Papa Leo XIV: Katekesi Kuhusu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: Wito wa Utakatifu

Utakatifu katika Kanisa unapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu na kwamba, haya ndiyo mapenzi ya Mungu na hujionesha katika kutimiza Mashauri ya Kiinjili, kielelezo cha utakatifu wa Kanisa. Watu wote wanaalikwa kuwa wakamilifu na hivyo kuhesabiwa haki katika Kristo Yesu; katika Ubatizo; na katika Ubatizo wa imani waamini wanafanywa kweli watoto wa Mungu na washiriki wa tabia ya Mungu, na hivyo watakatifu halisi na wanaonywa waishi vyema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipitisha Katiba ya Fumbo la Kanisa, yaani “Mwanga wa Mataifa” “Lumen gentium” tarehe 21 Novemba 1964. Hii ni Katiba inayozungumzia kuhusu: Fumbo la Kanisa na Kanisa kama Sakramenti katika Kristo Yesu, Kanisa kama Taifa la Mungu; Muundo wa Kihierarkia wa Kanisa na hasa Uaskofu; Waamini walei; Wito wa watu wote katika Kanisa kuwa watakatifu; Watawa; Tabia ya kieskatolojia ya Kanisa linalosafiri na umoja wa Kanisa lililo mbinguni; Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa katika Fumbo la Kristo Yesu na la Kanisa. Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 8 Aprili 2026 ilikita ujumbe wake katika Katiba ya Fumbo la Kanisa, yaani “Mwanga wa Mataifa” “Lumen gentium” mintarafu: Utakatifu na Mashauri ya Kiinjili katika Kanisa.  “Katika Kristo Kanisa ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote.” LG, 1. Katekesi hii imenogeshwa na sehemu ya Neno la Mungu inayokazia kuhusu maisha yanayompendeza Mungu: Utakatifu wa mwili na upendo wa kidugu. “Iliyobaki, ndugu, tunawasihi na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana. Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu. Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati.” 1The 4:1-3.

Wito wa watu wote katika Kanisa kuwa ni watakatifu
Wito wa watu wote katika Kanisa kuwa ni watakatifu   (@Vatican Media)

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika ile Sura ya Tano ya Fumbo la Kanisa wanakazia kuhusu: Wito wa watu wote katika Kanisa kuwa ni watakatifu: Utakatifu katika Kanisa; Wito wa watu wote kuwa watakatifu; namna nyingi za kutekeleza utakatifu ulio mmoja; pamoja na Njia za Utakatifu. Utakatifu katika Kanisa unapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu na kwamba, haya ndiyo mapenzi ya Mungu na hujionesha kwa namna ya pekee katika kutimiza Mashauri ya Kiinjili, kielelezo cha utakatifu wa Kanisa. Watu wote wanaalikwa kuwa wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu na hivyo kuhesabiwa haki katika Kristo Yesu; katika Ubatizo; na katika Ubatizo wa imani waamini wanafanywa kweli watoto wa Mungu na washiriki wa tabia ya Mungu, na hivyo watakatifu halisi na wanaonywa waishi iwastahilivyo watakatifu kwa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu na wawe na matunda ya Roho Mtakatifu, ili wafanywe watakatifu. Rej Gal 5:22; Rum 6: 22. Na kwamba, wanahitaji daima huruma ya Mungu na hivyo wasali kuomba msamaha wa dhambi. Mt 6:12. Kumbe, huu ni mwaliko kwa waamini kufuata nyayo za Kristo Yesu; watii mapenzi ya Mungu, wajitoe kwa moyo wote kwa ajili ya utukufu wa Mungu na huduma ya jirani. Hivyo utakatifu wa watu wa Mungu utazidi kuzaa matunda tele, kama inavyoshuhudiwa katika historia ya Kanisa kwa njia ya maisha ya watakatifu wengi. Mababa wa Kanisa wanasema, utakatifu si upendeleo wa watu wachache tu ndani ya Kanisa, bali ni zawadi inayowajukumisha Wabatizwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utukufu kwa Mungu na jirani zao. Upendo kwa Mungu na jirani ndio muhuri aliotiwa kila mfuasi wa kweli wa Kristo Yesu. Rej LG, 42.

Utakatifu na Mashauri ya Kiinjili Ndani ya Kanisa
Utakatifu na Mashauri ya Kiinjili Ndani ya Kanisa   (@Vatican Media)

