Tafuta

Wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo, Ijumaa tarehe 10 Aprili 2026 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican. Wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo, Ijumaa tarehe 10 Aprili 2026 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican.   (@Vatican Media)

Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo: Uchaguzi Mkuu wa Patriaki

Baba Mtakatifu Leo XIV amegusia asili ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo, matumaini katika Kristo Mfufuka yanawaalika wajumbe hawa kutokuwa na woga, bali watoe fursa kwa Roho Mtakatifu aweze kuwaongoza katika uchaguzi wao, ili kumpata mtu mwenyeheri, atakayeliongoza Kanisa la Baghdadi kwa mwanga wa imani, ushirika na majadiliano ya kiekumene, huku akiwa na moyo mweupe pe! Papa ametambua na kuthamini mchango wa Kardinali Louis Sako.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo (Chaldean Catholic Church) ni mkutano mkuu wa Maaskofu wa Kanisa hilo, linaloongozwa na Patriaki wa Babilonia ya Wakaldayo, Kardinali Louis Raphael Sako ambaye amemaliza muda wake wa uongozi. Sinodi hii ni chombo muhimu cha maamuzi, mageuzi, na ushirikiano katika Kanisa la Wakaldayo nchini Iraq na katika maeneo ya kidiaspora. Pamoja na mambo mengine, Sinodi hii inalenga: kusoma alama za nyakati, upyaishaji wa maisha na utume wa Kanisa; Mageuzi katika mchakato wa maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, ili yaweze kupatikana na kueleweka vyema zaidi kwa waamini, sanjari na kujadili kwa kina na mapana hali halisi ya Wakristo huko Iraq na maeneo mengine ambako haki, amani na maridhiano ni changamoto pevu kwa wakati huu. Wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo, Ijumaa tarehe 10 Aprili 2026 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican. Wajumbe hawa wanahudhuria mkutano mkuu wa uchaguzi ambao umewakutanisha mjini Roma kuanzia tarehe 9 Aprili hadi Jumatano tarehe 15 Aprili 2026, ili kufanya uchaguzi wa Patriaki mpya wa Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amegusia asili ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo, matumaini katika Kristo Mfufuka yanawaalika wajumbe hawa kutokuwa na woga, bali watoe fursa kwa Roho Mtakatifu aweze kuwaongoza katika uchaguzi wao, ili kumpata mtu mwenyeheri, atakayeliongoza Kanisa la Baghdadi kwa mwanga wa imani, ushirika na majadiliano ya kiekumene, huku akiwa na moyo mweupe pe!

Papa Leo XIV akizungumza na wajumbe wa Sinodi ya Kanisa la Baghdad
Papa Leo XIV akizungumza na wajumbe wa Sinodi ya Kanisa la Baghdad   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV ametambua na kuuthamini mchango wa Kardinali Louis Raphael Sako katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu amewataka wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo kuwa makini, wakweli na watu wazi katika matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii na kwamba, wao ni alama ya matumaini katika ulimwengu unaosiginwa na: Vita, chuki na uhasama, dhuluma, nyanyaso na ukatili wa hali ya juu, wao wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa amani. Watambue kwamba, utume wao ni kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka hata ikibidi kwa kuyamimina maisha yao. Baba Mtakatifu Leo XIV amesema asili ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo inapata chumbuko lake katika Mapokeo ya zamani ya Kanisa, mahali ambapo panafumbata historia ya wokovu; ni mahali penye amana na utajiri wa imani, tamaduni, ari na moyo wa kimisionari, kumbe wanaalikwa kutunza amana na utajiri huu kwa ujasiri na uaminifu. Ni Kanisa ambalo limepitia changamoto kubwa na limebaki na makovu ya vita, alama zinazogeuka kuwa ni kielelezo cha matumaini, ufufuko na maisha mapya. Katika mwanga wa Kristo Mfufuka, maadhimisho ya Sinodi hii ni mwaliko wa kuondokana na hofu pamoja na woga, kwa kujikita kikamilifu katika uchaguzi wa Patriaki mpya atakayeliongoza Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo, kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu awe ni chemchemi ya maelewano yanayobubujika kutoka katika sakafu ya Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu.

Asili ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo Mapokeo ya Kanisa
Asili ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo Mapokeo ya Kanisa   (@Vatican Media)

Patriaki mpya atakayechaguliwa awe kweli ni Baba katika imani, kielelezo cha umoja na ushirika, mnyenyekevu na awe ni mtu anayejielekeza katika ujenzi wa ushirika wa Kanisa katika upendo, huku akionesha heshima kwa kila mwamini. Rej 1Kor 13: 4-8. Patriaki mpya awe ni mtu wa heri, mtakatifu katika maisha ya kila siku, mchungaji mwenye kipaji na utamaduni wa kusikiliza kwa makini na anayetambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma na kwamba, awe ni mtu anayejitahidi kuwa ni sauti ya kinabii katika maisha na utume wa Kanisa. Awe ni mtu wa sala, shuhuda, mjenzi na mragibishaji wa umoja katika upendo, kwa kushirikiana na kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro sanjari na kukuza majadiliano ya kiekumene na waamini wa Makanisa mengine. Baba Mtakatifu Leo XIV ametambua na kuuthamini mchango wa Kardinali Louis Raphael Sako katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa upyaisho wa maisha ya kiroho; na kuendelea kuwa waaminifu katika Mapokeo ya Kanisa mintarafu liturujia na maisha ya kiroho yanayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Baba Mtakatifu Leo XIV amewataka wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo kuwa makini, wakweli na watu wazi katika matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, daima wajitahidi kulijenga Kanisa kwa ushuhuda wa maisha yao adili na matakatifu; wajizatiti katika malezi na majiundo ya makleri; wawe karibu na waamini wao katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji, ili waweze kuwa imara katika imani, matumaini na mapendo, waendeleo kubaki katika nchi yao “licha ya patashika nguo kuchanika ya vita na migogoro ya kijamii.” Waendelee kufurahia haki zote za kiraia, uhuru wa kidini na kamwe wasifanywe kuwa ni “watu wa kuja au watu wa daraja la pili katika nchi yao wenyewe.”

Papa Leo XIV ametambua mchango wa Kardinali Sako
Papa Leo XIV ametambua mchango wa Kardinali Sako   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka wajumbe hawa kutambua kwamba, wao ni alama ya matumaini katika ulimwengu unaosiginwa na: Vita, chuki na uhasama, dhuluma, nyanyaso na ukatili wa hali ya juu, wao wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa amani na utulivu unaosimikwa katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni na kamwe wasiwe ni watu wa kutaka kulipiza kisasi. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu awe ni kielelezo cha uwepo wake hai katika imani na upendo kwa kuendelea kuwasha moto wa matumaini na kamwe wasiogope kwani Kristo Mfufuka anatanguzana pamoja nao. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za Kitume.

Sinodi ya Wakaldayo
11 Aprili 2026, 17:11