Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV alianza Ibada ya Mkesha wa Jumamosi kuu kwa Liturujia ya Mwanga, ambamo alibariki moto wa Pasaka; akaadhimisha Liturujia ya Neno, Liturujia ya Ubatizo na Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV alianza Ibada ya Mkesha wa Jumamosi kuu kwa Liturujia ya Mwanga, ambamo alibariki moto wa Pasaka; akaadhimisha Liturujia ya Neno, Liturujia ya Ubatizo na Liturujia ya Ekaristi Takatifu.  (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV: Kesha la Pasaka ya Bwana 2026: Mashuhuda wa Fumbo la Ufufuko

Baba Mtakatifu Leo XIV alianza Ibada ya Mkesha wa Jumamosi kuu kwa Liturujia ya Mwanga, ambamo alibariki moto wa Pasaka; akaadhimisha Liturujia ya Neno, Liturujia ya Ubatizo ambamo amewabatiza Wakatekumeni wapya 10 kutoka: Italia, Korea, Uingereza na Ureno na hatimaye alihitimisha kwa kuadhimisha Liturujia ya Ekaristi Takatifu! Kesha la Pasaka ni mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na watangazaji wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam na matashi mema ya Sherehe ya Pasaka kwa mwaka 2026 zilizochapishwa kwenye Gazeti la L’Ossevatore Romano anasema, Kristo Yesu ni Bwana wa uzima, alikuwa amekufa, lakini amefufuka ni mzima na ni mshindi. Na sisi tunayo hakika ya ufufuko huu. Kristo Yesu amefufuka kweli kweli, Kristo Yesu, Mfalme wa ushindi utuhurumie! Kesha la Pasaka ni Mama wa Mikesha Yote ya Kanisa inayotawaliwa kwanza kabisa na kimya kikuu, ni kesha la Ufufuko wa Kristo Yesu. Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa analiita Kesha hili la Pasaka kuwa ni “Mama wa mikesha yote” kwa sababu katika usiku huu, Kanisa lipo macho kusubiria ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Ni siku ambayo Kanisa linatafakari kwa kina historia nzima ya ukombozi tangu kuumbwa kwa ulimwengu hadi siku hii Takatifu ambapo Kristo Yesu alifufuka kutoka wafu, siku ya tatu baada ya mateso na kifo chake. Rej. Mt. 16:21-23; Mk 8:31; Lk 9:21-22). Mkesha huu umegawanyika katika sehemu kuu nne: Baba Mtakatifu Leo XIV alianza Ibada ya Mkesha wa Jumamosi kuu kwa Liturujia ya Mwanga, ambamo alibariki moto wa Pasaka; akaadhimisha Liturujia ya Neno, Liturujia ya Ubatizo ambamo amewabatiza Wakatekumeni wapya 10 kutoka: Italia, Korea, Uingereza na Ureno na hatimaye alihitimisha kwa kuadhimisha Liturujia ya Ekaristi Takatifu!

Papa Leo XIV ameongoza Liturujia ya Neno
Papa Leo XIV ameongoza Liturujia ya Neno   (@VATICAN MEDIA)

Huu ni mkesha unaoragibisha maridhiano na amani inayopata chimbuko lake katika mwanga wa Mshumaa wa Pasaka, kielelezo cha Kristo Mfufuka. Waamini wanashiriki kikamilifu katika utume huu, kwa kurudia tena Ahadi zao za Ubatizo baada ya kutembea kwa siku arobaini Jangwani na kwa sasa wanashiriki Fumbo hili kuu la Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili, akateswa na hatimaye kufa kifo cha Msalaba, ili kufunua huruma, upendo na msamaha wake usiokuwa na kifani, kwa kuyamimina maisha yake. Liturujia ya Neno la Mungu imewakumbusha waamini kazi ya Uumbaji iliyokamilishwa kwa kuumbwa kwa mwanadamu katika sura na mfano wa Mungu, na hatimaye, akakabidhiwa kulinda, kutunza na kuendeleza kazi ya uumbaji. Mwanadamu alipotenda dhambi ya asili, akamwonesha Uso wa huruma na msamaha, kielelezo cha hija ya maisha inayokita mizizi yake katika neema na upatanisho.