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, waamini wanaitwa kutoa ushuhuda mkubwa sana mbele ya watu na hasa mbele ya wadhulumu. Kwa hiyo kifodini “Martyrium” kinathaminiwa na Mama Kanisa kuwa karama bora zaidi na uhakikisho mkuu wa upendo, ingawa ni waamini wachache wanaojaliwa neema ya kifodini, lakini kimsingi, waamini wote wanapaswa kuwa tayari kumkiri Kristo Yesu mbele ya watu, na kumfuata katika Njia ya Msalaba kati ya madhulumu ambayo hayakosekani kamwe katika Kanisa; hii ni alama ya imani na mapendo inayowasukumwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki na amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, njia za utakatifu wa maisha zinasimikwa katika: Upendo; Usikilizaji na Umwilishaji wa Neno la Mungu; Ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu; Kufunga na Kusali; mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili na kwamba, upendo ambao ni kifungo cha ukamilifu na utimilifu wa Sheria huziongoza njia zote za kutakatifuza, huzikamilisha na kuzielekeza zifikie kikomo chake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema Kristo Yesu, aliye Mwalimu na mfano wa Kimungu wa ukamilifu, analitakatifuza Kanisa, ndiye kichwa cha Fumbo la Mwili wake na Mchungaji mkuu wa Kanisa lake na kwamba, utakatifu wa maisha katika mwelekeo huu ni zawadi yake inayojidhihirisha katika maisha ya waamini wake, pale wanapoipokea kwa furaha na kuimwilisha katika matendo adili na matakatifu. Mtakatifu Paulo VI anakaza kusema, ili Kanisa liweze kushuhudia ukweli, lazima waamini wake wawe watakatifu, wenye nguvu na waaminifu, ambao Kristo Yesu anawafanyia mageuzi kutoka katika undani wa maisha yao na hivyo maisha ya kila mwamini yatamwakisi Kristo Yesu katika mwanga wa Roho Mtakatifu. Rej Rum 8: 29; LG, 40.

Utakatifu wa mwili na upendo wa kidugu
Utakatifu wa mwili na upendo wa kidugu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwamba, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanalielezea Kanisa Katoliki kuwa ni Takatifu daima, lakini bado lina safari kuuendea utimilifu wa utakatifu wake, tayari kumkiri Kristo Yesu mbele ya watu, na kumfuata katika Njia ya Msalaba kati ya madhulumu ambayo hayakosekani kamwe katika Kanisa pamoja na faraja ya Mungu. Uchungu wa uwepo wa dhambi ni mwaliko kwa waamini kutubu, kumwongokea na hatimaye, kujiaminisha kwa Kristo Yesu anayewapyaisha kwa njia ya upendo wake. Neema hii inalitaka Kanisa kuwakirimia waamini utume wanaopaswa kuutekeleza siku kwa siku, si tu kwa kujikita katika kanuni maadili, bali kielelezo cha maisha ya Kikristo katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na jumuiya ya waamini katika ujumla wao. Watawa wanayo dhamana kubwa katika maisha na utume wa Kanisa kama wanavyofafanua Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Sura ya 43 hadi 47. Hawa ni kielelezo cha sauti ya kinabii, wajenzi wa Ufalme wa Mungu na kwamba, tajiriba ya mang’amuzi ya Mashauri ya Kiinjili, ni zawadi ya Roho Mtakatifu inayowafanya baadhi ya waamini kujisadaka bila ya kujibakiza katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, huku wakisimika maisha yao katika: Utii, Ufukara na Usafi kamili, kielelezo kamilifu cha ushiriki wa maisha ya Kristo Yesu hadi pale Msalabani, mahali ambapo waamini wanakombolewa na kutakaswa. Itakumbukwa kwamba, hakuna jaribio lolote la mwanadamu ambalo haitakumbukwa na Mwenyezi Mungu, hadi mateso yanayowaunganisha waamini na Kristo Yesu na hivyo, kuwa ni njia ya utakatifu wa maisha. Hii ni neema inayogeuza na kubadilisha maisha hivyo kuwaimarisha katika kila jaribu, ikiwaonesha sio lengo la mbali kama lengo lao, bali kukutana na Mungu, ambaye alifanyika mwanadamu kwa upendo. Bikira Maria, Mama Mtakatifu wa Neno aliyefanyika mwili, daima awasaidie na kulinda safari yao.

Wito wa utakatifu wa maisha ni kwa waamini wote
Wito wa utakatifu wa maisha ni kwa waamini wote   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake kwa mahujaji na wageni waliohudhuria kwenye Katekesi yake anawataka waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo na amani. Kristo mfufuka awakirimie furaha na tumaini; huruma na upendo wake wa daima vikae nao daima. Kipindi cha Pasaka iwe ni fursa kwa waamini kumtolea Mungu sifa na utukufu kwa Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele. Amewaombea neema na baraka za Kristo Mfufuka zikao pamoja nao. Wafunikwe na upendo wa Kristo Yesu. Ushindi wake dhidi ya maovu na kifo uwakirimie ujasiri hasa vijana ili waweze kufuata kwa uaminifu mashauri ya Kiinjili hasa katika njia ya mifumo mbalimbali ya maisha ya kuwekwa wakfu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu uovu hauna nguvu tena na kifo kinakuwa njia ya mwanzo wa maisha mapya. Waamini wamwendee Kristo Yesu katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ili awajalie utakatifu wa maisha na hatimaye, wajenge urafiki na wajitahidi kupokea zawadi za Roho Mtakatifu na hivyo kuwa ni wahifadhi wa amani. Anawaalika vijana kuwa ni mashuhuda kwa shauku na ukarimu wa ujana wao, kwa uaminifu wao kwa Injili, daima, wakijitahidi kumfuasa Kristo Yesu aliye: Njia, Ukweli na Uzima. Kwa wagonjwa na wanandoa wapya, wajitahidi kuruhusu nuru ya Kristo Mfufuka kuwa ni faraja katika mioyo yao.

Utakatifu wa Maisha
08 Aprili 2026, 15:44

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >