Tafuta

Papa Leo XIV: Katekesi Kuhusu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: Liturujia Katika Fumbo la Kanisa

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walifanya mageuzi katika Liturujia ya Kanisa mintarafu: Biblia Mafundisho ya Mababa wa Kanisa na Liturujia ambayo Mama Kanisa amekuwa akiiadhimisha, mintarafu Mafumbo ya Maisha ya Kikristo yaani Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko. Kwa njia ya Liturujia ya Kanisa waamini wanafanyika kuwa ni wazao wateule, makuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa miliki ya Mungu ili wapate kutangaza fadhili za Mungu..

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI anasema, Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ilikuwa ni Pentekoste mpya kwa Kanisa Katoliki, kwa kutaka kusoma alama za nyakati, kusahihisha mapungufu yake, ili hatimaye, kuliwezesha Kanisa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kumletea mwanadamu maendeleo endelevu ya: kiroho na kimwili. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, lilikuwa ni tukio la matumaini ndani ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, wakatambua dhamana, wajibu na changamoto iliyokuwa mbele yao, wakaamua kujadili vipengele mbalimbali na hatimaye, kuvipigia kura. Ni Mtaguso uliowakusanya viongozi kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ili kujadili maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, chini ya uongozi na usimamizi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati huo akiwa katika nafsi ya Mtakatifu Yohane XXIII; Ukatafsiriwa kwa vitendo na Mtakatifu Paulo VI pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II. Baba Mtakatifu Benedikto XVI akapyaisha mafundisho yake kwa Katekesi makini kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Sala. Hayati Baba Mtakatifu Francisko akaendelea kujipambanua kwa kutaka ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu ili kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo Yesu, kila mmoja kadiri ya karama, wito na dhamana yake ndani ya Kanisa.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulifanya mageuzi kwenye Liturujia ya Kanisa
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulifanya mageuzi kwenye Liturujia ya Kanisa   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican tarehe 11 Oktoba 1962, katika mahubiri yake, alikazia kuhusu: Upendo ambao Kristo Yesu ameonesha kwa Kanisa lake, licha ya dhambi, udhaifu na mapungufu ya kibinadamu na hata wakati mwingine, kumezwa na malimwengu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kurejea tena katika chemchemi ya upendo ule wa awali ulioneshwa na Kristo Yesu kwa Kanisa lake: Moja, takatifu, katoliki na la mitume. Hili ni Kanisa linalotumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayomwilishwa katika imani tendaji. Kanisa katika upendo, unyenyekevu na sadaka, linakabidhiwa utume wa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Kristo na wa Mungu; kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na utamadunisho, ili kushiriki: furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya walimwengu. Mkazo ni ushiriki mkamilifu wa ukuhani wa waamini wote unaowawezesha kushiriki sadaka ya Ekaristi Takatifu, kwa kupokea Sakramenti za Kanisa, kwa kusali na kwa njia ya ushuhuda wa maisha matakatifu, toba, wongofu wa ndani, kwa kujikana na kwa upendo wenye utendaji; Umoja wa watu wa Mungu ukipewa kipaumbele cha kwanza. Kanisa litambue kwamba, maskini wanao upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa hakika Kanisa ni Sakramenti ya umoja inayowaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na hivyo kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Ni jukumu la Mama Kanisa kuendelea kujikita katika Mapokeo, sera na mikakati ya shughuli za kiuchungaji. Mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Huu pia ni ni mwaliko wa kujenga na kudumisha ushirika wa Kanisa, ili wote wawe na umoja kama Kristo Yesu alivyojisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Mkazo ni ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu katika Ibada ya Misa Takatifu
Mkazo ni ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu katika Ibada ya Misa Takatifu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, anaendeleza Mzunguko wa Katekesi unaojikita katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji Mpya wa Nyaraka zake, ili kugundua tena uzuri na umuhimu wa tukio hili la Kikanisa, Kipindi cha neema ambacho kwa hakika, Mama Kanisa amekifaidi sana katika Karne ya ishirini. Kumbe, hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Katiba ya “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia” inaelezea kanuni za jumla za marekebisho na ukuzaji wa Liturujia Takatifu; Fumbo Takatifu la Ekaristi, Sakramenti nyingine na visakramenti; Liturujia ya Vipindi; Mwaka wa Liturujia wa Kanisa, Muziki Mtakatifu; na hatimaye, ni Sanaa Takatifu na Vifaa vitakatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafafanua nafasi ya Liturujia katika fumbo la Kanisa kwa kusema kwamba, maana kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu.” Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waoneshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo Yesu na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli. Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana lakini lenye mambo yasiyoonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye kufanya hija.

