Umuhimu wa Mafuta Matakatifu Katika Maisha na Utume wa Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta na kuweka wakfu Krisma ya Wokovu, ni ufunuo wa Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo unaofumbatwa katika huduma, karama na neema mbalimbali za Roho Mtakatifu katika hija ya maisha yake kumwendea Kristo Yesu. Mafuta ni alama ya ushirika, furaha, upendo na mshikamano. Ni alama ya imani inayoimarisha vifungo vya upendo kwa njia ya Roho Mtakatifu ili kutangaza na kushuhudia: Ukuu, uzuri na utakatifu wa familia ya Mungu. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, kamwe hawatindikiwi na mafuta ya neema ya imani, matumaini na mapendo. Huu ni mwaliko wa kuboresha maisha ya kiroho kwa kujikita katika: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Matendo adili na matakatifu na kwamba, Msalaba uwe ni kimbilio na ngao ya maisha ya mwamini. Baba Mtakatifu Leo XIV Alhamisi kuu tarehe 2 Aprili 2026 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Kubariki Mafuta na kuweka wakfu Mafuta ya Krisma ya Wokovu, “Sacrum Chrisma.” Ni mafuta yanayowaweka wakfu Wakristo, ili hatimaye, kushiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Ibada hii ya Misa Takatifu inalionesha Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Wokovu, inayotakasa. Baba Mtakatifu Leo XIV amebariki: Mafuta ya Wakatekumeni na Mafuta ya Wagonjwa pamoja kuweka wakfu Mafuta ya Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo, Sakramenti ya Kipaimara na wanapowekwa wakfu kuwa Mapadre na Maaskofu.
Kwa vile Mapadre ni waadhimishaji na wagawaji wa Mafumbo ya Kanisa, wanapaswa kujitakatifuza katika maisha yao, kwa kuambatana na Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti. Haya ni mafuta yanayotumika pia kutabaruku Kanisa kwa kupaka Altare na kuta za Kanisa kuonesha kwamba, Jengo hili, yaani Kanisa limetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya mambo matakatifu ya Mungu, yaani Mafumbo ya Kanisa. Mafuta haya ni ishara ya uwepo wa Roho Mtakatifu. Haya ni mafuta yaliyotiwa manukato na kuwekwa wakfu na Askofu mahalia, huashiria paji la Roho Mtakatifu kwa mbatizwa mpya. Amekuwa Mkristo, yaani “Mpakwa” na Roho Mtakatifu na hatimaye, ameingizwa katika Kristo Yesu, ambaye amepakwa mafuta kama: Kuhani, Nabii na Mfalme. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anachambua kuhusu umuhimu wa Mafuta Matakatifu katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba yana malengo matakatifu.
Hii ni siku ambayo Mama Kanisa amebariki pia Mafuta ya Wagonjwa: “Oleum infirmorum.” Mafuta haya hutumika katika Sakramenti ya Mpako wa wagonjwa na hutolewa kwa wagonjwa walio katika hatari kubwa, kwa kuwapaka mafuta usoni na mikononi; mafuta yaliyobarikiwa itakiwavyo, yaliyokamuliwa kutoka katika matunda ya Mizeituni kwa kusema mara moja tu: “Kwa Mpako huu Mtakatifu na kwa pendo lake kuu, Bwana akujaze kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Akuondoe katika enzi ya dhambi, akuweke huru. Kwa wema wake akupe nafuu katika mateso yako na kukujalia neema.” Ni mafuta yanayoweza kuleta: faraja, msamaha wa dhambi na uponyaji kadiri ya mapenzi ya Mungu pamoja na kumwondolea dhambi mgonjwa ambaye hawezi kuungama. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi anasema, Mafuta ya Wagonjwa yanatumika kuwafariji na kuwatia nguvu wagonjwa na wale walio dhaifu na kwamba, yanapaswa kutumika kwa imani na uadilifu mkubwa kama atakavyo Mwenyezi Mungu.
