Tafuta

Papa Leo XIV,mkesha wa sala:Vita vinagawanya,matumaini yanaunganisha

Vita hugawanya,tumaini huunganisha.Kiburi hukanyaga,upendo huinua.Ibada ya sanamu hupofusha,Mungu aliye hai huangaza.Imani ndogo,chembe ya imani,inatosha kukabiliana pamoja,kama wanadamu na pamoja na wanadamu,katika saa hii ya kusisimua ya kihistoria.Ni katika tafakari ya Papa Leo XIV wakati wa Mkesha wa kuombea amani katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican,Aprili 11.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV ameongoza mkesha wa sala kwa ajili ya amani, Jumamosi jioni  tarehe 11 Aprili 2026 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Hata hivyo kabla ya kuanza sala hiyo, Papa alikwenda katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kuwasalimia na kuwashukuru waamini na mahujaji waliofika kuungana naye.

Papa akiwasalimia waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kabla ya sala
Papa akiwasalimia waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kabla ya sala   (@Vatican Media)

Akiwa katika Jukwaa mbele ya Basilika, Papa alisema:“Salamu za kidugu na kubwa sana kwenu nyote. Asante kwa uwepo wenu, kwa kuitikia wito huu, mwaliko huu wa kuungana na sauti zetu, mioyo yetu, na maisha yetu kuombea amani. Sote tuna amani mioyoni mwetu. Amani itawale kweli ulimwenguni kote na tuwe wabebaji wa ujumbe huu. Mungu anatusikiliza, Mungu anatusindikiza! Yesu alituambia kwamba pale palipo na wawili au watatu wamekusanyika kwa jina lake, yuko pamoja nao. Katika siku hizi za Oktava ya Pasaka, tunaamini sana uwepo wa Yesu aliyefufuka kati yetu.”

Papa akiwaelekea waamini na mahujaji kabla ya sala kwa ajili ya amani
Papa akiwaelekea waamini na mahujaji kabla ya sala kwa ajili ya amani   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea kusema kuwa “Sasa, tukiwa tumeungana katika kusali Rozari Takatifu, tukiomba maombezi ya Mama yetu Maria, tunataka kuwaambia ulimwengu wote kwamba inawezekana kujenga amani, amani mpya; kwamba inawezekana kuishi pamoja na watu wote wa dini zote, wa rangi zote; kwamba tunataka kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo tukiwa tumeungana kama kaka na dada, wote tukiwa tumeungana katika ulimwengu wa amani. Ombeni pamoja nasi! Asante kwa uwepo wenu! Mungu awasindikize  na wapendwa wenu leo ​​na siku zote. “ Papa aliongeza kwamba anawapatia baraka hapo na kisha kusali pamoja katika Basilika na kwamba wangeweza kufuatilia kwenye skrini. “Asante tena kufika!” Aliwapatia baraka.

Kwa njia hiyo mara baada ya Rosari Takatifu na Litania ya Bikira Maria, Papa Leo XIV  aliwageukia waamini waliokuwa ndani ya Basilika ya Mtakatifu Petro na kutafakarii:  “Kaka na dada, sala yetu ni kielelezo cha imani ile ambayo kwa mujibu wa Neno la Yesu, inaweza kuhamisha Mlima(Mt 17,20). Asante kwa kuitikia mwaliko  huu, kukusanyika hapa, kwenye  kaburi la Mtakatifu Petro, na katika maeneo mengi duniani ili kuomba amani.”

Kila tendo waliwasha mshumaa
Kila tendo waliwasha mshumaa   (@Vatican Media)

Vita vinagawanya, matumaini yanaunganisha

Papa aliendelea kusema, “Vita hugawanya, matumaini huunganisha. Kiburi hukanyaga, upendo huinua. Ibada ya sanamu hupofusha, Mungu aliye hai huangaza. Inatosha imani ndogo, chembe ya imani, wapendwa, kukabiliana pamoja, kama wanadamu na pamoja na wanadamu, saa hii ya kusisimua katika historia. Kiukweli, sala si kimbilio la kuepuka majukumu yetu, wala dawa ya kutuliza maumivu yanayosababishwa na dhuluma nyingi. Badala yake, ni jibu la bure, la ulimwengu wote, na la usumbufu kwa kifo: sisi ni watu ambao tayari tunafufuka! Ndani ya kila mmoja wetu, katika kila mwanadamu, Mwalimu wa ndani anafundisha amani, anatusukuma kukutana, anahamasisha sala. Basi tuinue macho yetu! Tuinuke kutoka kwenye kifusi! Hakuna kinachoweza kutufungia katika hatima iliyopangwa awali, hata katika ulimwengu huu ambapo makaburi yanaonekana hayatoshi, kwa sababu tunaendelea kusulibisha, kuharibu maisha, bila haki na bila huruma.

