Ask.Kilaini:‘Magnifica Humanitas’inatulinda dhidi ya'akili'isiyo ya kiutu na hisia zake
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Bado tunaendelea na kutazama kwa kina kuhusu Waraka wa Kwanza wa Baba Mtakatifu Leo XIV uliochapishwa tarehe 25 Mei 2026. Maoni mengi kutoka viongozi wa kikatoliki na wasio wa kikatoliki na hata viongozi wa taasisi za umma yanavuma katika mitandao ya kijamii. Ni katika muktadha ambavyo vyombo vya Radio Vatican-Vatican News, vinaendelea na chimba chimba hizo kuhusu Waraka huu ulivyogusa. Kwa upande wa Askofu Method Kilaini, Askofu Msaidizi Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba nchini Tanzania, akihojiana na Vatican News awali ya yote alianza “kutoa shukrani kwa Baba Mtakatifu kwa waraka wake wa Magnifica Humanita. Kwake yeye kwamba, “Mbali na shughuli zangu za kichungaji, mimi ni mwanahistoria (Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, 1990), na ninafundisha Historia ya Kanisa, darasani na kwenye radio na TV. Mmoja wa mapapa ninaowapenda ni Papa Leo XIII kwa sababu, katika historia, alipingana na mwelekeo wa wakati huo na kuongoza Kanisa katika kushughulikia masuala ambayo yalikuwa muhimu kwa watu wa wakati wake, yaani Mapinduzi ya Viwanda. Papa wetu alipochukua jina hilo, nilifurahi, na sasa anachukua njia hiyo hiyo katika waraka wake wa kwanza.”
![]()
Askofu Kilaini,Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba,Tanzania
Mapapa wamekuwa wakishughulikia kwa ujasiri masuala halisi ya sasa
Askofu Kilaini aliendelea kusema kuwa, “Nimesoma waraka wa ‘Magnifica Humanitas,’ mara kadhaa. Masuala yaliyoshughulikiwa yanafaa hasa sasa kwa wakati wetu. Wakati akisherehekea miaka 135 ya Waraka wa Rerum Novarum wa Papa Leo XIII, anarudia kanuni zile zile kwamba "Ingawa mambo mengi ya kihistoria yaliyoelezwa na Papa Leo XIII yamebadilika, angalau mitazamo miwili inabaki kuwa muhimu sana leo: ubora wa kazi ya binadamu kuliko mawazo yoyote yanayozingatia fedha au kutengeneza bidhaa pekee; - kuzingatia watu na familia ambazo zinaweza kuathiriwa zaidi na unyonyaji - na uhusiano usioweza kutenganishwa kati ya kutangaza Injili na kujali utaratibu wa kijamii wenye kuleta haki. Kwa hivyo Rerum Novarum inaendelea kutukumbusha kwamba hakuna uinjilishaji halisi ambao haujishugulishi pia na maisha ya jamii ya wanadamu." (MH na 30). Kwa maneno mengine, Maendeleo ni kwa ajili ya mwanadamu na si mwanadamu kwa ajili ya maendeleo. Katika waraka wake anatukumbusha mafundisho haya katika nyaraka za kipapa kuanzia Rerum Novarum ya Papa Leo XIII hadi Fratelli Tutti (Wote ni Ndugu) ya Papa Francisko. Sio mwendelezo tu, lakini mbali na kutafakari uthibitisho wa zamani, anashughulikia kwa ujasiri masuala halisi ya sasa ikiwemo Akili Unde (AI), uhamiaji, kazi na utumwa mamboleo.”
![]()
Papa Leo XIV wakati wa Uwasilishaji wa Waraka wa Kitume wa Magnifica Umanitas (@Vatican Media)
Inaleta faraja na haueni kuona Baba Mtakatifu anakiri makosa yaliyofanywa na Kanisa
Askofu Kilaini anasimulia vile vile kwamba “katika kufundisha Historia ya Kanisa, nikiwa Mwafrika, mimi huona aibu kila wakati ninapofundisha juu ya biashara ya watumwa, kwani Kanisa wakati huo katika ngazi zote halikupinga utumwa na biashara ya watumwa. Inaleta faraja na haueni kwamba Baba Mtakatifu amekiri dhuluma hii na upofu wa Kanisa kwa hilo. Akiandika juu ya historia ya utumwa anakiri kwamba: "Hili ni jeraha katika kumbukumbu ya Kikristo, ambalo hatuwezi tujitenga nalo. Haiwezekani kutohisi huzuni kubwa tunapotafakari mateso na fedheha kubwa waliyopitia watu wengi tofauti kabisa na hadhi yao isiyopimika kama watu wanaopendwa na Bwana milele.”Kwa hili, kwa jina la Kanisa, naomba msamaha kwa dhati." (MH 176)” alisisitiza Askofu.
