Tafuta

Papa Le XIV:Bikira Maria ni mshiriki bora wa Jumuiya ya Kanisa!

Baba Mtakatifu Leo XIV aliongoza Katekesi yake Mei 13 katika Sikukuu ya Bikira Maria wa Fatima kujikita kufafanua Katiba ya Lumen Gentium kuwa inasema:"Bikira Mtakatifu,aliyechaguliwa tangu milele,ndani ya mpango wa kufanyika mwili kwa Neno,kuwa Mama wa Mungu,alishirikiana kwa njia ya pekee kabisa katika kazi ya Mwokozi ya kurejesha uhai usio wa kawaida kwa roho,kupitia utii,imani,tumaini na upendo wa dhati.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV akiongoza Katekesi yake katika kumbukizi ya siku ya siku kuu ya Mama Yetu wa Fatima, iadhimishwayo kila ifikapo tarehe Mei 13, ya Kila mwaka, kwa waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, amendelea na  mwendelezo wa Katekesi zake kuhusu: Mtaguso wa Pili wa Vatican na kwamba  ulitaka kuweka sura ya mwisho ya Katiba ya Kidogma kuhusu Kanisa kwa Bikira Maria(LG 52-69).” Yeye "anatambulika kama mshiriki mkuu na wa kipekee wa Kanisa, mfano na kielelezo bora zaidi kwake katika imani na upendo" (LG 53).

Katekesi ya Papa Leo XIV
Katekesi ya Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV alisema kwamba “Maneno haya yanatualika kuelewa jinsi katika Maria, ambaye chini ya tendo la Roho Mtakatifu alimkaribisha na kumzaa Mwana wa Mungu aliyekuja katika mwili, tunaweza kutambua kielelezo, mshiriki bora, na mama wa jumuiya nzima ya Kanisa. Akijiruhusu kuumbwa na kazi ya Neema, kutimizwa ndani yake, na kukaribisha zawadi ya Aliye Juu Zaidi kwa imani yake na upendo wake wa kibikira, Maria ndiye kielelezo kamili cha kile ambacho Kanisa lote linaitwa kuwa: kiumbe wa Neno la Bwana na mama wa watoto wa Mungu aliyezaliwa kwa upole kwa tendo la Roho Mtakatifu.”

Maria ni mshiriki bora wa jumuiya ya Kanisa

Papa aliendelea kudadavua kwamba zaidi ya hayo, akiwa mwamini bora kabisa, akitupatia umbo kamili la uwazi usio na masharti kwa fumbo la kimungu katika ushirika wa watu watakatifu wa Mungu, Maria ni mshiriki bora wa jumuiya ya Kanisa. Hatimaye, anapozaa watoto katika Mwana, mpendwa katika Mpendwa wa milele aliyekuja kati yetu, Maria ni mama wa Kanisa lote, ambalo linaweza kumgeukia kwa uaminifu wa kifamilia, kwa uhakika wa kusikilizwa, kulindwa, na kupendwa. Sifa hizi za Bikira Maria zinaweza kuoneshwa kwa kumzungumzia kama ishara ya mwanamke wa Fumbo.

Maria ndiye Picha ya  mwanamke wa Fumbo

Neno "mwanamke" linaakisi uthabiti wa kihistoria wa binti huyu kijana wa Israeli, ambaye alipewa uzoefu wa ajabu wa kuwa mama wa Masiha. Usemi "ikoni" au picha unasisitiza kwamba ndani yake harakati mbili za kushuka na kupanda zinatimizwa: ndani yake huangaza uchaguzi huru wa Mungu na ridhaa huru ya imani katika Yeye. Kwa hivyo Maria ndiye Picha ya  mwanamke wa Fumbo, yaani, ya mpango wa kimungu wa wokovu, ambao hapo awali ulikuwa umefichwa na kufunuliwa kikamilifu katika Yesu Kristo.

Mtaguso ulituachia fundisho wazi juu ya nafasi ya pekee iliyohifadhiwa kwa Bikira Maria katika kazi ya Ukombozi (LG, 60-62). Ulikumbusha kwamba Mpatanishi pekee wa wokovu ni Yesu Kristo (taz. 1 Tim 2:5-6) na kwamba Mama yake Mtakatifu Sana "hafifishi au kupunguza upatanisho huu wa kipekee wa Kristo, bali anaonesha nguvu yake" (LG, 60). Wakati huo huo, "Bikira Mtakatifu, aliyechaguliwa tangu milele, ndani ya mpango wa kufanyika mwili kwa Neno, kuwa Mama wa Mungu, […] alishirikiana kwa njia ya pekee kabisa katika kazi ya Mwokozi ya kurejesha uhai usio wa kawaida kwa roho, kupitia utii, imani, tumaini, na upendo wa dhati. Kwa sababu hiyo akawa mama yetu kwa utaratibu wa neema" (ibid., 61).

Waamini na mahujaji katika Katekesi
Waamini na mahujaji katika Katekesi   (@Vatican Media)

Kwa mama,Kanisa linatafakari fumbo lake

Fumbo la Kanisa pia linaoneshwa katika Bikira Maria: ndani yake, Watu wa Mungu hupata asili yao, mfano wao, na nchi yao ikiwakilishwa. Katika Mama wa Bwana, Kanisa linatafakari fumbo lake, si tu kwa sababu linapata ndani yake mfano wa imani ya bikira, upendo wa mama, na agano la mwenzi ambalo ameitwa, lakini pia na zaidi ya yote kwa sababu linatambua ndani yake mfano wake, mfano bora wa kile anachoitwa kuwa. Kama inavyoonekana, tafakari kuhusu Mama Bikira zilizokusanywa katika Lumen Gentium zinatufundisha kupenda Kanisa na kutumikia ndani yake utimilifu wa Ufalme wa Mungu unaokuja na utakaotimizwa kikamilifu katika utukufu.

Basi Baba Mtakatifu Leo XIV aliomba kwamba “ tujiruhusu kuchangamotishwa  na mfano huu mkuu, Maria, Bikira na Mama, na tumwombe atusaidie, kupitia maombezi yake, kujibu kile tunachoombwa kupitia mfano wake: Je, ninaishi uanachama wangu katika Kanisa kwa imani ya unyenyekevu na hai? Je, ninatambua ndani yake jumuiya ya agano ambalo Mungu amenipa la kurudisha upendo wake usio na kikomo? Je, ninahisi kuwa sehemu hai ya Kanisa, kwa utii kwa wachungaji walionipatia na Mungu? Ninamtazama Maria kama mfano, mshiriki bora, na mama wa Kanisa, na ninamwomba anisaidie kuwa mfuasi mwaminifu wa Mwanae.

Papa akielekeza sehemu ya jaribio la 1981
Papa akielekeza sehemu ya jaribio la 1981   (@Vatican Media)

Kwa kuhitimisha Papa Leo XIV alisema: “Dada na kaka, Roho Mtakatifu, aliyemshukia Maria na ambaye tunamwomba kwa unyenyekevu na uaminifu, atujalie kupata uzoefu kamili wa mambo haya ya ajabu. Na, baada ya kusoma Katiba ya Lumen Gentium, tumwombe Bikira Maria atupatie zawadi hii: upendo wa Mama Mtakatifu kwa Kanisa ukue ndani yetu sote. Na iwe hivyo!”

KATEKESI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

 

13 Mei 2026, 12:46