Tafuta

2026.05.16 Papa akutana na watoto wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Kipaimara wa Jimbo Kuu la Genova,Italia. 2026.05.16 Papa akutana na watoto wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Kipaimara wa Jimbo Kuu la Genova,Italia.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV kwa watoto wa Kipaimara,Jimbo Kuu la Genova:muwe mashuhuda

Papa Leo XIV akikutana na watoto wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Kipaimara kutoka kwa Jimbo Kuu la Genova Jumamosi Mei 16,aliwashauri wasiishi imani yao peke yao bali kwa pamoja wakiunda urafiki na kujenga jumuiya zinazodumu.Amewasihi waitikie ndiyo kwa Yesu katika ulimwengu unatoka kutengenisha naye

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kutoka Jimbo Kuu la mjimkuu wa Liguria, Genova nchini Italia kwa kusindikizwa na Askofu Mkuu Marco Tasca, takriban watu 600 kuanzia watoto wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Kipaimara na wale ambao tayari, pamoja na Mapadre na makatekista 150, walipokelewa asubuhi tarehe  16  Mei 2026 na Baba Mtakatifu  Leo XIV katika Ukumbi wa Baraka katika Jumba la Kitume mjini Vatican, ambapo Papa aliwapatia maarifa katika salamu zake bila maandishi. Baba Mtakatifu akiwageukia kwanza kabisa  aliwasalimu kuanzia na Askofu Mkuu na kwa wote waliokuwa kwenye ukumbi. Aliwakaribisha katika nyumba ya Mtakatifu Petro, Vatican  na Roma. “Mmetoka Genova, na kutoka katika Parokia mbalimbali. Kuna Parokia ninayoijua vizuri zaidi, Manesseno: wako wapi? Mko hapa? Mmefanya vizuri! Nyote mmefanya vizuri! Karibuni!," Papa alisema.

Papa na watoto wa Jimbo Kuu la Genova,Italia
Papa na watoto wa Jimbo Kuu la Genova,Italia   (@Vatican Media)

Furaha ya Askofu ni kuadhimisha Kipaimara

Papa aliongeza kusema kuwa “Mojawapo ya furaha kubwa ya Askofu, nadhani katika majimbo yote, ni kuadhimisha  Kipaimara, kwa sababu ni zawadi ya Roho Mtakatifu kweli. Baadhi yenu tayari mmepokea Sakramenti, wengine bado wanajiandaa. Ni vizuri sana kupokea Sakramenti hii, kwa sababu utimilifu wa Roho Mtakatifu hutupatia shauku hii, nguvu hii, uwezo huu wa kumfuata Yesu Kristo, kusema "ndiyo" kwa Bwana kila wakati, kutoogopa kufuata kwa ujasiri, kuishi imani katika ulimwengu ambao mara nyingi hutaka kutuongoza mbali na Yesu.” Papa Leo XIV aliendelea: “Na Roho Mtakatifu yuko pamoja nasi kwa njia ya pekee Dominika ijayo, tunaposherehekea Pentekoste: ukumbusho wa uzoefu wa wanafunzi wa kwanza, Mitume, waliompokea Roho Mtakatifu ili kutangaza Injili, kutangaza upendo wa Mungu. Na nyote mko na mtakuwa washiriki katika utume huu, kwa sababu sote tumetumwa: kwa familia zenu, kwa marafiki zenu, kwa watu wote. Ninyi pia lazima muwe shuhuda aliye hai wa Roho anayeishi ndani yetu.”

Papa amekutan an watoto wa kipaimara wa Jimbo Kuu la Genova
Papa amekutan an watoto wa kipaimara wa Jimbo Kuu la Genova   (@Vatican Media)

Kutoweka Parokiani baada ya Kipaimara

Kwa hivyo, Papa Leo aliongeza:  “ikiwa kutoa Kipaimara ni mojawapo ya furaha kubwa ya Askofu, lakini kuna jambo lingine linalosikitisha. Ni kwamba wakati mwingine, Askofu anapotoa Kipaimara, zawadi ya Roho Mtakatifu, baadaye hawaoni watoto tena! Wanatoweka kutoka Parokiani. Na katika hili ninataka kuwaomba kwamba: mzingatie hasa mojawapo ya karama za Roho Mtakatifu, ambayo inaitwa 'uvumilivu.' Msisahau yale mliyoyapitia wakati huu, ikiwa ni pamoja na furaha ya kuja Roma, kusherehekea pamoja, kusali pamoja: furaha hii iishi mioyoni mwenu na kuendelea kuwa wanafunzi waaminifu wa Yesu Kristo; Mvumilie katika imani, mrudi parokiani, kwani kuna shughuli nyingi, fursa nyingi, lakini zaidi ya yote ya  maisha ya imani, kwa sababu Yesu Kristo anataka kutembea nanyi, na kila mmoja wenu, na nanyi nyote katika jumuiya, jambo ambalo ni muhimu sana. Hatuiishi imani tu, tunaishi pamoja. Na kuunda mahusiano haya ya urafiki, ya jumuiya, ni njia ya kuishi uvumilivu kama wanafunzi wa Yesu," Papa alifafanua.

Papa na watoto wa Kipaimara wa Jimbo Kuu la Genova,Italia
Papa na watoto wa Kipaimara wa Jimbo Kuu la Genova,Italia   (@Vatican Media)

Ushauri wa Papa: "Mbaki na kudumu katika imani"

“Kwa hivyo, msisahau hili! Ni vizuri kuja Roma, ni vizuri kupokea Sakramenti, ni vizuri kupokea utimilifu wa Roho Mtakatifu, lakini ni muhimu sana kwamba kila mmoja wenu pia afanye ahadi hii, ahadi hii kwa Bwana: kwamba mnataka kweli kuendelea kuwa kama  marafiki zake, wanafunzi wake, wamisionari wake, na kwamba mnataka kudumu katika imani. Kwa hivyo ninawaachieni neno hili.” Papa Leo XIV alisisitiza tena kwa hawa watoto: “Ninawaalika msimame, ili tuweze kuomba pamoja sala ambayo Yesu alitufundisha. Kisha ninawapati baraka zangu na kuwasalimu baadhi yenu ninapoondoka. Siku hii pia iwe msaada mkubwa kwenu katika safari yenu ya imani." Baba Mtakatifu alihitimisha kwa kusali pamoja sala ya Baba Yetu..., Baraka na kuwatakia heri wote.

Papa Leo XIV akizungumza na Watoto wa Jimbo Kuu la Genova, Italia
Papa Leo XIV akizungumza na Watoto wa Jimbo Kuu la Genova, Italia   (@Vatican Media)
PAPA NA WATOTO WA KIPAIMARA WA GENOVA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

16 Mei 2026, 12:44