Tafuta

Nyumba ya Kupunguza Mateso: “La Casa Sollievo della Sofferenza" inasimama kama ushuhuda wa kina wa Injili ya huruma na upendo kutoka kwa Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, O.F.M. Cap. (1887–1968) Nyumba ya Kupunguza Mateso: “La Casa Sollievo della Sofferenza" inasimama kama ushuhuda wa kina wa Injili ya huruma na upendo kutoka kwa Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, O.F.M. Cap. (1887–1968)  

Hospitali ya Mtakatifu Padre Pio: Huduma ya Huruma na Upendo Kwa Wagonjwa

Hospitali hii ni kielelezo cha msingi wa huduma ya upendo na udugu wa kibinadamu kwa wagonjwa na watu wenye udhaifu; huduma inayotolewa na wafanyakazi katika sekta ya afya kwa sadaka na majitoleo makubwa. Magonjwa na mateso ni mambo yanayopelekea watu kuvunjika na kupondeka moyo, lakini upendo una nguvu ya kuwainua tena wale wote waliovunjika na kupondeka moyo, kwa njia ya huduma makini kwa wagonjwa. Miaka 70 ya Huduma makini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utakatifu na mateso ni sehemu ya fumbo la maisha ya mwanadamu linaloweza kueleweka tu kwa njia ya Ufunuo. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanahudumia Injili ya uhai katika hatua zake zote hadi pale mauti ya kawaida inapomfika mtu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kanuni maadili na utu wema ni mwongozo makini kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, ili kulinda maisha ya binadamu na kutomdhulu mtu. Hapa watu wanapaswa kuongozwa na kanuni ya dhahabu inayoratibu uhusiano na watu wengine kwamba, “Basi yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo: maana hiyo ndiyo torati na manabii.” Mt. 7:12. Hii ni kanuni muhimu sana katika huduma ya afya inayopaswa kuboreshwa kwa kujenga na kudumisha uhusiano na mafungamano kati ya: mgonjwa, wafanyakazi katika sekta ya afya, ndugu na jamaa ya mgonjwa, wanajumuiya ambao wana uhusiano wa karibu na mgonjwa. Sanaa ya matibabu, mchakato wa huduma pamoja na matibabu endelevu ni mambo msingi katika huduma ya afya na hasa zaidi kwa wagonjwa mahututi na wale ambao wako kufani. Kristo Yesu anawaalika wafuasi wake kuwa ni Wasamaria wema kwa kuwekeza katika huduma ya tiba, ili kuokoa maisha ya watu, kielelezo cha upendo wa Mungu, ambaye kimsingi ni chanzo, maana na hatima ya maisha ya binadamu. Wajibu wa kimaadili, ukiongozwa na imani, uwasaidie watu kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, chanzo cha uhai. Kifo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na wanasayansi wanapaswa kutambua ukweli huu. Daima mgonjwa apewe tiba hata wale wenye magonjwa sugu na ya muda mrefu. Hii ni huduma ya tiba: kimwili, kisaikoljia, kijamii, kifamilia na katika maisha ya kiroho, kwa kuzingatia taalimungu ya maisha ya mwanadamu. Wadau mbalimbali wamsaidie mgonjwa kujiandaa kufa kifo chema, akiwa anasindikizwa na neema ya utakaso na upendo wa Mungu. Pale ambapo imani na matumaini vinakosekana wakati mgonjwa anapokaribia kifo kuna hatari ya kutumbukia katika kifolaini au msaada wa kutaka kujinyonga.

Kristo Yesu anawaalika wafuasi wake kuwa ni Wasamaria wema
Kristo Yesu anawaalika wafuasi wake kuwa ni Wasamaria wema   (ANSA)

Nyumba ya Kupunguza Mateso: “La Casa Sollievo della Sofferenza,” “House for the relief of Suffering” inasimama kama ushuhuda wa kina wa Injili ya huruma na upendo kutoka kwa Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, O.F.M. Cap. (1887–1968) aliyejulikana sana kwa maisha yake ya sala, unyenyekevu, huruma na upendo kwa maskini na wagonjwa, na karama za maisha ya kiroho ikiwa ni pamoja na kubahatika kupata Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu mwilini mwake. Hospitali hii ilifunguliwa tarehe 5 Mei 1956 na Mwaka 2026 inaadhimisha kumbukizi ya Miaka 70, tangu kuanzishwa wake tukio ambalo limeadhimishwa tarehe 5 Mei 2026 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV, tarehe 27 Mei 2026 ameunda Tume ya Uendeshaji na Usimamizi wa Mfuko wa "Casa Sollievo della Sofferenza - Opera di San Pio da Pietrelcina, O.F.M. Cap." Yaani “Mfuko wa Nyumba ya Kupunguza Mateso, Kazi ya Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, O.F.M. Cap.” Kama sehemu muhimu sana ya mwendelezo wa maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa kuganga na kuponya magonjwa na udhaifu, dhamana na utume ambao Mama Kanisa amekabidhiwa kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe: “Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.” Mt 10:1.

