Tafuta

Siku ya wakimbizi na wahamiaji inaadhimishwa tarehe 27 Septemba 2026 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Hata mmoja tu wa watoto hawa” kwa kufanya rejea kwenye Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo: 18:5. Siku ya wakimbizi na wahamiaji inaadhimishwa tarehe 27 Septemba 2026 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Hata mmoja tu wa watoto hawa” kwa kufanya rejea kwenye Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo: 18:5.  (AFP or licensors)

Kauli Mbiu Maadhimisho Siku ya 112 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani Septemba 2026

Siku ya wakimbizi na wahamiaji inaadhimishwa tarehe 27 Septemba 2026 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Hata mmoja tu wa watoto hawa” kwa kufanya rejea kwenye Injili: “Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi.” Mt 18:5. Papa Leo XIV anakusudia kuelezea wasiwasi wa Kanisa kwa watoto wadogo wanaohusika moja kwa moja na uhamiaji, akikumbuka wajibu wa kumkaribisha kila mmoja wao kama Injili inavyofundisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chimbuko la Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ni kutokana na: mahangaiko pamoja na mateso ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kutokana na madhara makubwa ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Ndiyo maana Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. LG 1. Papa Pio X, kunako mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 na kuanza kusherehekewa na Kanisa la Kiulimwengu.

Siku ya 112 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani Sept. 2026: Watoto
Siku ya 112 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani Sept. 2026: Watoto   (ANSA)

Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akawa ni kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki kuanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, kama sehemu ya sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika shughuli za kichungaji ili kusikiliza na kujibu kwa dhati kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha.

Kauli Mbiu: "Hata mmoja tu wa watoto hawa." Mt 18:5
Kauli Mbiu: "Hata mmoja tu wa watoto hawa." Mt 18:5

Ni matumaini ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwamba, sera na mikakati hii itaendelea kumwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso mambo ambayo kimsingi yanasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Tangu mwaka 1952, Siku hii ilikuwa ikiadhimishwa Dominika baada ya Sherehe ya Tokeo la Bwana. Lakini kunako mwaka 2018, Baba Mtakatifu Francisko baada ya kusikiliza maoni na kuridhia maombi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia akaamua kwamba, Siku hii iadhimishwe Dominika ya mwisho ya Mwezi Septemba.

Haki msingi za watoto wakimbizi na wahamiaji
Haki msingi za watoto wakimbizi na wahamiaji

Na kwa mwaka huu, inaadhimishwa tarehe 27 Septemba 2026 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Hata mmoja tu wa watoto hawa” kwa kufanya rejea kwenye Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo: “Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi.” Mt 18:5. Kwa uchaguzi huu, Baba Mtakatifu Leo XIV kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya 112 ya wakimbizi na wahamiaji duniani, anakusudia kuelezea wasiwasi wa Kanisa kwa watoto wadogo wanaohusika moja kwa moja na uhamiaji, akikumbuka wajibu wa kumkaribisha kila mmoja wao kama Injili inavyofundisha. Hii si mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu kuzungumza kwa mamlaka juu ya suala hili, lakini hali ya sasa ya ukimbizi na uhamiaji inatoa changamoto mpya ambazo zinatishia kwa kiasi kikubwa: Utu, heshima haki msingi za watoto wadogo zenye kuhitaji majibu ya haraka yenye tija na ufanisi. Kwa hivyo, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hili sio suala la kujadili namba au asilimia, kwa sababu “hata mmoja tu” anathamani kubwa zaidi.

Siku ya Wakimbizi 2026
09 Aprili 2026, 15:05