Tafuta

Papa Leo XIV anasema Kwaresima ni Kipindi cha toba na wongofu wa ndani; muda wa Sala na tafakari ya Neno la Mungu inayozamishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Papa Leo XIV anasema Kwaresima ni Kipindi cha toba na wongofu wa ndani; muda wa Sala na tafakari ya Neno la Mungu inayozamishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.  (© JUGO MEDIA)

Papa Leo XIV: Kwaresima: Toba, Wongofu, Neno, Sala Na Sakramenti Za Kanisa

Kwaresima ni muda muafaka wa kukutana na Yesu katika: Neno, Sala, Sakramenti ya Ekaristi na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu sanjari na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni muda uliokubaliwa wa kukutana na Kristo Yesu katika historia ya kila mwamini. Ni muda wa waamini kuzamisha maisha yao katika sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga na kudumisha mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kipindi cha Kwaresima, ambacho kwa mwaka huu 2026 kinanogeshwa na ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kauli mbiu: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani.” Kwaresima ni kipindi ambacho Kanisa kama Mama na Mwalimu, anawaalika watoto wake kutoa kipaumbele cha pekee kwa Fumbo la Mungu katikati ya maisha yao, ili imani ipate tena nguvu na mioyo ya waamini isipotee katikati ya mahangaiko na bughudha za maisha ya kila siku. Kila safari ya wongofu wa ndani huanza pale waamini wanaporuhusu Neno la Mungu liwafikie na kulikaribisha kwa moyo wa unyenyekevu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna uhusiano kati ya karama ya Neno la Mungu, Nafasi ya Ukarimu na mabadiliko ambayo Neno hili linaleta. Kwa sababu hiyo, safari ya Kwaresima inakuwa fursa muafaka ya kusikiliza sauti ya Mungu na hivyo kupyaisha tena maamuzi ya kumfuasa Kristo Yesu, kwa kutembea katika njia ile iendayo Yerusalemu ambako Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko vinapata utimilifu wake.

Kwaresima ni wakati wa sala na tafakari inayomwilishwa katika matendo
Kwaresima ni wakati wa sala na tafakari inayomwilishwa katika matendo   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 18 Februari 2026 amewaambia waamini kwamba, Kwaresima ni muda muafaka wa kukutana na Kristo Yesu katika: Neno, Sala, Sakramenti, hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu sanjari na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni muda uliokubaliwa wa kukutana na Kristo Yesu katika historia na safari ya maisha ya kila mwamini. Ni muda wa waamini kuzamisha maisha yao katika sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga na kudumisha mshikamano na udugu wa kibinadamu. Moyo wa sala, tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti katika Kipindi hiki cha Kwaresima ni mambo yanayoweza kuwasaidia waamini kuzama katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa wafu uletao maisha na uzima wa milele; ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu.

Kwaresima 2026
18 Februari 2026, 15:30