Mama Kanisa amekuwa mstari wa mbele kutoa huduma kwa wagonjwa
Mama Kanisa amekuwa mstari wa mbele kutoa huduma kwa wagonjwa   (ANSA)

Mama Kanisa katika maisha na Mapokeo yake, amekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma kwa wagonjwa na watu dhaifu, kama kielelezo cha ushuhuda wa huduma ya upendo, kama inavyojionesha katika Nyumba ya Kupunguza Mateso: “La Casa Sollievo della Sofferenza,” “House for the relief of Suffering” iliyoanzishwa na Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, O.F.M. Cap. Hiki ni kielelezo cha ukarimu, msaada na huduma kwa wagonjwa, mahujaji na familia zao, huku wakiongozwa na maisha ya kiroho ya Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, O.F.M. Cap. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika Ulimwengu mamboleo kuna mageuzi makubwa ya nyakati, sayansi na teknolojia; sheria na uchumi na kwamba, hizi ni changamoto za maisha na utume wa Kanisa katika sekta ya huduma ya afya kwa wagonjwa. Mabadiliko haya yanahitaji uwekezaji mkubwa na usimamizi wa busara wa rasilimali vifaa tiba na fedha kutoka kwa waamini, taasisi za umma na zile za binafsi ambazo kimsingi zinashiriki kikamilifu Utume na Mafundisho ya Kanisa kuhusu huduma kwa wagonjwa. Tume hii itakuwa na dhamana na wajibu wa kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka katika sekta ya afya. Itakuwa na jukumu la kuchanganua hali ya sasa ya Mfuko huu; kwa kubainisha suluisho bora zaidi, kwa kuongeza ufanisi wa utume na kazi zake, ili kutoa suluhu ya matatizo na changamoto hizi.

Kumbukizi ya Miaka 70 ya Hospitali ya Mt. Padre Pio
Kumbukizi ya Miaka 70 ya Hospitali ya Mt. Padre Pio

Kwa upande wake Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahubiri yake kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Nyumba ya Kupunguza Mateso: “La Casa Sollievo della Sofferenza,” “House for the relief of Suffering” amesema, hospitali hii ni kielelezo cha msingi wa huduma ya upendo na udugu wa kibinadamu kwa wagonjwa na watu wenye udhaifu; huduma inayotolewa na wafanyakazi katika sekta ya afya kwa sadaka na majitoleo makubwa. Magonjwa na mateso ni mambo yanayopelekea watu kuvunjika na kupondeka moyo, lakini upendo una nguvu ya kuwainua tena wale wote waliovunjika na kupondeka moyo, kwa njia ya huduma makini kwa wagonjwa. Hii ni Hospitali yenye kiwango cha hali ya juu sana cha ubora katika huduma kwa wagonjwa na tafiti za kisayansi. Kardinali Pietro Parolin amewataka madaktari na wahudumu katika Hospitali hii kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu; kwa amani na utulivu wa ndani na kwamba, waendelee kujikita katika uaminifu kwa kuandika historia ya huduma ya upendo katika sekta ya afya, inayopata chimbuko lake katika tunu msingi za Kiinjili; maisha na utume wa Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, O.F.M. Cap. Hospitali hii, bado inayo fursa ya kuendelea kuandika kurasa nyingi za unabii.

Hospitali ya Mt. Padre Pio ni chemchemi ya huruma na upendo katika huduma
Hospitali ya Mt. Padre Pio ni chemchemi ya huruma na upendo katika huduma   (Michele Martino)

Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatano tarehe 13 Mei 2026 alipata nafasi ya kuzungumza, kuwapatia zawadi ya Rozari Takatifu pamoja na kupiga picha ya ukumbusho na mahujaji 49 kutoka Tanzania: Kati yao kulikuwa kuna Mapadre 3, Wanandoa 3 na wengine wote waliosalia ni Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women of Tanzania Association) ambacho ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika.” Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Mahujaji hawa walipata nafasi ya kutembelea San Giovanni Rotondo,  sehemu muhimu ya Madhabahu ya Padre Pio. Mama Evaline Malisa Ntenga, Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania ana simulia kwa ufupi historia ya maisha ya Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, O.F.M. Cap.

Huduma ya Upendo kwa wagonjwa
28 Mei 2026, 13:35