganyika, huko Pugu kunako mwaka 1888, huku wakitokea nchini Ujerumani kwa nia ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Tarehe 13 Januari 1889 wamisionari hawa waliuwawa kikatili na utawala wa Sultani na baadhi yao, wakafanikiwa kukimbilia sehemu nyingine. Wamisionari wakajenga shule ya Sekondari ya Mtakatifu Francis, ambayo leo hii inajulikana kama Pugu Sekondari, chimbuko la vuguvugu za ukombozi nchini Tanganyika. Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa kutambua umuhimu wa eneo la Pugu, kwa maisha na utume wa Kanisa, likaamua kujenga Kituo cha Hija cha Pugu, kama kumbukumbu ya Wamisionari walioyamimina maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kituo cha Hija cha Pugu, kinapata tena umaarufu kwa kuwa ni mahali ambapo Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anazikwa kama alama ya ndoa ya maisha ya kiroho na Askofu Jimbo. Hapa ni mahali ambapo Kardinali Pengo alipapenda kama mahali pake maalum pa sala na tafakari, tangu alipokuwa Gambera wa Seminari kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam. Alipokuwa akirejea kutoka safarini, alipitia kwanza Pugu, ili kusali, eneo la mashuhuda wa kwanza wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Kardinali Pengo alikuwa ni mtu wa sala na tafakari ya kina
Kardinali Pengo alikuwa ni mtu wa sala na tafakari ya kina   (©TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Alipenda sana kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya wokovu kwa sababu inatafakarisha maisha, utume, mateso, kifo, na ufufuko wa Kristo Yesu kupitia macho ya Bikira Maria. Kupitia matendo ya furaha, mwanga, uchungu, na utukufu, sala hii inakuwa ni muhtasari wa: upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Kardinali Pengo katika maisha na utume wake kama Askofu, aliwapenda watoto wa Utoto Mtakatifu, akawekeza sana katika malezi na makuzi yao; akaanzisha Rozari ya Watoto Parokia ya Kurasini ili kusali na kuombea miito mitakatifu. Alitoa upendeleo wa pekee kwa Parokia zilizokuwa pembezoni mwa Jimbo kuu la Dar Es Salaam na kati ya Parokia hizi ni Parokia ya Mafia ambako aliwekeza katika huduma mbalimbali za kiroho na kimwili, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kardinali Polycarp Pengo alikuwa ni mtu wa sala, mchamungu, mwadilifu, mpole, msikivu na kwamba, aliwapenda sana Mapadre wake. Kardinali Pengo ni kiongozi aliyeleta mabadiliko makubwa katika: usimamizi wa rasilimali fedha ya Kanisa, akawataka watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam kujikita katika: Ukweli, uwazi na ushiriki wa waamini walei katika kudhibiti rasilimali fedha ya Kanisa.

Kardinali Pengo aliwekeza katika malezi ya watoto
Kardinali Pengo aliwekeza katika malezi ya watoto

Ikumbukwe kwamba, Askofu anapopewa dhamana ya kuongoza, kutakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu, anavikwa pete ambayo ni alama ya "ndoa" kati yake na Kanisa mahalia (Jimbo). Kama vile mwanandoa anavyobaki na mwenzi wake hadi kifo, Askofu mahalia anachukuliwa kama "Baba na Mume" wa kiroho wa Kanisa mahalia. Kumzika ndani ya Kanisa Kuu ni ishara kuwa hatengani na kundi lake hata baada ya kifo; anabaki kuwa sehemu ya historia ya jimbo hilo daima. Neno "Cathedral" linatokana na mzizi neno la Kilatini “Cathedra” likimaanisha Kiti. Hiki ni Kiti cha mamlaka ya: Kuongoza, Kutakatifuza na Kufundishia aliyokabidhiwa Askofu mahalia. Kwa kuwa Kanisa kuu ndicho kitovu cha mamlaka yake na "nyumbani" kwake rasmi kiroho, ni mahali stahiki kisheria kwake yeye kupumzika akisubiri ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Itakumbukwa kwamba, tangu enzi za Kanisa la Mwanzo, masalia ya Mitume na viongozi wa Kanisa yaliheshimiwa na kuzikwa mahali pa ibada kwa mfano: Kaburi la Mtakatifu Petro, Mtume liko chini ya Altare kuu, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Askofu ni mfuasi wa Mitume, hivyo kuzikwa kwake Kanisani kunawakumbusha waamini kwamba imani yao imejengwa juu ya msingi wa Mitume walioyamimina maisha yao kama ushuhuda kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, wakawa tayari kuwalinda, kuwaongoza na kuwafundisha watu wa Mungu waliokabidhiwa kwao na Mama Kanisa.