Tunajua vema kwamba haiwezakani amani kwa kila gharama

Mtakatifu Yohane Paulo II shuhuda wa amani bila kuchoka, kwa hisia katika muktadha wa mgogoro wa Iraq kunako 2003 alisema: “Mimi ninatoka katika kizazi cha aliyeishi Vita ya Pili ya Dunia na aliyenusurika. Ninawajibu wa kuwambia vijana wote, walio wadogo zaidi yangu, ambao hawakupata  uzoefu: “ Vita kamwe visitokee tena, kama alivyosema Paulo VI katika ziara yake ya kwanza katika Umoja wa Mataifa.” Lazima kufanya yote iwezekanavyo ! Tunajua vema kwamba haiwezakani amani kwa kila gharama. Lakini tunajua jinsi gani ilivyo uwajibikaji huu mkubwa”(san Giovanni Paolo II, Sala ya Malaika wa Bwana 16 Machi 2003).   Sala hutufundisha kutenda. Katika maombi, uwezekano mdogo wa kibinadamu unaunganishwa na uwezekano usio na kikomo wa Mungu. Mawazo, maneno, na matendo kisha huvunja mnyororo wa shetani wa uovu na kuwekwa katika utumishi wa Ufalme wa Mungu: Ufalme ambao hakuna upanga, hakuna ndege isiyo na rubani, hakuna kisasi, hakuna kupuuzia uovu, hakuna faida isiyo ya haki, bali ni heshima, uelewa, na msamaha pekee.

Sala kwa ajili ya amani
Sala kwa ajili ya amani   (@Vatican Media)

Kaka na dada wa Baba Mmoja aliye mbinguni unapotea

Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea:  Hapa tuna kizuizi cha ule upuuzi wa uweza wote ambao unaotuzunguka unazidi kuwa usiotabirika na wa fujo. Ulinganifu wa nguvu katika familia ya wanadamu unaharibika sana. Hata Jina takatifu la Mungu, Mungu wa uzima, linavutwa katika mazungumzo ya kifo. Ulimwengu wa kaka na dada wa Baba mmoja mbinguni umetoweka, na, kama katika ndoto mbaya, ukweli umejaa maadui. Kila mahali tunahisi vitisho, badala ya wito wa kusikiliza na kukutana. Kaka na dada, wale wanaoomba wanajua mapungufu yao wenyewe; hawaui na hawatishii kifo. Badala yake, wale ambao wamemgeuzia Mungu aliye hai  kisogo, wamekuwa watumwa wa kifo, wakijigeuza wenyewe na nguvu zao kuwa sanamu bubu, kipofu, na kiziwi(taz. Zab 115:4-8), ambao kwao wanajitolea kila thamani na kudai kwamba ulimwengu mzima upige goti."

Waamini katika sala
Waamini katika sala   (@Vatican Media)

Miungu binafsi inatosha na kujinadi na nguvu

Papa Leo XIV alisisitiza kuwa,“Inatosha ibada ya sanamu ya nafsi na fedha! Inatosha kwa kujinadi na nguvu! Inatosha vita! Nguvu ya kweli hudhihirishwa katika kutumikia maisha. Mtakatifu Yohane XXIII, kwa urahisi wa Kiinjili, aliandika: "Kila mtu hufaidika na amani: watu binafsi, familia, na familia nzima ya wanadamu." Na akirudia maneno ya Pio XII, kwa haraka aliongeza: "Hakuna kinachopotea kwa amani. Kila kitu kinaweza kupotea kwa vita." (Barua ya Kitume, Pacem in terris, 62).  Baba Mtakatifu Leo XIV kwa hiyo aliomba, “ tuunganishe nguvu za kimaadili na kiroho za mamilioni, mabilioni ya wanaume na wanawake, wazee na vijana, ambao leo wanaamini katika amani, ambao leo huchagua amani, ambao huponya majeraha na kurekebisha uharibifu ulioachwa na wazimu wa vita. Papa Leo XIV hakuishia hapo, bali alieleza kuwa, “Ninapokea barua nyingi kutoka kwa watoto wa maeneo ya migogoro: ukizisoma,  unagundua, pamoja na ukweli wa kutokuwa na hatia, hofu na ukatili wote wa vitendo ambavyo baadhi ya watu wazima hujivunia kwa fahari. Tusikilize sauti za watoto!

Kila tendo la Rosari, uliwashwa mshumaa kutoka Taa ya  Assisi ya amani
Kila tendo la Rosari, uliwashwa mshumaa kutoka Taa ya Assisi ya amani   (@VATICAN MEDIA)

Hakika, kuna majukumu ya kulazimisha kwa viongozi wa mataifa. Tunawalilia: acha! Huu ni wakati wa amani! Kaeni kwenye meza za mazungumzo na upatanisho, si kwenye meza ambapo silaha hupangwa na kifo kinapangwa! Hata hivyo, kuna jukumu kubwa sawa kwa sisi sote, wanaume na wanawake kutoka nchi nyingi tofauti: umati mkubwa unaokataa vita, kwa matendo, si maneno tu. Sala inatulazimisha kubadilisha kile kilichobaki cha vurugu mioyoni na akilini mwetu: tugeuke hadi Ufalme wa amani unaojengwa siku baada ya siku, nyumbani, shuleni, mitaani, jamii za kiraia na kidini, tukirudisha msingi kutoka katika mabishano na kujiuzulu kwa urafiki na utamaduni wa kukutana. Turudi kuamini katika upendo, kiasi, na siasa nzuri. Tujielimishe na kushiriki katika hayo moja kwa moja, kila mmoja akiitikia wito wake mwenyewe. Kila mtu ana nafasi yake katika picha hii nzuri ya kisanaa ya amani.

