Tafuta

Taasisi ya Kitaifa ya Usalama wa Jamii (INPS) ndiyo taasisi kuu ya hifadhi ya jamii katika mfumo wa pensheni ya umma nchini Italia. Taasisi ya Kitaifa ya Usalama wa Jamii (INPS) ndiyo taasisi kuu ya hifadhi ya jamii katika mfumo wa pensheni ya umma nchini Italia.   (@Vatican Media)

Hotuba ya Papa Leo XIV Kwa Taasisi ya Usalama wa Kijamii Italia, INPS

Papa Leo XIV: Aliwataka kutenda ipasavyo katika kukuza uwajibikaji wa kijamii unaochanganya maendeleo ya kiuchumi na uwiano wa jamii kwa kuongoza maamuzi kuelekea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili kupambana na ongezeko kubwa la umaskini nchini Italia. Papa Leo XIV anasema, Ulimwengu ni tajiri sana, lakini idadi ya maskini inaongezeka kwani kuna mamlioni ya watu duniani kote wamezama katika dimbwi la umaskini wa mahitaji muhimu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taasisi ya Kitaifa ya Usalama wa Jamii (INPS) ndiyo taasisi kuu ya hifadhi ya jamii katika mfumo wa pensheni ya umma nchini Italia. Wafanyakazi wote wa umma na wale kutoka katika sekta ya binafsi pamoja na wafanyakazi wa kujitegemea ambao hawana mfuko wao wa pensheni wa kujitegemea, lazima wajiandikishe katika INPS. INPS iko chini ya usimamizi wa Wizara ya Kazi na Sera za Kijamii. Mfumo wa kwanza wa dhamana ya pensheni, uliokusudiwa tu kwa wafanyakazi wa umma na wanajeshi, ulianza 1895, wakati wa serikali ya nne ya Crispi. Ilipanuliwa kwa aina zingine za wafanyikazi na serikali ya Pelloux I na Orlando, lakini uanachama wa lazima ulianzishwa na serikali ya Mussolini kunako mwaka 1923. Viongozi na wanachama wa Taasisi ya Kitaifa ya Usalama wa Jamii nchini Italia (INPS), Ijumaa tarehe 10 Aprili 2026 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican. Katika hotuba yake Baba Mtakatifu Leo XIV: Aliwataka kutenda ipasavyo katika kukuza uwajibikaji wa kijamii unaochanganya maendeleo ya kiuchumi na uwiano wa jamii kwa kuongoza maamuzi kuelekea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili kupambana na ongezeko kubwa la umaskini nchini Italia. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Ulimwengu ni tajiri sana, lakini idadi ya maskini inaongezeka kwani kuna mamlioni ya watu duniani kote wamezama katika lindi la umaskini uliokithiri kwa kukosa: Chakula, malazi, matibabu, elimu, umeme, maji safi na salama pamoja na huduma muhimu za afya. Hata hivyo utajiri usio na uwiano unabaki mikononi mwa wachache na kwamba hali hii si haki, kwani kuna ukosefu wa usawa. Mzizi wa ukosefu wa usawa sio ukosefu wa rasilimali, lakini hitaji la kushughulikia shida zinazoweza kutatuliwa, zinazohusiana na usambazaji wao wa usawa zaidi, ili kufikiwa kwa akili ya maadili na uaminifu. Katika muktadha huu, kuitikia mahitaji madhubuti ya watu daima kumekuwa lengo kuu la Kanisa Katoliki, katika ulimwengu wa kazi na katika kutoa msaada kwa wahitaji.

Viongozi na wanachama wa INPS wakiwa na Papa Leo XIV
Viongozi na wanachama wa INPS wakiwa na Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Papa Leo XIII, alikazia uwazi kuwa ni jambo umuhimu sana la usalama wa kijamii na huduma, ili "kuhakikisha kwamba mfanyakazi hakosi kazi kamwe, na kwamba fedha zinapatikana ili kusaidia kila mtu binafsi, si tu katika migogoro ya ghafla na isiyotarajiwa ya viwanda, lakini pia katika hali ya udhaifu, uzee, na ajali" Rej. Rerum Novarum, 4. Na kuhusu uungwaji mkono kwa walio hatarini zaidi, alisema: “Iwapo familia yoyote itatokea kujikuta katika hali mbaya kiasi kwamba haina uwezo kabisa wa kuzikimbia yenyewe, ni sawa kwamba mamlaka za umma kuingilia kati nyakati hizo, kwa kuwa kila familia ni sehemu ya chombo cha kijamii.” Rej. Rerum Novarum, 11). Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mama Kanisa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa ameinua haki ya ustawi kuwa kiwango cha haki ya binadamu, kama haki "ya usalama katika tukio la ugonjwa, ulemavu, ukosefu wa fursa za ajira, kujikimu kwa sababu ya hali zilizo nje ya uwezo wa mtu.” Pacem in Terris, 6. Mtindo unaopendekezwa ni ule wa mfumo wa usalama unaotegemea mshikamano, unaozingatia kanuni ya auni, uwajibikaji wa kijamii, na udugu wa kibinadamu, daima kwa lengo la kuelekeza uingiliaji wa ustawi ili kuhakikisha kwamba kila mtu anapata "maisha yenye heshima kupitia kazi” Rej. Laudato si', 128). Muhtasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa unakazia kuhusu kanuni ya mshikamano unaowawezesha watu wawe na ufahamu mkubwa wa deni lao kwa jamii ambamo wanaishi.

Papa Leo XIV akiwasikiliza viongozi wa INPS
Papa Leo XIV akiwasikiliza viongozi wa INPS   (@Vatican Media)

Katika hali hii nchini Italia, jukumu la kuongoza bila shaka lazima kutambuliwa katika Taasisi ya INPS, ambayo inaongoza kazi yake katika pande mbalimbali, kwa kutekeleza sera za pensheni inayozalisha na ufanisi wa maendeleo ya kijamii, kuanzia na ulinzi wa mazingira magumu zaidi na uwekezaji katika vijana. Kumbe INPS lazima kulinda mshikamano na usawa wake, katika suala la pensheni na kusaidia wafanyakazi katika taaluma zao zote kwani mazingira katika Ulimwengu mamboleo yamebadilika kwa kiasi kikibwa kutokana na: Ufadhili wa biashara, usambazaji wa uzalishaji kwa kiwango cha Kimataifa, gharama kubwa za wafanyikazi, na, juu ya yote, maendeleo ya haraka ya kiteknolojia, yenye athari kubwa kutokana na matumizi ya teknolojia ya akili unde, yanayohitaji kuchambuliwa na kuthaminiwa na hasa kutokana na watu kutokuwa na uhakika, hali inayoleta mahitaji na majukumu mapya kwa serikali na mtu binafsi kuridhika kwake lazima kuhusishe taasisi za hifadhi ya jamii, na hasa INPS. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha hotuba yake kwa kuwakumbusha kwamba, mwanadamu ndiye faradhi, kumbe anapaswa kupendwa na kutumikiwa kwa dhamiri nyofu, uwajibikaji na upatikanaji na kwamba wafanye kazi kwa ajili ya watu wote. Wasimame kidete kuwasaidia watu dhaifu, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na uhuru unaowawezesha kuishi maisha ya kibinadamu. Amewatakia viongozi na wanachama wote wa INPS heri na baraka katika kazi yao na kwamba, anaendelea kuwabeba katika sala zake na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.

Usalama wa Kijamii
13 Aprili 2026, 16:18