![]()
Waraka wa Kitume wa Papa Leo XIV wa magnifica Humanitas (@Vatican Media)
Hii inanikumbusha mafundisho ya Papa Leo XIII, akisema kwamba Kanisa ni la Kimungu na la kibinadamu katika barua yake kwa Maaskofu na Mapadre wa Ufaransa mwaka 1899. "Mwanahistoria wa Kanisa ataweza kudhihirisha asili ya kimungu ya kanisa, jinsi liilivyo bora kuliko dhana zote na mpangilio wa kidunia, hata hivyo kwa uaminifu asifiche au kuondoa majaribu ambayo makosa ya watoto wake, na wakati mwingine hata ya makuhani wake, yamemletea Mwenzi wa Kristo (Kanisa) katika kipindi cha karne nyingi. Ikisomwa kwa njia hii, historia ya Kanisa yenyewe inaunda uthibitisho mzuri na wa mwisho wa ukweli na Umungu wa Ukristo.” Papa Leo XIV amekuwa na ujasiri wa "kuomba msamaha kwa dhati" kwa makosa yaliyofanyika.
Papa Leo XIV anafuata nyao za watangulizi wake
Katika waraka huu, Baba Mtakatifu anazungumzia suala la Akili unde (AI). Hapa anafuata nyayo za watangulizi wake anapokabiliwa na uvamizi ambao una upanga wenye makali kuwili wa kufanya mema lakini pia kuharibu. Kwa maendeleo ya filamu, radio na televisheni, Papa Pius XII alitoa Waraka wa 'Miranda Prorsus’ yaani (maajabu ya ubunifu) wa tarehe 8 Septemba 1957; Papa Mtakatifu Yohane Paulo II alizungumzia kuhusu mitandao mwaka 2002, na Papa Francisko akizungumzia kuhusu mawasiliano, akitaja Akili Unde(AI). Askofu Mstaafu wa Jimbo la Bukoba, hakuishia hapo bali anasisitiza kwamba “Binafsi, ninafurahi kwamba Baba Mtakatifu amezungumzia kuhusu uvumbuzi huu wenye utata kabla hatujachelewa.
![]()
Waraka wa Kitume wa Papa Leo XIV (@Vatican Media)
Masuala aliyogusia ya AI si kwamba tuyaepuke bali kuwa waangalifu na uwajibikaji
Masuala aliyogusia Baba Mtakatifu Leo XIV ni halisi, si kwamba tunapaswa kuepuka Akili Unde, lakini tunapaswa kuwa waangalifu na kusaidia kuifanya itoe matokeo chanya na sio uharibifu wa mwanadamu. Anaeleza kwa ufupi, akisema: "Teknolojia ina nguvu ya kuponya, kuunganisha, kuelimisha na kulinda nyumba yetu ya pamoja; lakini pia inaweza kugawanya, kutenga na kuzalisha aina mpya za dhuluma. Kwa ufupi, teknolojia yenyewe si suluhisho la matatizo ya wanadamu, na wala si mbaya kiasili. Hata hivyo, katika utendaji, teknolojia haiegemei upande wowote, kwa sababu inachukua sifa za wale wanaiobuni, kufadhili, kudhibiti na kutumia."(MH9) Akili Unde inaweza kutumika kuwafanya watu watumwa au kuwaweka huru, inaweza kutumika kuelimisha watu au kubuni silaha za vita zinazoharibu na kutokomeza binadamu. Inaweza kuongeza ukweli na mahusiano mazuri au kukuza uongo, kwa sababu ina "Uwezo wa kudhibiti maudhui, picha na video za kuwaonyesha watu kwa mitazamo yenye upendeleo au inayopotosha." (MH 132).
![]()
Askofu Kilaini
Tunajifunza katika hali zote,mwanadamu na ubinadamu ndio wa kwanza
Kwa njia hiyo, Mwanahistoria wa Kanisa huyo anasisitiza kuwa, “Ninaamini kwamba tunajifunza kwamba katika hali zote, mwanadamu na ubinadamu ndio wa kwanza. Katika wakati wa (AI), mwanadamu anapaswa kudumisha utu wake, ukweli, uhuru na asidanganywe kwa njia bandia. Tunapaswa kujenga ustaarabu uliojengwa juu ya upendo, haki, udugu, na mazungumzo. Hatupaswi kujenga mnara wa Babeli kulingana na uchoyo, mgawanyiko na ubinafsi, bali kujenga Mji Mtakatifu wa Yerusalemu kulingana na mshikamano na heshima ya pande zote.”
Tujiunge na Baba Mtakatifu kufuata nyayo za Bikira Maria kwa wimbo wa Magnificat
Kwa kuhitimisha, Askofu Kilaini alibanisha kwamba “Kwa Afrika na kwingineko, Magnifika Humanitas ni zawadi kubwa, kwani inatulinda kutokana na utumwa mpya na utawala wa watu wachache ambao huenda wasiwe na dhamiri njema. Wanataka ulimwengu udhibitiwe si na mwanadamu kwa furaha na huzuni zake, upendo na maumivu, imani na uvumilivu, bali kwa 'akili' isiyo ya kiutu na hisia zake. Sote na tujiunge na Baba Mtakatifu katika kufuata nyayo za Bikira Maria wa wimbo wake wa Magnificat na hivyo kumsifu na kuishi, tukiweka kila kitu mikononi mwa Bwana.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.
