Tafuta

POPE-AFRICA/CONGO

Papa Afrika,Parolin:Wakatoliki wako mstari wa mbele kwa mabadiliko

Papa Leo XIV anasafiri kwenda Afrika ili kuwa karibu na wale wanaoishi pembezoni mwa maisha,akipeleka tumaini la Kristo.Hili linarudiwa na Katibu Mkuu wa Vatican Kardinali Parolin kabla ya Ziara ya Tatu ya Kitume ya Papa,ambayo inaanza Jumatatu,Aprili 13.

Massimiliano Menichetti

Algeria, Cameroon, Angola, na Guinea ya Ikweta zinasubiri kuwasili kwa Papa Leo XIV, ambaye atakuwa barani Afrika kuanzia Jumatatu, Aprili 13, hadi Alhamisi, Aprili 23. Wakati wa hatua ya kwanza ya ziara yake, Baba Mtakatifu pia atatembelea Annaba, jiji la kale la Hippo, "sio ishara ya ukumbusho tu," alisisitiza Katibu Mkuu wa  Vatican, Kardinali Pietro Parolin, "bali ni kitendo cha utambulisho wa kina na, zaidi ya yote, mshikamano wa kiroho." Maandalizi ya mwisho yanaendelea katika nchi hizo nne, huku matarajio yakiwa makubwa kwa maneno ya Papa. Kama Msemamaji mkuu wa Ofisi ya Habari ya Vatican,  Matteo Bruni alivyosisitiza wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari wakati wa kuwasilisha Ziara yake ya Tatu ya Kitume, haya yatazingatia, miongoni mwa mambo mengine, mada za amani, mazungumzo, utunzaji wa uumbaji, uhamiaji, na familia. Kuhusu mantiki ya uchu ambayo mara nyingi inasumbua bara la Afrika, ikichochea umaskini, ufisadi, na vurugu, Kardinali Parolin anatumaini kwamba Wakatoliki watakuwa wajenzi wa haki, amani, na mshikamano.

Kardinali Parolin, Baba Mtakatifu atakuwa barani Afrika kuanzia Aprili 13 hadi 23, akiimarisha jumuiya za Wakatoliki katika imani yao. Atatembelea nchi nne zenye ajenda yenye shughuli nyingi, ikiwa ni pamoja na mikutano ya kitaasisi, mikutano na hali halisi ya wenyeji, na sherehe. Ni  jambo gani la pamoja linalounganisha ratiba mbalimbali?

Jambo kuu linaloongoza Ziara  hii ya Kitume lipo katika chaguo la Baba Mtakatifu la kupeleka uwepo wa Kanisa ambapo mateso ya wanadamu ni makali zaidi. Nchi nne zenye historia tofauti, miktadha ya kijamii, na changamoto za kisiasa, lakini zimeunganishwa na ukweli wa msingi unaofanana unaooneshwa na mwanga na kivuli: Jumuiya hai zenye mizizi ya kikatoliki lakini pia umaskini, udhaifu, ukosefu wa usawa, na mivutano isiyotatuliwa. Papa Leo XIV anasafiri kwenda Afrika ili kuwa karibu na wale wanaoishi pembezoni mwa maisha. Nchi ya kwanza ni Algeria.

Papa Leo XIV pia atatembelea Msikiti Mkuu huko Algiers na ataadhimisha Misa Takatifu huko Annaba, jiji la kale la Hippo. Je, kurudi huku kwa maeneo ya Mtakatifu wa Hippo kuna umuhimu gani kwa Papa ambaye ni mwana wa Mtakatifu Agostino na hii inaweza kuathiri vipi mazungumzo ya Waislamu na Wakristo katika nchi yenye Waislamu wengi?

Kama mwana wa kiroho wa Mtakatifu Agostino, na Papa wa kwanza kuwa wa Shirika la Kiagostiniani, kusafiri kwenda Annaba si ishara ya ukumbusho tu, bali ni kitendo cha utambulisho mkubwa na, zaidi ya yote, mshikamano wa kiroho. Papa Leo anajua ardhi hii na aliitembelea mara kadhaa kama Mkuu wa  Awali wa Shirika. Katika muktadha huu, Mtakatifu Agostino anawakilisha kipengele cha mazungumzo: anaunda sehemu ya asili ya kukutana kati ya tamaduni  ya Kikristo na ulimwengu wa Kiislamu. Ziara ya Msikiti Mkuu wa Algiers inaendana kikamilifu na mtazamo huo, kama mwendelezo wa asili wa njia ya mazungumzo kati ya dini mbalimbali ambayo tayari yameanza nchini Uturuki na Lebanon; mazungumzo ambayo Baba Mtakatifu anakusudia kuyafuata kwa uvumilivu na azma.

