Hotuba ya Papa Leo XIV Kwa Mabalozi Wapya Mjini Vatican 2026
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Diplomasia ya Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, inatoa kipaumbele cha pekee kwa uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Vatican katika medani mbalimbali za Kimataifa. Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu. Hizi ni haki za wote zisizoweza kukiukwa wala kutenguliwa. Ni za binadamu wote bila kujali: wakati, mahali au mhusika. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Haki ya kwanza kabisa ni uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale anapofariki dunia kadiri ya mpango wa Mungu. Mkazo umewekwa katika haki ya uhuru wa kidini inayofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu. Hiki ni kiini cha haki msingi kinachofumbata haki nyingine zote. Kuheshimu na kuthamini haki hii ni alama ya maendeleo halisi ya binadamu katika medani mbalimbali za maisha. Haki inakwenda sanjari na wajibu! Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kuheshimu haki msingi za binadamu, kichocheo muhimu sana cha amani na utulivu miongoni mwa binadamu. Kanisa linapenda kusimama kidete: kulinda na kudumisha haki na amani sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mwanga na chachu ya tunu msingi za Kiinjili!
Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948. Takwimu zinaonesha kwamba, Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184 duniani. Mabalozi wakazi wanaoishi mjini Roma kwa sasa ni 89, wengine, ni mabalozi wanaowakilisha nchi zao wakiwa wanatoka nje ya Roma. Kuna Mashirika ya Kimataifa kama vile, Shirikisho la Nchi za Kiarabu pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR. Ni katika kukuza na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi mbalimbali duniani, Baba Mtakatifu Leo XIV Alhamisi tarehe 21 Mei 2026 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wa nchi nane ambao ni: Balozi Loai Yahya AL-ERYANI kutoka Yemen, Balozi Philip Bob JUSU kutoka Sierra Leone, Balozi Jerobeam SHAANIKA kutoka Namibia; Balozi Amina Priscille LONGOH kutoka Chad; Balozi Dassanayake Mudiyanselage Sumith Priyantha kutoka Sri Lanka; Balozi Urujeni BAKURAMUTSA kutoka nchini Rwanda; Balozi. Rajeshwar JEETAH kutoka Mauritius pamoja na Balozi Nahida SOBHAN kutoka Bangaladesh. Baba Mtakatifu amewasihi Mabalozi hawa wapya mjini Vatican kumfikishia salam zake za dhati kwa Marais wa nchi zao.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amegusia kuhusu Sherehe ya Pentekoste chemchemi ya umoja; diplomasia inayokuza majadiliano na kutafuta maridhiano yanayosimikwa katika wongofu wa ndani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kupyaisha huduma ya wanadiplomasia na kuimarisha mashirika ya kimataifa, ili kuunda fursa za kukutana na upatanisho. Baba Mtakatifu anasema, katika wakati ambapo "amani hutafutwa kupitia silaha kama sharti la kuthibitisha utawala wa mtu mwenyewe," kuna haja ya haraka ya kurudi kwenye "diplomasia ambayo inakuza majadiliano na kutafuta maridhiano" katika ngazi zote: baina ya nchi mbili, kikanda, na Kimataifa. Majadiliano kama hayo, yachochewe na unyoofu wa kutafuta njia zinazoongoza kwenye amani; katika misingi ya ukweli na uwazi, bila upotoshaji au ujenzi wa uadui, ili kuondokana na hali ya kutoelewana na hivyo uaminifu kujengwa upya katika muktadha wa mahusiano ya Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, majadiliano haya hayana budi kujikita katika ukweli, uwazi na wongofu wa ndani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujikita katika haki na utu na kwamba, haiwezekani kupima mafanikio kwa kujikita katika nguvu au ustawi na kuwapuuza maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hakika, upendo wa Kristo Yesu kwa walio wadogo na waliosahaulika unawalazimisha waamini kukataa kila aina ya uchoyo na ubinafsi unaowaacha maskini na walio hatarini wasionekane (taz. Apostolic Exhortation Dilexi Te, 4 October 2025, 9).
Baba Mtakatifu anawasihi Mabalozi wapya kujenga na kudumisha mshikamano na sadaka binafsi ili kupyaisha huduma ya wanadiplomasia na hatimaye, kuimarisha mashirika ya Kimataifa, ili kuunda fursa za watu kukutana na upatanisho. Taasisi hizi zinasalia kuwa vyombo vya lazima vya kusuluhisha migogoro na hivyo kukuza ushirikiano. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema wakati ambapo mivutano ya kijiografia na kisiasa inaendelea kuwagawa walimwengu ni muhimu huduma ya kidiplomasia kuifanya iwe ni ya uwakilishi zaidi, yenye ufanisi na yenye mwelekeo wa ujenzi wa umoja wa familia ya binadamu. Huduma yao kama Mabalozi inajenga daraja la thamani, uaminifu na ushirikiano kati ya nchi zao na Vatican. Kumbe, juhudi za pamoja zinaweza kuchangia katika mchakato wa ujenzi mpya wa ushirikiano wa Kimataifa kwa kuwavuta wale ambao husahauliwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii na kwa njia hii, wanaweza kuweka misingi thabiti zaidi ya ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika haki, udugu wa kinabadamu na amani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, watapata ushirikiano mkubwa kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na Mabaraza mbalimbali ya Kipapa. Amewataka Mabalozi wapya kuhakikisha kwamba, wanaimarisha majadiliano, maelewano sanjari na kuchangia amani inayohitajika sana kwa wakati huu na mwishoni amewapatia baraka zake za kitume.