Kardinali Pengo alipenda kusali kwenye Kituo cha Hija cha Pugu
Kardinali Pengo alipenda kusali kwenye Kituo cha Hija cha Pugu

Kadiri ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa Katoliki kuna katazo la jumla la kuzika miili ya watu ndani ya Makanisa ili kutunza utakatifu wa mahali hapo. Rej. Sheria n. 1239 §2, Sheria hii inatoa ruhusa kwa viongozi wafuatao kuzikwa ndani ya Makanisa. Hawa ni pamoja na Baba Mtakatifu, Khalifa wa Mtakatifu Petro. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alizikwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma, Makardinali, kama alivyozikwa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa tarehe 6 Oktoba 2021 kwenye Kanisa kuu la Jimbo Katoliki Bukoba, Tanzania baada ya Kanisa hilo kufanyiwa ukarabati mkubwa uliodumu kwa tarkibani miaka 17. Wengine wanaozikwa kwenye Makanisa ni Maaskofu, kama ilivyokuwa kwa Askofu Justin Tetemu Samba wa Jimbo Katoliki la Musoma, kunako mwaka 2006. Huu ni utaratibu unaotambua hadhi ya wachungaji wakuu wa Kanisa.

Kardinali Pengo aliwapenda na kuwathamini Mapadre wake.
Kardinali Pengo aliwapenda na kuwathamini Mapadre wake.

Ikumbukwe kwamba, Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kuhusu ushirika wa mema ndani ya Kanisa, kwa kuunganishwa na Kristo Yesu aliye kichwa cha Fumbo la Mwili wake yaani Kanisa na ushiriki huu unafanyika kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na hivyo mema yote haya yanakuwa ni hazina ya pamoja. Huu ni ushirika wa mambo matakatifu “Sancta” na ushirika kati ya watu watakatifu “Sancti.” Yote haya husaidia kukua katika ushirika wa Roho Mtakatifu “Koinonia” na kushirikisha ulimwengu. Rej. KKK 946-954. Kumbe, uwepo wa kaburi la Askofu ndani ya Kanisa huwasaidia waamini kuendeleza ushirika wa maisha ya kiroho na mchungaji wao; kaburi ni ukumbusho kwa waamini kwa ajili ya kumwombea na kuomba maombezi yake mbele ya Mungu, kielelezo cha ushirika kati ya watu wa Mungu.

Papa Leo XIV ametuma salam za rambirambi kwa watu wa Mungu Dar.
Papa Leo XIV ametuma salam za rambirambi kwa watu wa Mungu Dar.   (@VATICAN MEDIA)

Ni katika muktadha wa Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu, Baba Mtakatifu Leo XIV amemtumia salam za rambirambi Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania kufuatia kifo cha Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam kilichotokea tarehe 19 Februari 2026 majira ya Saa 4:00 Usiku, akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kutoa salama zake za rambirambi kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam. Anamshukuru Mungu kwa huduma ya Kiaskofu aliyoitekeleza katika majimbo kadhaa nchini Tanzania. Anamkumbuka hasa kwa sadaka na majitoleo yake katika malezi na majiundo ya awali na endelevu ya Makleri, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kati ya Mwaka 2007 hadi mwaka 2009 alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, akafanikiwa kuwaunganisha Maaskofu wa Kusini mwa Afrika na Kaskazini, kwa kukazia moyo wa SECAM kujitegemea kwa rasilimali watu na vitu. Na katika maisha na utume wake kama Kardinali, aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Mabaraza mbalimbali ya Kipapa kwa ajili ya huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuiweka roho ya Kardinali Polycarp Pengo, Mchungaji mnyenyekevu, katika huruma ya Kristo Yesu, Mchungaji Mwema. Kwa waombolezaji na wote walioguswa na msiba huu mzito, huku wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele, anapenda kuwapatia faraja na baraka zake za kitume!

Kardinali Pengo
26 Februari 2026, 15:07