Nchini Cameroon, Baba Mtakatifu atatembelea miji mitatu: Yaoundé, Bamenda, na Douala, ikiwa na matukio muhimu kama vile mkutano wa amani huko Bamenda na ziara ya kituo cha watoto yatima. Kwa kuzingatia mvutano katika baadhi ya maeneo ya nchi, ziara hii inaweza kuchukua jukumu gani katika kukuza upatanisho na amani kati ya jumuiya?

Kwa miaka kadhaa, mgogoro umekuwa ukiendelea katika maeneo yanayozungumza Kiingereza nchini Cameroon, na kusababisha waathiriwa wengi. Watu wa Bamenda wanapitia hali hiyo. Kwa hivyo, katika muktadha wa hali ya usalama na kibinadamu inayozidi kuzorota, ziara ya Mrithi wa Petro inaonesha umakini na utunzaji ambao Mchungaji wa Kanisa la ulimwengu wote anao kwa kundi lake, akijitahidi kuelewa matatizo yao moja kwa moja na kutembea nao. Ziara yake kwa Bamenda ni ya mchungaji anayejitambulisha na kundi lake. Kwa ujumla zaidi, Baba Mtakatifu hutembelea nchi kama mbebaji wa matumaini, hasa kwa vijana, wa upatanisho na amani. Ujumbe wake ni mwaliko wa mazungumzo na kuheshimiana.

Kituo cha tatu ni Angola, ambapo Papa atatembelea, pamoja na mji mkuu, Luanda, maeneo ya mfano kama vile Muxima na Saurimo, akikutana na jumuiya za Kanisa na jumuiya mahalia. Ni ujumbe gani ambao Baba Mtakatifu anakusudia kupeleka kwa nchi yenye rasilimali nyingi lakini pia yenye ukosefu wa usawa mkubwa wa kijamii?

Sehemu tatu ambazo Baba Mtakatifu atatembelea nchini Angola, kwa maana fulani, zinaashiria changamoto na matumaini ambayo nchi inapitia kwa sasa. Luanda na Saurimo zinawakilisha utajiri wa nchi. Mji mkuu sasa ni kitovu cha ustawi, kinachovutia uwekezaji wa kigeni na uhamiaji kutoka maeneo ya vijijini. Saurimo ni kitovu kinachojulikana kwa shughuli zake za uchimbaji madini, hasa almasi. Ingawa unyonyaji wa maliasili umeleta ustawi, baadhi ya matokeo yake mabaya hayawezi kupuuzwa, kama vile unyonyaji wa wafanyakazi, kuzidi kwa mgawanyiko wa kijamii na kiuchumi, na athari za mazingira. Na kisha, ziara katika madhabahu ya  Maria huko  Muxima inawakilisha uhai wa imani ambao umewasaidia watu wa Angola kushinda matukio mbalimbali ya kusikitisha ya historia yao. Ningependa kuongeza kwamba mimi pia nilipitia uhai wa Kanisa  mahalia nilipokwenda kwa ajili ya kumweka wakfu kwa Kiaskofu Germano Penemote, Balozi wa kwanza wa Vatican mwenye asili ya Angola.

Nchi ya mwisho itakuwa Guinea ya Ikweta, ikihitimisha safari kupitia Malabo, Mongomo, na Bata, kwa mikutano na vijana, familia, ulimwengu wa utamaduni, na hata wafungwa. Uangalifu huu maalum kwa vijana na familia una umuhimu gani katika nchi ambapo Kanisa lina uwepo mkubwa katika jamii?

Guinea ya Ikweta ni miongoni mwa nchi zenye Wakatoliki wengi barani Afrika, huku 80% ya wakazi wakifuata imani ya Kikatoliki. Kwa kufuata nyayo za Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, aliyetembelea nchi hiyo mwaka  1982, ziara hii inaadhimisha miaka 170 ya kuanza kwa Uinjilishaji wa nchi hiyo (1855-2025), ikiwa na kauli mbiu: "Kristo, nuru ya Guinea ya Ikweta, kuelekea mustakabali wa matumaini." Kwa Ziara  hii ya Kitume, watu wa Guinea ya Ikweta wanakumbuka yaliyopita kwa kujiamini katika safari ya imani na matumaini kuelekea mustakabali. Ziara ya Papa na mikutano yake, hasa na vijana na familia, huamsha upya mwali wa imani yao, ikiwatia moyo kukuza na kudumu katika maadili ya Kikristo. Ni mwaliko wa upendo na wa kibaba wa upatanisho, haki, na uvumilivu katika imani, pamoja na matumaini ya athari chanya kwa jamii.

