Tafuta

Mama Kanisa anaadhimisha Juma la “Laudato si” litakalofikia kilele chake Dominika tarehe 24 Mei 2026, Sherehe ya Pentekoste. Mama Kanisa anaadhimisha Juma la “Laudato si” litakalofikia kilele chake Dominika tarehe 24 Mei 2026, Sherehe ya Pentekoste. 

Maadhimisho ya Juma la Laudato si Kuanzia Tarehe 17 - 24 Mei 2026

Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 17 Mei 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewaambia waamini kwamba, Mama Kanisa anaadhimisha Juma la “Laudato si” na kilele chake ni Dominika tarehe 24 Mei 2026. Maadhimisho haya yanayofanyika sehemu mbalimbali za dunia, yakilenga kukuza na kudumisha utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, na yanaragibishwa na Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki kwani uharibifu wa mazingira ni kati ya vyanzo vikuu vya umaskini, ujinga, magonjwa, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, jamii inayotunza na kuheshimu mazingira, hiyo inaweza kudumisha furaha, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Uharibu wa mazingira unahitaji toba na wongofu wa kiikolojia, ili kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya mwanadamu kwa kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Ikumbukwe kwamba, hii pia ni dhamana ya kijamii inayopania kuupatia umaskini kisogo pamoja na kuhakikisha kwamba rasilimali ya dunia inatumika vyema zaidi kwa ajili ya: Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo, mafao ya wengi sanjari na wongofu wa kiikolojia, kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu.

Juma la Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote
Juma la Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote   (@Vatican Media)

Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” uliozinduliwa hapo tarehe 18 Juni 2015 mjini Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, Dominika tarehe 17 Mei 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewaambia waamini na mahujaji kwamba, Mama Kanisa anaadhimisha Juma la “Laudato si” litakalofikia kilele chake Dominika tarehe 24 Mei 2026, Sherehe ya Pentekoste. Maadhimisho haya yanayofanyika sehemu mbalimbali za dunia, yakilenga kukuza na kudumisha utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, yanaragibishwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu.

Maadhimisho ya Juma la Laudato si kwa Mwaka 2026
Maadhimisho ya Juma la Laudato si kwa Mwaka 2026   (@Vatican Media)

Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi, mtu wa amani na majadiliano, aliyejitahidi kuishi ukweli katika hali ya unyenyekevu; kwa hakika maisha yake yanang'aa kwa mwanga angavu, kwa kuwa yalitiwa msukumo na ujasiri wa kuishi katika ukweli, na ufahamu kwamba ulimwengu wa amani unajengwa kuanzia na mioyo ya unyenyekevu iliyoelekezwa kuelekea mji wa mbinguni.  Moyo mnyenyekevu na wa kupenda amani ndio ambao Baba Mtakatifu Leo XIV anatamani kuuona kwa kila mmoja wao na kwa watu wote wa Mungu. Anasema, wakati huu wa kufanya kumbukizi ya ujumbe wake wa amani na Mwenyezi Mungu, majirani pamoja na kazi yote ya uumbaji. Inasikitisha kuona kwamba, katika miaka ya hivi karibuni kutokana na vita, kinzani na migogoro sehemu mbalimbali za dunia, maendeleo mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote yamedumaa. Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii kuwatia shime wanaharakati wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na wale wote wanaoendelea kujisadaka katika ikolojia ya maendeleo endelevu ya binadamu kupyaisha tena dhamana na utume wao kwa sababu utunzaji wa amani ni utunzaji wa zawadi ya maisha!

Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya wote ni wajibu wa kimaadili
Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya wote ni wajibu wa kimaadili   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume wa “Laudato si”, anapembua kwa kina na mapana kuhusu: Mambo yanayotokea katika mazingira; Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Uumbaji. Anabainisha vyanzo vya mgogoro wa ikolojia vinavyohusiana na watu, baadaye anazama zaidi kufafanua maana ya ikolojia katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Anatoa ushauri kuhusu njia za kupanga na kutekeleza na mwishoni anajiekeza zaidi katika elimu ya ikolojia na maisha ya kikristo!

Juma la Laudato si
19 Mei 2026, 14:40