Papa Leo XIV na ukaribu kwa ajili ya Watu wa China&nchi zinazoteseka kwa vita
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya sala ya Malkia wa Mbingu, Dominika tarehe 24 Mei 2026 wakati Mama Kanisa anasheherekea Pentekoste, sikukuu kubwa ya kuzaliwa kwa Kanisa, Baba Mtakatifu Leo XIV akiwageukia waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro alisema: “Leo ni Siku ya Maombi kwa ajili ya Kanisa nchini China, ukumbusho wa kiliturujia wa Bikira Maria, Msaada wa Wakristo, unaoheshimiwa kwa ibada kubwa katika Madhabahu ya Sheshan huko Shanghai. Tuunganishe sala zetu na zile za Wakatoliki wa China, kama ishara ya upendo wetu kwao na ushirika wao na Kanisa la ulimwengu wote na Mrithi wa Petro.”
Watu wa china waweze kuwa mbegu ya matumaini na amani
Papa Leo XIV, kadhalika aliendelea kuwa: “Maombezi ya Malkia wa Mbinguni yawapatie Jumuiya ya waamini nchini China neema ya umoja na kuwapa kila mtu nguvu ya kushuhudia Injili katika mapambano yao ya kila siku, ili wawe mbegu ya matumaini na amani.”
Waliopoteza maisha katika mgodi,China,Nchi Takatifu na mashariki ya Kati
Na zaidi Papa aliongeza “Hasa, ninaomba amani ya milele kwa ajili ya waathiriwa wa ajali iliyotokea siku chache zilizopita katika mgodi kaskazini mwa China. Kwa Maria Mtakatifu sana Msaada wa Wakristo, tunawakabidhi pia jumuiya za Kikristo za Nchi Takatifu, Lebanon na Mashariki ya Kati nzima, ambao wanateseka kwa sababu ya vita.”
Salamu
Papa alitoa salamu zake kwa mahujaji kuanzia Roma na na mahujaji kutoka nchi mbalimbali! “Hasa, ninawasalimu kundi la watu wenye ulemavu kutoka Poland; pamoja na mahujaji ambao wamekuja kwa baiskeli kutoka Kelmis, Ubelgiji—hongera!” Papa alihitimisha kwa kuwatakia Dominika Njema ya Pentekoste.