Mwadhama  ziara hii ya kwenda Afrika ina umuhimu gani pia katika ngazi ya kidiplomasia?

Kila Ziara  ya Kitume ina umuhimu wa kidiplomasia kwa sababu inawakilisha fursa ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili kati ya Vatican na nchi zilizotembelewa na Papa. Hii inampa fursa ya kukutana na mamlaka na kujadili masuala ya maslahi ya pamoja, kitaifa, kikanda, na kimataifa. Katika bara la Afrika, hii inachukua umuhimu maalum kwa sababu bara hilo lina uwezo mkubwa lakini pia changamoto kubwa. Kama inavyojulikana, diplomasia ya Papa ina malengo yaliyo wazi: kulinda uhuru wa msingi, hasa uhuru wa kidini, kuhamasisha amani, kuhamasisha mazungumzo, ikiwa ni pamoja na mazungumzo kati ya dini, kutetea heshima ya kila mwanadamu, na kuhimiza maendeleo fungamani  ya watu. Kwa mtazamo huu, kila hatua ya Ziara  ya Kitume ijayo, ambayo inahusisha Maghreb yaani Algeria na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, inakuwa fursa ya kuthibitisha tena kujitolea kwa Kanisa, pamoja na taasisi za kiraia na kidini, kwa ajili ya kuishi pamoja kwa amani kati ya imani na makabila tofauti, haki ya kijamii, mapambano dhidi ya umaskini, na ulinzi wa utu wa binadamu. Hatimaye, katika kuunga mkono Afrika yenye haki zaidi, amani, na usaidizi.

Mara nyingi Afrika inakabiliwa na mantiki ya uchu na mara nyingi huakisiwa na umaskini, ufisadi, na vurugu. Tunawezaje kuvunja mizunguko hii, na jukumu la Wakatoliki ni muhimu kiasi gani katika michakato hii?

Afrika ni bara lenye utajiri wa rasilimali za binadamu, kiutamaduni, na asili, lakini mara nyingi hukabiliwa na mienendo inayozuia maendeleo yake: Umaskini, ufisadi, vurugu, na mantiki ya unyonyaji ambayo pia hutoka nje na kuwafanya watu walio tayari kuwa maskini waishio katika mazingira magumu kuwa maskini zaidi. Kuvunja mifumo hii kunahitaji kujitolea na uvumilivu. Kanisa Katoliki lipo Afrika kupitia shule, hospitali, vituo vya mapokezi, na kazi za upendo, ambazo mara nyingi hujumuisha mwitikio halisi wa mahitaji ya msingi ya watu. Lakini mwitikio wa Kanisa hauishii na kazi za upendo tu: unahusisha uundaji wa dhamiri na elimu ya vijana katika maadili ya utu, haki, na mshikamano. Hapa ndipo waamini Wakatoliki wanapoitwa kuchukua jukumu muhimu, si kama wanufaika wa ujumbe, bali kama wahusika wakuu wa mabadiliko katika maisha yao, katika jamii na taasisi mbalimbali.

Je, una matumaini gani kwa ziara hii ya kitume, katika nchi ambayo pia unaipenda sana?

Matumaini yangu ni kwamba Ziara hii ya Kitume itaacha alama kubwa katika nyanja tatu zinazohusiana kwa karibu: amani, mazungumzo, na ukuaji wa Kanisa mahalia. Amani, kwanza kabisa, katika nchi ambazo bado zina makovu ya migogoro na mgawanyiko, na ambapo uwepo wa Baba Mtakatifu unaweza kukuza hisia ya upatanisho. Mazungumzo, ambapo kukutana na mamlaka za kiraia na wawakilishi wa mila na tamaduni zingine za kidini kunaweza kufungua nafasi mpya za uelewano wa pande zote. Hatimaye, ukuaji wa Makanisa mahalia, mara nyingi madogo, wakati mwingine yametengwa, lakini daima ni wakarimu. Afrika ni bara changa, lenye imani na nguvu nyingi, na ziara ya Baba Mtakatifu ni kitendo cha kujiamini katika mustakabali wake, yaani mustakabali ambao Kanisa linakusudia kuendelea kuusindikiza kwa kujitolea na matumaini.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

12 Aprili 2026, 09:24