Papa Leo XIV:Katika Kwaresima tutengeneze nafasi ya ukimya na kusikiliza
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya kwanza ya Kwaresima, tarehe 22 Februari 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa katika Dirisha la Jumba la Kitume mjini Vatican aliwageukia waamini na mahujaji waliokusanyika wengi katika Uwanja wa Mtakatifu Petro wakiwa chini ya Anga la Blue na jua, Papa alisema "Kaka na dada wapendwa, Dominika njema! Leo ni Dominika ya Kwanza ya Kwaresima, Injili inatuzungumzia kuhusu Yesu ambaye, akiongozwa na Roho, anakweenda jangwani na kujaribiwa na shetani (Rej Mt 4:1-11)." Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa " Baada ya kufunga kwa siku arobaini, anahisi uzito wa ubinadamu wake: kimwili, njaa, na kimaadili, majaribu ya shetani. Anapitia magumu yaleyale tunayopitia sisi sote katika safari yetu, na kwa kumpinga shetani, anatuonesha jinsi ya kushinda udanganyifu na mitego yake. Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea kusema kuwa Liturujia, pamoja na Neno hili la Uzima, linatualika kutazama Kwaresima kama safari angavu ambapo, kupitia sala, kufunga, na kutoa sadaka, tunaweza kufufua ushirikiano wetu na Bwana katika kufikia kazi bora ya kipekee ya maisha yetu."
Papa Leo XIV alisema hii ni kuhusu kumruhusu Yeye kuondoa madoa na kuponya majeraha ambayo dhambi inaweza kuwa imeyasababisha, na kujitolea kuifanya istawi katika uzuri wake wote, kwa utimilifu wa upendo, kisima pekee cha furaha ya kweli. Hakika, ni safari yenye kuhitaji juhudi nyingi, na hatari ni kwamba tunakatishwa tamaa au kushawishiwa na njia zisizohitaji juhudi nyingi za kutimiza, kama vile utajiri, umaarufu, na nguvu (rej Mt 4:3-8). Haya, ambayo pia yalikuwa majaribu ya Yesu, hata hivyo, ni mbadala wa furaha ambayo tuliumbwa nayo, na mwishowe, yanatuacha bila kuepukika na milele bila kuridhika, bila kutulia, na utupu.
Papa Leo XIV alisisitiza kuwa hii ndiyo sababu Mtakatifu Paulo VI alindika kwamba toba, mbali na kuwafanya wanadamu wetu kuwa wamaskini, huitajirisha, kuisafisha na kuiimarisha inaposafiri kuelekea upeo ambao "lengo lake ni upendo na kujikabidhi katika Bwana" (Katiba ya Kitume Paenitemini, Februari 17, 1966, I). Kiukweli Papa alisema kuwa, toba inatufanya tuelewe mapungufu yetu, na inatupa nguvu ya kuyashinda na kupata, kwa msaada wa Mungu, ushirika mkubwa zaidi naye na sisi kwa sisi. Baba Mtakatifu aidha alitoa ushauri muhimu kwamba “Katika wakati huu wa neema, tufanye mazoezi kwa ukarimu, pamoja na sala na matendo ya huruma: tutengeneze nafasi ya ukimya; tunyamazishe televisheni, radio, na simu za mkononi kwa muda.
Tutafakari Neno la Mungu, tukaribie Sakramenti; tusikilize sauti ya Roho Mtakatifu, anayesema nasi mioyoni mwetu, na tusikilizane, katika familia zetu, katika sehemu zetu za kazi, na katika jamii zetu, alisema. Papa aliendelea kuwa “Tutenge muda kwa wale walio peke yao, hasa wazee, maskini, na wagonjwa. Tuachane na yasiyo ya lazima na kushiriki kile tunachoweka akiba na wale wasio na mahitaji ya lazima. Kisha, kama Mtakatifu Agostino asemavyo, "sala yetu, inayotolewa kwa unyenyekevu na upendo, katika kufunga na kutoa sadaka, katika kiasi na msamaha, kutoa mema na kutorudisha mabaya, kugeuka na kuacha mabaya na kutenda mema" (Mahubiri 206, 3), itafika Mbinguni na kutupatia amani. Tukabidhi safari yetu ya Kwaresima kwa Bikira Maria, Mama ambaye huwasaidia watoto wake kila wakati hasa wakati wa majaribu," Papa alihitimisha.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here
