Papa Leo XIV:Inawezekana kuishi kwa amani&kuthamini tofauti
Vatican News
Kufuatia ziara yake katika Msikiti wa Algiers Jumatatu alasiri, tarehe 13 Aprili 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV alifanya pia ziara ya faragha katika Kituo cha Kukaribisha na Urafiki cha Masista Wamisionari wa Agostiniani ili kutoa heshima ya kumbukumbu ya masista waliouawa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Algeria na kuwashukuru Masista hao kwa huduma yao ya upendo.
Papa alikaribishwa na jumuiya iliyoko katika Wilaya ya Bab El Oued, takriban kilomita 16 kutoka mji wa Algiers. Wakati wa ziara yake, alikaa na watawa hao na kukutana na wale wanaoendeleza dhamira yao ya ukarimu, elimu, na urafiki katika muktadha uliojaa kumbukumbu na upatanisho. Ziara ya Papa Leo XIV ilitengwa hasa kwa ajili ya kuwakumbuka watawa wawili wa Jumuiya hiyo ambao walikuwa miongoni mwa mashahidi 19 wa Algeria waliouawa kati ya 1994 na 1996 wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Sr. Esther Paniagua Alonso na Sr. Caridad Álvarez Martín waliuawa mnamo tarehe 23 Oktoba 1994 wakati wa "Muongo Mweusi," kama Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Algeria vinavyojulikana, walipokuwa njiani kuelekea ibada ya Misa.
Shuhuda hadi kufikia hatua ya kuuawa kishahidi
Kulingana na taarifa ya Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Vatican, Papa Leo XIV alitafakari na ushuhuda wao ndani ya ushuhuda mpana wa mashahidi wa Algeria, akielezea kwamba maisha yao yanaonesha mwelekeo ulioandikwa kwa undani katika hali ya kiroho ya Mtakatifu Agostino: ule wa ushuhuda, hata kufikia hatua ya kuuawa kishahidi. "Uwepo wenu hapa unamaanisha mengi," alisema Papa huku akikumbuka ziara iliyopita,na alizungumzia zawadi ambayo Mtakatifu Agostino anawakilisha katika sehemu hiyo ya dunia, ambayo inahamasisha "heshima kwa utu wa kila mtu," akibainisha kwamba "inawezekana kuishi kwa amani, kuthamini tofauti."
Hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, hii ilikuwa jumuiya ambayo Masista Wamisionari wa Mtakatifu Agostino waliishi, na ambapo masista hao wawili waliouawa waliondoka kwa ajili ya utume wao wa kila siku. Kumbukumbu yao, Papa alikumbusha, inabaki kuwa uwepo hai unaoendelea kuangazia maana ya ushuhuda wa Kikristo.
Katika mwisho wa mkutano huo, Papa Leo XIV aliwashukuru masista kwa huduma yao na kuwatia moyo waendelee katika utume huo. Pia alikumbusha kwamba ukumbusho wa mashahidi 19 wa Algeria unaadhimishwa tarehe 8 Mei, siku ile ile ya kuchaguliwa kwake, akiunganisha kumbukumbu yao na upeo wa kiroho wa pamoja wa ushuhuda na matumaini.
Kituo cha Kukaribisha na Urafiki
Mjengo huo kwa sasa unaendeshwa na Masista wawili kati ya watatu wanaoishi katika nyumba ya huko Basilika ya Mama Yetu wa Afrika huko Algiers. Hutumika kama mahali pa kukutana wazi kwa wakazi wa eneo hilo, ukitoa shughuli za kila siku zinazofanywa kwa usaidizi wa walimu wa kitaalamu wa mataifa mbalimbali.
Shughuli hizi zinajumuisha usaidizi wa baada ya shule kwa watoto na kozi za lugha ya Kifaransa na Kihispania kwa vijana na watu wazima, pamoja na warsha kwa wanawake, wanaojifunza kushona, kufuma, uchoraji, na kutengeneza vito.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.