Mama wa amani utuombee
Mama wa amani utuombee   (@Vatican Media)

Rozari inatuunganisha

Rozari, kama aina nyingine za sala za kale, imetuunganisha jioni hii katika mdundo wake wa kawaida, unaotegemea marudio: amani hivyo huweka nafasi, neno baada ya neno, ishara baada ya ishara, kama mwamba unaobubujika tone kwa tone, kama kusuka kwenye kitanzi huendeleza harakati baada ya harakati. Hivi ni vipindi virefu vya maisha, ishara ya uvumilivu wa Mungu. Hatuhitaji kuzidiwa na kasi ya ulimwengu usio na uhakika wa kile tunachokifuatilia, ili kurudi kutumikia mdundo wa maisha, maelewano ya uumbaji, na kuponya majeraha yake. Kama Papa Francisko alivyotufundisha, "tunahitaji mafundi wa amani, walio tayari kuanzisha michakato ya uponyaji na kukutana upya kwa ustadi na ujasiri" (Fratelli Tutti, 225).Kiukweli, kuna 'usanifu' wa amani, ambapo taasisi mbalimbali za jamii huingilia kati, kila moja kulingana na uwezo wake, lakini pia kuna 'ufundi' wa amani unaotuhusisha sote" (FT, 231).

Kuomba amani ya kweli ulimwengu
Kuomba amani ya kweli ulimwengu   (@Vatican Media)

Duniani kote, ikiwa kila jumuiya inakuwa 'nyumba ya amani,' tunajifunza kutuliza uadui kupitia mazungumzo

Baba Mtakatifu aliomba kwa kaka na dada kwamba,  “turudi nyumbani tukiwa na dhamira hii ya kusali kila wakati, bila kuchoka, na kwa uongofu mkubwa wa mioyo. Kanisa ni watu wazuri katika huduma ya upatanisho na amani, likisonga mbele bila kuyumba, hata wakati wa kukataa mantiki ya vita kunaweza kugharimu kutokuelewana na dharau yake. Linatangaza Injili ya amani na linatufundisha kumtii Mungu kuliko wanadamu, hasa linapohusu hadhi isiyo na kikomo ya wanadamu wengine, walio hatarini kutokana na ukiukwaji wa sheria za kimataifa mara kwa mara.” Katika ulimwengu wote, ni matarajio kuwa kila jumuiya inaweza kugeuka kuwa “nyumba ya amani, mahali wanapojifunza kuondoa uadui kwa njia ya mazungumzo. Mahali ambapo wanatenda haki na kuhifadhi msamaha. Leo zaidi ya hapo awali, kiukweli, tunahitaji kuonesha kwamba amani si utopia"(Ujumbe wa Siku ya amani Duniani, 1° Januari  2026).

Watu wa mataifa kutoka mabara yote waliawasha taa kwa ajili ya amani
Watu wa mataifa kutoka mabara yote waliawasha taa kwa ajili ya amani   (@Vatican Media)

Sala

Kwa kuhitimisha Papa Leo XIV alisema “kaka  na dada wa kila lugha, watu, na taifa: sisi ni familia moja inayoomboleza, kutumaini, na kufufuka tena. "Haitakuwa na vita tena, tukio lisilo na kurudi; haitakuwa na vita tena,  huzuni na vurugu" (Mtakatifu Yohane Paulo II, Sala ya Amani, Februari 2, 1991). Wapendwa, amani iwe nanyi nyote! Ni amani ya Kristo aliyefufuka, tunda la sadaka yake ya upendo msalabani. Kwa hivyo, tunamgeukia Yeye katika maombi yetu: Bwana Yesu, ulishinda kifo bila silaha au vurugu: uliyeyusha nguvu yake kwa nguvu ya amani.

Tupe amani yako,kama wanawake wasio na uhakika asubuhi ya Pasaka, kama wanafunzi waliojificha na wenye hofu.

Tutumie Roho wako,pumzi inayotoa uzima, inayopatanisha, inayowafanya wapinzani na maadui kuwa kaka na dada.

Ututie moyo wa Maria, mama yako, aliyesimama na moyo uliochomwa chini ya msalaba wako, imara katika imani kwamba utafufuka tena.

Uzimu wa vita na uishe, na Dunia itunzwe na kupandwa na wale ambao bado wanajua jinsi ya kuzalisha, kulinda, na kupenda maisha.

Utusikilize, Bwana wa Maisha!

Kuomba amani ya kweli
Kuomba amani ya kweli   (@Vatican Media)
Sala ya kuombea zawadi ya amani 11 Aprili 2026
11 Aprili 2026, 20:05