Wagonjwa wa hospitali ya Watoto ya Vatican wachora mchoro kwa ajili ya Papa Leo XIV
Salvatore Cernuzio na Claudia Torres katika ndege na Sr.Christine Masivo,CPS
Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV kwa mataifa manne ya Afrika ilianza kwa rangi nyingi ndani ya ndege ya Papa Jumatatu, tarehe 13 Aprili 2026. Wakati wa salamu za kawaida, waandishi wa habari kutoka Baraza la Kipapa la Mawasiliano walimkabidhi Baba Mtakatifu mchoro uliochorwa na watoto wanaopata huduma katika hospitali ya Watoto ya Bambino Gesù jijini Roma. Inamwonesha Papa Leo XIV akiwa amevaa miwani na kubeba mkoba wenye neno “Injili”, karibu kuanza safari na watoto.
Waandishi wa habari wa Vatican kuelezea ujumbe wa amani
Watoto wanaonekana wakiweka matofali ya ujenzi, kama wajenzi wa amani. Ni ujumbe wenye kugusa moyo ambao watoto walio lazwa hospitalini walitaka kuonyesha msaada wao kwa Baba Mtakatifu alipoanza safari yake kwenda Algeria, Cameroon, Angola, na Guinea ya Ikweta. Waandishi wa habari wa Vatican walielezea ishara ya ujumbe wa amani wa mchoro huo, wakati ambapo migogoro katika sehemu mbalimbali za dunia inaendelea kuhatarisha watoto.
Kazi kubwa ya Hospitali ya Papa
Kwa kujibu, Papa Leo XIV alitabasamu na kusema, "Asante sana." Kazi kubwa ya Hospitali ya Bambino Gesù katika nyakati hizi za vita inajulikana sana: tangu Urusi ilipoishambulia Ukraine kwa bomu kwa mara ya kwanza, imewakaribisha zaidi ya wagonjwa 2,000 wa Ukraine katika wodi zake. Katika miaka ya hivi karibuni, wagonjwa wengine 30 kutoka Ukanda wa Gaza wamelazwa katika idara zake mbalimbali, baadhi yao wakihitaji huduma ngumu sana ya matibabu. Picha hiyo ilichorwa katika chumba cha kuchezea cha hospitali hiyo, njia panda ya kukutana ambako watoto na watu wazima hukusanyika kila siku, vijana wanaopata matibabu, na wazazi wanaoandamana na watoto wao. Wakristo wa madhehebu tofauti, Waislamu, na watu wa dini zingine pia hukusanyika hapo.
Wajenzi wa amani
Katika chumba cha kuchezea,watoto pamoja na kaka na dada za wagonjwa, wanaweza kucheza, kupiga gumzo, na kupumzika, kutokana na msaada wa waelimishaji wataalamu wanaowashirikisha wale walio chini ya uangalizi wao katika miradi na shughuli zinazozingatia mada ya amani. Wazo ni kwamba katika enzi iliyojaa chuki na vurugu, kama Papa Leo alivyosema mara kwa mara, ni muhimu kukuza katika vizazi vipya hamu ya kuwa “wajenzi wa amani.” “Sisi, wajenzi wa amani, tuko pamoja nawe, Papa Leo!” waliandika watoto kwenye mchoro wa Papa. Pia waliambatanisha michoro na jumbe zingine, kama vile moja iliyoelekezwa kwa watoto na watu wazima, wakiwahimiza “wasibishane.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.