Umoja na Ushirika wa Watu wa Mungu ipewe kipaumbele cha kwanza
Umoja na Ushirika wa Watu wa Mungu ipewe kipaumbele cha kwanza   (@Vatican Media)

Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya kimungu, yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo yaelekee mji ujao tunakoelekea. Hivyo Liturujia kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa wawe hekalu takatifu la Bwana, makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo.  Wakati huohuo kwa namna ya ajabu Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumhubiri na kumshuhudia Kristo Yesu; na kwa njia hiyo inawaonesha wale walio nje [nalo,] Kanisa lililo ishara iliyoinuliwa juu kati ya Mataifa, ambayo chini yake watoto wa Mungu waliotawanyika wakusanyika katika umoja mpaka liwepo zizi moja chini ya mchungaji mmoja. Rej. SC, 2. Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 20 Mei 2026 imenogeshwa na sehemu ya Neno la Mungu: “Akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo:” Ef 1:9-10. Katekesi hii imehudhuriwa pia na Mheshimiwa Sana Aram I wa Wakatoliki wa Kanisa la Kitume la Armenia pamoja na ujumbe wake. Kwa njia ya Liturujia ya Kanisa waamini wanafanyika kuwa ni wazao wateule, makuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa miliki ya Mungu ili wapate kutangaza na kushuhudia fadhili za Mungu. Rej. 1Pt 2:9. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walifanya mageuzi makubwa katika Liturujia ya Kanisa mintarafu: Maandiko Matakatifu, Mafundisho ya Mababa wa Kanisa na Liturujia ambayo Mama Kanisa amekuwa akiiadhimisha, mintarafu Mafumbo ya Maisha ya Kikristo yaani Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu na kupaa kwake mbinguni na kwamba, hii ni Sakramenti inayowaunganisha waamini kwa jina la Kristo Yesu na hatimaye, kuwazamisha katika Fumbo hili kuu. Katika Sakramenti hii, Kristo Yesu anaendelea kutenda kwa nguvu ya Roho wake Mtakatifu; anatakatifuza na kuliunganisha Kanisa katika sadaka yake kuu inayotolewa kwa Baba yake wa mbinguni.

Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili
Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili   (@Vatican Media)

Kristo Yesu, Kuhani mkuu anaendelea kutekeleza dhamana yake katika Neno linalotangazwa, Sakramenti za Kanisa zinapoadhimishwa na kwa njia ya huduma ya Mapadre, yupo hasa chini ya Maumbo ya Mkate na Divai, yaani Ekaristi Takatifu na wanapoiadhimisha kwa uchaji, waamini wanageuka kuwa nao ni Ekaristi Takatifu, sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, Makao makuu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Waamini wanashiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu kwa akili, kwa moyo na kwa matendo wakielewa vyema Fumbo hilo kwa njia ya matendo ya kiliturujia na Sala. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Leo XIV huu ni ufunuo wa Kanisa katika sala. Liturujia ni kielele na chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, Huduma kwa maskini na kuwaimarisha katika kulimwilisha Fumbo la Pasaka katika maisha yao. Waamini kwa kutangaza Neno la Mungu, kwa kuadhimisha Sakramenti za Kanisa na kusali wanahimizwa na kutiwa shime na Mama Kanisa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa matendo ya ndani na yale ya nje. Waamini wanakumbushwa kwamba, Ibada ya kiroho inapaswa kuwa ni kielelezo cha maisha mapya. “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Rum 12:1.

Ujumbe wa Mh. Sana Aram I wa Wakatoliki wa Armenia amehudhuria
Ujumbe wa Mh. Sana Aram I wa Wakatoliki wa Armenia amehudhuria

Kumbe, Liturujia ina nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwani Liturujia kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa wawe hekalu takatifu la Bwana, makao ya Mungu katika Roho. Hii ni changamoto anasema Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, Kanisa linapaswa kuwa wazi, likionesha ukarimu kwa wote. Roho Mtakatifu anayeishi na kutumika, ndiye anaye wapeleka watu kwa Kanisa na kwamba watu wote wanapaswa kuwa ni mashuhuda na watangazaji hodari wa Habari Njema ya Wokovu, wakijitahidi kujenga na kudumisha umoja kwa kutambua kwamba wote wamealikwa kwenye karamu ya Mwanakondoo. Kumbe, wanapaswa kutenda haki na kuonesha utakatifu wa maisha. Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaalika waamini kujiruhusu wao wenye kuumbwa ndani mwao na Ibada, alama, ishara na zaidi ya yote uwepo hai wa Kristo Yesu katika Liturujia ambayo watapata fursa ya kuitafakari kwa kina kwa Katekesi zijazo.

Papa Leo XIV Liturujia
20 Mei 2026, 15:56

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >