Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV anatembelea Barani Afrika kama shuhuda na mjumbe wa matumaini, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu Leo XIV anatembelea Barani Afrika kama shuhuda na mjumbe wa matumaini, amani na upatanisho.   (@Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Barani Afrika 2026: Lengo Kuu

Papa Leo XIV akiwa Barani Afrika atazungumzia masuala mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kuhusu:: Haki, Amani, Majadiliano, Utunzaji wa Mazingira; wakimbizi na wahamiaji pamoja na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; Mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; magonjwa, ujinga, njaa na vita na kwamba, ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kuwa Wakatoliki Barani Afrika wataendelea kujipambanua kuwa ni mashuhuda wa haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija za Kitume za Khalifa wa Mtakatifu Petro nje ya Vatican zinapania pamoja na mambo mengine: kuwatia shime, ari na mwamko wa kimisionari, watu watakatifu wa Mungu ili wawe tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Kristo Yesu ili kwa njia ya: Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma aweze kuwagusa na kuwatakasa kutoka katika undani wa maisha yao, kama ilivyokuwa kwa yule mtu kipofu tangu kuzaliwa kwake. Rej Yn 9:1-25. Hii ni changamoto ya kusikiliza kwa makini na hatimaye kumwilisha tunu msingi za Kiinjili, Kiutu, Kitamaduni, Kijamii na Kisiasa katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji na kama sehemu mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili mambo ambayo ni sawa na chanda na pete. Rej. Yn 9:1-25. Ni hija zinazopania kuwaimarisha watu wa Mungu katika imani, matumaini na mapendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumatatu tarehe 13 hadi 23 Aprili 2026 anafanya hija ya kitume ya Siku 10 kwa kutembelea miji 11nchini Algeria, Cameroon, Angola pamoja na Guinea ya Ikweta “Equatorial Guinea.” Baba Mtakatifu Leo XIV anatembelea Barani Afrika kama shuhuda na mjumbe wa matumaini, amani na upatanisho. Hapa mkazo ni kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inajikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, ili kweli Bara la Afrika liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Kanisa ni chombo na shuhuda wa upatanisho, dhamana ambayo limepewa na Kristo Yesu!

Papa Leo XIV Barani Afrika: Shuhuda wa haki, amani na maridhiano
Papa Leo XIV Barani Afrika: Shuhuda wa haki, amani na maridhiano   (@Vatican Media)

Massimiliano Menichetti Mratibu mkuu wa Radio Vatican katika mahojiano maalum na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuhusu Hija ya Tatu ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV Barani Afrika na kwamba atazungumzia masuala mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Barani Afrika, yakiwemo masuala yanayohusu: Haki, Amani, Majadiliano, Utunzaji wa Mazingira nyumba ya wote; wakimbizi na wahamiaji pamoja na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; Mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; magonjwa, ujinga, njaa na vita na kwamba, ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kuwa Wakatoliki Barani Afrika wataendelea kujipambanua kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kardinali Parolin anakaza kusema: Papa Leo XIV anatembelea Afrika kuonesha mshikamano wake wa upendo na wale wanaoishi pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; Majadiliano ya kidini na waamini wa Dini ya Kiislam; majadiliano yanayosimikwa katika kuheshimiana na kuthaminiana; changamoto na matumaini ya watu wa Mungu nchini Angola katika maisha na utume wa Kanisa mahalia; Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji nchini Guinea ya Ikweta kuanzia mwaka 1855-2025, Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini. Hii ni fursa kwa Kanisa Barani Afrika kuwa: ni chombo cha haki, amani na upatanisho wa kweli; kwa kujikita kikamilifu katika kujenga na kudumisha maridhiano, haki jamii; Kwa kusima kidete kupambana; Na ujinga, umaskini na magonjwa, ili kunogesha haki msingi za binadamu pamoja na mshikamano Barani Afrika.

Lengo ni kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu
Lengo ni kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu

Wakatoliki watambue kwamba wao ni wadau wakuu wa mageuzi katika maisha yao na kwamba, ustawi na maendeleo ya Kanisa Barani Afrika kwa siku zijazo nikuendelea kujikita katika kuwasindikiza watu wa Mungu Barani Afrika katika sadaka na matumaini. Lengo kuu la hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV ni kutaka kuleta uwepo wa Kanisa mahali ambapo mateso ya mwanadamu ni makubwa zaidi. Hizi ni Nchi nne, zinatofautiana katika historia, muktadha wa kijamii, na changamoto za kisiasa, lakini zimeunganishwa na ukweli wa kimsingi unaoangaziwa na mwanga na kivuli: Jumuiya za Kikatoliki zilizochangamka na zilizokita mizizi yake kwa Kristo Yesu, lakini pia zinazosiginwa na umaskini, udhaifu, ukosefu wa usawa, na mivutano na kinzani zisizo kuwa na suluhu, Papa Leo XIV anataka kuonesha ukaribu na wale wanaoishi pembezoni mwa vuipaumbele vya maisha. Dhamira kuu ya Hija ya Kitume inatokana na uamuzi wa Baba Mtakatifu wa kuleta uwepo wa Kanisa mahali ambapo mateso ya mwanadamu ni makubwa zaidi. Hizi ni nchi nne, tofauti katika historia yao, muktadha wa kijamii, na changamoto za kisiasa, lakini zimeunganishwa na ukweli wa kimsingi unaoangaziwa na mwanga na kivuli: jumuiya za Kikatoliki zilizochangamka na zilizokita mizizi, lakini pia umaskini, udhaifu, ukosefu wa usawa, na mivutano isiyotatuliwa. Papa Leo XIV anasafiri Barani Afrika kuwa karibu na wale wanaoishi pembezoni mwa vipaumbele vya maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV amewahi kuzitembelea baadhi ya nchi hizi alipokuwa Mkuu wa Shirika la Waagostiani “The Order of St. Augustine, OSA” na kwamba, anapenda kukazia majadiliano ya kidini; ujenzi wa madaraja ya watu kukutana, kwa kutembelea kwenye Msikiti mkuu wa Algeria; huu ni mwendelezo wa majadiliano aliyoyaanzisha wakati wa hija yake ya Kitume nchini Uturuki na Lebanon; majadiliano ya dhati anayotaka kuyaendeleza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa dhati na uvumilivu.

Kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote
Kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote   (AFP or licensors)

Akiwa nchini Cameroon, Baba Mtakatifu Leo XIV kama kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki anapenda kufahamu kwa ukaribu zaidi: matatizo, changamoto na fursa kwa watu wa Mungu nchini humo, anatembelea nchini humo kama mjumbe na shuhuda wa matumaini, hasa kwa vijana wa kizazi kipya; ili kuragibisha na kukoleza mchakato wa haki, amani na upatanisho, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Cameroon kuendelea kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi na hali ya kuheshimiana. Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa nchini Angola, anatembelea mji wa Luanda na Saurimo, kielelezo cha utajiri wa Angola; fursa, matatizo ya unyonyaji na ukandamizaji wa wafanyakazi kwenye machimbo ya madini, madhara yake katika mustakabali wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote nchini Angola. Kardinali Pietro Parolin anakaza kusema yeye ni shuhuda wa uhai wa Kanisa nchini Angola, mambo alioyaona wakati wa kumweka wakfu Monsinyo Germano Penemote kuwa Askofu mkuu na Balozi wa kwanza Vatican kutoka nchini Angola. Jubilei ya Miaka 170 ya Uinjilishaji nchini Guinea ya Ikweta kuanzia mwaka 1855-2025, inanogeshwa na kauli mbiu “Kristo Yesu Mwanga wa Guinea ya Ikweta, kuelekea kwenye matumaini” ni mwaliko kwa watu watakatifu wa Mungu nchini humo kuyaangalia yaliyopita kwa imani na kuanza kujielekeza katika hija ya imani na matumaini, ni wakati kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kuwasha tena moto wa imani kwa kuwaimarisha vijana katika tunu msingi za Kiinjili, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa, huku wakiendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini humo.

Papa Leo XIV akizungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mku wa Vatican
Papa Leo XIV akizungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mku wa Vatican   (@Vatican Media)

Kardinali Pietro Parolin anasema, Diplomasia ya Papa Leo XIV inajikita katika: Ukweli, Haki na Amani kama uzoefu na mang’amuzi ya kuweza kukutana na watu na tamaduni mbalimbali. Katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anapania pamoja na mambo mengine: Kuimarisha majadiliano katika ukweli na uwazi; kuendelea kufahamu amana na utajiri wa nchi mbalimbali na hivyo kupata fursa ya kuweza kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo sanjari na kuendelea kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu. Anapenda kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu; uhuru wa kidini; Utu, heshima na kwamba, anapania kuragibisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hija hii ya kitume, inamkutanisha Baba Mtakatifu Leo XIV na viongozi mbalimbali na kwamba, hii ni fursa kwa Mama Kanisa kuendelea kuhimiza: Maridhiano, Haki Jamii, Mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na njaa mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za kijamii, ili kuweza kulisimika Bara la Afrika katika: haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Bara la Afrika lina amana na utajiri mkubwa wa maliasili, rasilimali watu na tamaduni, lakini kwa bahati mbaya linaendelea kuzama katika ukosefu wa maendeleo endelevu ya binadamu, rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Kanisa Barani Afrika limeendelea kuwa ni mdau makini wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa njia ya huduma katika sekta ya elimu, afya na maendeleo kama sehemu muhimu ya kusikiliza na kujibu kilio cha Maskini na Dunia Mama. Kanisa linakazia umuhimu wa kumwilisha tunu msingi za Kiinjili, kiutu, kitamaduni na kifamilia; Utu, haki na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kwamba, Wakristo Barani Afrika wanapaswa kuwa ni wadau wakuu wa mageuzi katika maisha yao binafsi, jumuiya na kwenye taasisi mbalimbali.

Diplomasia ya Vatican inakita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi
Diplomasia ya Vatican inakita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi   (@VATICAN MEDIA)

Ni matumaini ya Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwamba, Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumatatu tarehe 13 hadi 23 Aprili 2026 kwa kutembelea nchini Algeria, Cameroon, Angola pamoja na Guinea ya Ikweta, itasaidia kujenga na kudumisha: Haki, amani, upatanisho, majadiliano na ukuaji wa Kanisa mahalia katika ukarimu; maridhiano na utulivu kwenye nchi ambazo bado zina madonda makubwa ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Kanisa Barani Afrika bado ni changa, lakini linabeba ndani mwake amana na utajiri imani, uhai na kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV ana imani kubwa katika ustawi na maendeleo ya Kanisa Barani Afrika, na kwamba, Kanisa la Kiulimwengu litaendelea kulisindikiza kwa sadaka na majitoleo makubwa pamoja na matumaini.

Papa Leo XIV Barani Afrika
11 Aprili 2026, 17:55