Tafuta

Kristo Yesu amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia watu maisha na uzima wa milele. Kwa ufufuko wake amewajalia waamini maisha mapya. Kristo Yesu amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia watu maisha na uzima wa milele. Kwa ufufuko wake amewajalia waamini maisha mapya.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Fumbo la Pasaka ya Bwana: Kiini Cha Imani ya Kanisa

. Pasaka ni kielelezo cha uumbaji mpya uliofanywa na Kristo Yesu Mfufuka na huo ni mwanzo wa maisha mapya na ya milele na ushindi wa Mwenyezi Mungu dhidi ya adui wa kale. Kwa hakika mwanadamu katika Ulimwengu mamboleo anayo kiu ya Injili ya matumaini na kwamba, kwa waamini kufufuka pamoja na Kristo, wanawajibika kwa sasa kutangaza na kuishuhudia Injili ya matumaini sehemu mbalimbali za dunia, watangaze kwa watu wote furaha ya Injili ya Ufufuko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha Ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia watu maisha na uzima wa milele. Kwa ufufuko wake amewajalia waamini maisha mapya. Hiki ndicho kiini cha imani ya Kanisa kwamba, Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti na kuwa kifo hakina tena sauti ya mwisho juu ya maisha ya binadamu. Huu ni ukweli ambao si rahisi kuupokea kwani daima mwanadamu anaandamwa na nguvu ya kifo ndani na nje ya maisha yake kwa njia ya dhambi inayokita mizizi yake katika maisha ya watu na kuwafanya wasiweze kuponyoka na kusonga mbele; wanapoandamwa na hali ya kukata na kujikatia tamaa; upweke hasi unaopekenya Injili ya matumaini; wasiwasi unaposhika kasi na hivyo kuondoa ile furaha ya Injili; pale waamini wanapojisikia kuelemewa na upweke hasi au kuhisi kwamba, wanasalitiwa au kukataliwa; wanapoelemewa na udhaifu wao, mahangaiko pamoja na changamoto za kila siku, hapo waamini wanahisi kuishiwa na matumaini na hivyo kushindwa kuona njia ya kuweza kuwaondoa katika hali kama hiyo!

Kristo Yesu amefufuka kwa wafu ameshinda dhambi na mauti
Kristo Yesu amefufuka kwa wafu ameshinda dhambi na mauti   (@Vatican Media)

Hii ni sehemu ya mahuburi yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Sherehe ya Pasaka ya Bwana, Dominika tarehe 5 Aprili 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.Fumbo la kifo daima linaendelea kujionesha katika: Ukosefu wa haki msingi za binadamu; Ubinafsi; Nyanyaso dhidi ya maskini; Ukosefu wa uangalizi makini kwa watu dhaifu na wanyonge ndani ya jamii; vita; madonda na kilio cha watu wengi sehemu mbalimbali za dunia; Uchu wa fedha, mali na madaraka; matumizi mabaya ya rasilimali za dunia pamoja na vita inayopelekea mauaji na uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka ni mwaliko wa kuangalia juu kwa matumaini sanjari na kuendelea kuboresha ari na moyo unaopandikiza mbegeu ya ushindi, kama ilivyokuwa kwa Maria Magdalena na yule mwanamke mwingine kuendelea kugundua Kaburi la Kristo Yesu ambalo lilikuwa tupu, ili kutoa fursa ya kuwezesha kuchipuka tena maisha mapya.

Ufufuko wa Kristo ni chemchemi ya maisha mapya
Ufufuko wa Kristo ni chemchemi ya maisha mapya   (@VATICAN MEDIA)

Kristo Mfufuka yu hai na anaendelea kuishi kati ya waja wake na kwa njia ya Ufufuko wake, anawawezesha waamini kuuona mwanga wake na hivyo kuchipusha tena matumaini kwani kifo hakina tena neno la mwisho katika maisha ya mwanadamu na kwamba, mwanadamu anaendelea kufanya hija ya ukamilifu katika maisha yake, kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, waamini pia wameifia dhambi na hivyo kufufuka na Kristo Yesu. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, Ufufuko wa Kristo siyo tukio la kale, unayo nguvu muhimu ambayo imeupenya ulimwengu huu. Pale ambapo kila kitu kinaonekana kama kimekufa, ghafla ishara za ufufuko huchipua. Ni nguvu isiyoweza kuzuilika. Mara nyingi inaonekana kama vile Mungu hayupo. Kila upande unaonekana ukosefu wa haki, uovu, kutokujali na ukatili ambavyo huzidi kuendelea. Lakini ni ukweli pia kwamba, daima katikati ya giza kitu fulani kipya kuchipuka katika uhai na baada ya muda huzaa matunda. Rej Evangelii gaudium, 276.

Ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini
Ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini   (@Vatican Media)

Hatimaye, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya matumaini na ukumbusho kwamba, katika Fumbo la Ufufuko, kuna uumbaji mpya unaotendeka kila siku, kama ilivyokuwa Siku ile ya kwanza ya juma. Rej Yn 20:1. Ufufuko wa Kristo Yesu unawarejesha waamini katika kazi ya Uumbaji, Siku ya kwanza, Mwenyezi Mungu alipoumba mbingu na dunia, mwanzo wa maisha mapya yenye nguvu zaidi ya kifo yanayochipuka kwa ajili ya binadamu. Pasaka ni kielelezo cha uumbaji mpya uliofanywa na Kristo Yesu Mfufuka na huo ni mwanzo wa maisha mapya na ya milele na ushindi wa Mwenyezi Mungu dhidi ya adui wa kale. Kwa hakika mwanadamu katika Ulimwengu mamboleo anayo kiu ya Injili ya matumaini na kwamba, kwa waamini kufufuka pamoja na Kristo, wanawajibika kwa sasa kutangaza na kuishuhudia Injili ya matumaini sehemu mbalimbali za dunia, huku wakiwa wameambatana na Maria Magdalena, watangaze kwa watu wote furaha ya Injili ya Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu na pale ambapo utamaduni wa kifo unaendelea kutawala, mwanga angavu wa maisha upate kung’ara! Kristo Pasaka ya waamini, aendelee kuwabariki na kuwakirimia walimwengu amani yake.

Pasaka ya Bwana 2026
05 Aprili 2026, 15:34