Liturujia ya Ubatizo Kwa Wakatekumeni 10
Liturujia ya Ubatizo Kwa Wakatekumeni 10   (@Vatican Media)

Yote haya yanajionesha katika Wito na sadaka ya Abramu; Ukombozi wa Waisraeli kutoka utumwani Misri, mwanzo wa maisha mapya na njia ya amani, inayomwezesha Roho Mtakatifu kufanya mageuzi na kubadilisha mioyo ya watu wateule wa Mungu, waliokengeuka kutokana na dhambi iliyowagawa na kuwasababishia kifo. Wakaona nguvu ya upendo wa Mungu unaounganisha na kuwakirimia tena maisha, kielelezo kwamba, kwa njia ya Pasaka ya Bwana, waamini wanateseka, kufa na hatimaye kufufuka na Kristo Yesu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, huku wakiwa na ushirika wa watakatifu wa Mungu, na hivyo wanafanyika mawe hai ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Rej 1Pet 2:4-5. Mwinjili Mathayo anasimulia jinsi ambavyo siku ile ya kwanza ya Juma wanawake waliokuwa na uchungu pamoja na wasi wasi walivyokwenda kulitazama kaburi la Kristo Yesu, wakidhani kwamba, wangelikuta kaburi likiwa limesilibwa na kulindwa na Askari, kielelezo cha dhambi, inayowatenganisha waamini pamoja na Mungu wao; kizingiti kinachofisha matumaini. Lakini imani na upendo wa Maria Magdalena na Mariamu yule wa pili ukawaweza kuwa ni mashuhuda wa kwanza wa Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, wakaona na kushuhudia nguvu ya upendo wa Mungu, maisha na uzima wa milele, dhidi ya utamaduni wa kifo, chuki na uhasama, na tazama wakakutana na Kristo Mfufuka akisema: “Salamu! Mt 28:9.

Kesha la Pasaka: Mwaliko wa kuwa ni Mashuhuda wa Ufufuko wa Bwana
Kesha la Pasaka: Mwaliko wa kuwa ni Mashuhuda wa Ufufuko wa Bwana   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hii ni changamoto kwa waamini kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka kwa maneno na imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa kukita maisha katika Injili ya amani na umoja: Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, “Ingawa sisi ni wakristo wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja. Haya ni maneno kutoka katika Kauli mbiu yake ya kiaskofu: “In Illo uno unum.”Katika Liturujia ya Ubatizo ambamo amewabatiza Wakatekumeni wapya 10 kutoka: Italia, Korea, Uingereza na Ureno, anasema, Wakatekuneni hawa watazaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu na hivyo kuwa ni Mashuhuda wa Injili na waamini watapata tena fursa ya kurudia Ahadi zao za Ubatizo, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika medani mbalimbali za maisha. Hata leo hii bado kuna makaburi yaliyosilibwa kwa ukosefu wa imani, woga, uchoyo na ubinafsi; chuki na uhasama mambo yanayopelekea kuvunja uhusiano kati ya watu kwa njia ya: vita, ukosefu wa haki msingi za binadamu pamoja na utengano kati ya watu na Mataifa.

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni Mashuhuda wa Ufufuko wa Kristo
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni Mashuhuda wa Ufufuko wa Kristo   (@Vatican Media)

Hatimaye, Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuondokana na mwelekeo wa maisha ya namna hii, hata kama itawagharimu, kwani kuna mfano wa watu ambao walijisadaka na leo hii matunda ya kazi zao yanaonekana, kielelezo cha neema na nguvu ya Kristo Mfufuka iliyokuwa ikitenda kazi ndani mwao katika upendo na ukweli na kwa ujasiri wa Neno la Mungu na nguvu walizopokea kutoka kwa Mungu, wakatenda yote haya kwa sifa na utukufu wa Mungu. Waamini waongozwe na mifano yao bora ya maisha na katika Kesha la Pasaka waamini wajizatiti kukuza na kudumisha maua na matunda ya Pasaka yaani maridhiano, haki na amani.

Mkesha wa Pasaka 2026
05 Aprili 2026, 15:02