Mafuta ya Wakatekumeni: “Oleum Catechumenorum” ni ishara ya nguvu ya Kristo Yesu kwa waamini wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Ubatizo, ili waweze kupata uwezo wa kupambana na vishawishi pamoja na dhambi. Ni mafuta yanayowaandaa Wakatekumeni kupambana dhidi ya uovu na hivyo kuwakirimia waamini neema ya awali kabla ya kupokea Sakramenti ya Ubatizo. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi anakaza kusema: Mafuya ya Wakatekemeni yanatumika kuwaandaa wakatekumeni wanapoelekea kupokea Sakramenti ya Ubatizo, kumbe wakatekumeni wanapaswa kuandaliwa vyema, waelewe imani yao ya Kikristo na kuipokea imani hiyo, ili hatimaye waweze kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao kwa kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni: Kuhani, Nabii na Mfalme. Mama Kanisa anafundisha kwamba, Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha Mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya upendo, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Akataka pia kuwapatia amana ya upendo huu na kuendelea kubaki kati yao na kuendelea kuwashirikisha Fumbo la Pasaka, aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kielelezo cha sadaka, shukrani, kumbukumbu endelevu na uwepo wake kati yao katika alama ya Mkate na Divai!
Alhamisi kuu ni Siku ambayo Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu ya Upadre inayopata utimilifu wake katika Daraja ya Uaskofu; Ni Siku ambayo Kristo Yesu aliweka pia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hii ni siku ambayo Kristo Yesu aliwaweka Mitume wake, wawe wafuasi wake wa karibu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, hii ni siku ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre na kuwashukuru Mapadre kwa sadaka na majitoleo yao licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake kwa mwezi Aprili 2026 anawaalika waamini kuwakumbuka na kuwaombea Mapadre wanaopitia changamoto katika maisha na utume wao. Huu ni mwaliko kwa Mapadre kuishi mintarafu Daraja Takatifu ya Upadre, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wa Kipadre, wakitambua kwamba, kwa njia ya Daraja Takatifu ya Upadre wanashirikishwa maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mapadre wanapaswa kusimama kidete ili kuweza kuishi fadhila za maisha na utume wa Kipadre, kwa kujitahidi kuishi kama Kristo mwingine “Alter Christus” ili kwamba, waamini waweze kumtambua Kristo Yesu ndani mwao. Hii pia ni Siku ambayo Mapadre wanarudia tena ahadi pamoja na viapo vyao, jambo wanalopaswa kulifanya kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, ili kuendelea kuimarisha urika wao pamoja na Maaskofu wao mahalia.
Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi anawataka Mapadre wawe ni watu wenye tija, afya njema na wanaompendeza Mungu. Wajenge tabia, utamaduni na mazoea ya kusali pamoja, kuwajibika, kudumisha upendo, waoneshe ukomavu wa imani, maadili na ukomavu wa wakfu sanjari na kufanya yote yanayompendeza Mungu. Wajitahidi kukamilishana, kusaidiana, wakue na kukomaa katika wito, wakfu na utume wao kama Mapadre. Waone fahari kushirikiana na waone aibu wanapoishi kama mchana na usiku. Wajitahidi kuwa ni Mapadre na Makuhani wa Mungu kwa kupendana, kutakatifuzana na kuleana. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake, Alhamisi kuu 2026 amejikita kutafakari kuhusu utume ambao kila Padre amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, wao ni wahudumu wa watu ambao ni wamisionari, waliobatizwa katika Roho Mtakatifu na hivyo kufanywa kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa na kwamba wamepakwa mafuta na Roho wa uhuru, faraja, Unabii na Umoja. Huu ni utume unaosimikwa katika upatanisho unaowataka “kujinyandua” kutoka katika malimwengu bila woga, tayari kukutana na Kristo Yesu anayewakarimu, kwa kusoma alama za nyakati; utamaduni mpya unaoundwa na mabadiliko haya inakuwa ni fursa mpya ya uinjilishaji, ili hatimaye kuliwezesha Kanisa kufikisha Neno la Mungu kwenye kiini cha maisha ya watu, ushuhuda wa Fumbo la Mwili wa Kristo unaoundwa na watu wengi na Askofu Oscar Arnulfo Romero ni shuhuda wa upendo na mshikamano wake na Kristo Yesu hadi dakika ya mwisho ya maisha yake kwa ajili ya Kanisa na uzalendo wa nchi yake. Huu ni utume unaofumbatwa katika umoja na ambao kimsingi ni chimbuko la amani, tayari kutangaza: mateso, kifo na ufufuko, huku wakingojea ujio wa Kristo Yesu!
