Papa Leo XIV Hija ya Kichungaji Acerra: Miaka 11 ya Waraka wa Laudato si
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Juma la “Laudato si”, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 23 Mei 2026 amefanya hija ya kichungaji eneo la Acerra, maarufu kama "Terra dei Fuochi" yaani “Ardhi ya moto” eneo ambalo limeathiriwa sana na taka maalum na hatari zilizotupwa eneo hili kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za nchi na mashirika pamoja na makampuni ya uhalifu. Hili ni eneo linalopatikana katika Majimbo ya Napoli na Caserta. Uchafuzi huu wa mazingira nyumba ya wote, kimekuwa ni chanzo kikuu cha kusambaa na kuenea kwa magonjwa ya Saratani sanjari na uchafuzi mkubwa wa mazingira. Baba Mtakatifu Leo XIV amepata nafasi ya kukutana na kusalimiana na watu wa Mungu, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka kumi na moja; yaani tarehe 24 Mei 2015, Baba Mtakatifu Francisko alipochapisha Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Huu ni Waraka unaozungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa ikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya Ikolojia na maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuunganisha athari za uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote, magonjwa ya kijamii; vita na kinzani; wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi pamoja na baa la umaskini linalopekenya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaunda mfumo wa uchumi na masuala ya kijamii yanayokita misingi yake katika haki, heshima na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, daima: utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza.
Hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Leo XIV ni kutekeleza ile nia iliyooneshwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Accerra tarehe 24 Mei 2020, hija hii ikafutwa kutokana na mlipuko wa Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, (COVID-19). Hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Leo XIV huko Acerra ni kuonesha mshikamano wa huruma na upendo kwa familia zilizoathirika kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira ambao umepelekea vifo vya watu wengi katika eneo hili. Hiki ni kilio cha watu wa Mungu kwa Serikali ya Italia, inayopaswa kutoa majibu muafaka. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake kwa watu wa Mungu mkoa wa Campania, lakini zaidi familia za waathirika wa uchafuzi mkubwa wa mazingira, amesema Waraka huu ni kielelezo cha utume wa Kanisa, kilio cha kazi ya uumbaji na maskini, kilio ambacho kimesikika mbele ya Mwenyezi Mungu kutokana na vifo na maafa makubwa yaliyosababishwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, tabia ya kutojali ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mambo ambayo yamechangia kuharibu mazingira asilia na ya kijamii, na kwamba, kilio hiki kinadai toba na wongofu wa kiikolojia.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema yuko kati yao kama chemchemi ya faraja kwa waathirika waliowapoteza wapendwa wao na wahusika kutoadhibiwa kwa muda mrefu; yuko kati yao kama kielelezo cha shukrani kwa wale ambao wamejibu ubaya kwa kutenda mema na kwamba, Kanisa limesimama kidete kukemea uchafuzi mkubwa wa mazingira kwa sauti ya kinabii na hivyo kuwa ni chemchemi ya matumaini na maisha mapya kama Nabii Ezekieli anavyosimulia: “Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye Bwana akanichukua nje katika roho, akaniweka chini katika bonde lile lililojaa mifupa, akanipitisha pande zote. Nikaona ya kuwa ni wengi sana bondeni, na wote walikuwa wamekauka” Ezekieli 37:1-2. Eneo hili kwa asili lilijulikana kama “Campania felix” yaani “Mkoa wa furaha” kielelezo cha maisha, uzuri na uzao. Hii ni furaha iliyokuwa inabubujika kutoka katika uzalishaji wa mazao; amana na utajiri wake wa kitamaduni, kwa bahati mbaya furaha hii imekatishwa na utamaduni wa kifo unaopata chimbuko lake kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, wao wamechagua fungu bora la kuanzisha safari na dhamana ya kutafuta haki msingi!
Kanisa lina dhamana ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, Neno la Mungu ni chemchemi ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo, ukosefu wa haki msingi za binadamu, hali ya kutojali; uhalifu na rushwa mambo ambayo yanaendelea kukoleza utamaduni wa kifo, lakini Mwenyezi Mungu ana uwezo mkubwa wa kugeuza maombolezo kuwa ni kicheko na furaha. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume wa “Laudato si” kwa kukazia uchaguzi wa mfumo wa maisha ambao haichafui sana mazingira; teknolojia iwe ni kwa ajili ya kutatua matatizo na changamoto za maisha ya watu, alikazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. Laudato si, 112. Hapa Injili inakuwa ni chemchemi ya maisha mapya; kwa watu kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano; kwa kukazia elimu makini; fadhila ya uaminifu katika kazi; ugawanaji sawa wa majukumu na madaraka, kwa kuwaheshimu binadamu na viumbe wengine wote, changamoto kwa Jumuiya hii kuungana na kushikamana katika imani na utekelezaji wa dhamana na majukumu mbalimbali yaliyoko mbele yao, ili maisha yaweze kusonga mbele!
Baba Mtakatifu Leo XIV anawaombea Roho Mtakatifu ili awajalie kuona “Jeshi kubwa la amani” likiinuka ili kuganga na kuponya majeraha; Moto wa Roho Mtakatifu unaopyaisha, Moto unaowasha mioyo na akili za watu, ili wajikite katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; moto wa faraja, uangalifu na upendo wa kweli. Roho Mtakatifu awe ni chemchemi ya maisha mapya kwa familia zilizokumbwa na athari kubwa za uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote, wawarishe jirani zao hisia ya uwajibikaji; wafishe chuki, uhasama na tabia ya kutaka kulipiza kisasi kwa kuwa watu wa kwanza kutenda haki, kwa ushuhuda wa maisha pamoja na kufundisha kujali. Hii ni safari ambayo inatekelezwa na Kanisa, kwa kutangaza na kushuhudia haki msingi, Injili ya maisha pamoja na malezi ya utunzaji bora wa mazingira. Baba Mtakatifu anawakumbusha viongozi wa Kanisa kwamba, wamepewa dhamana ya kuongoza, kuwa karibu na watu wa Mungu katika unyenyekevu, ujirani mwema; kwa kusamehe na kusahau, ili kuondokana na utamaduni wa upendeleo na kiburi ambao umesababisha madhara makubwa ndani na nje ya Italia; utamaduni huu lazima ukomeshwe. Roho Mtakatifu awe ni chemchemi ya umoja na ushirikiano, ili kuzaliwa upya kwa mazingira na jamii, yote haya yapate uhalisia wake kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, kwa kuzishika Amri za Mungu, ili Mungu aweze kuwa ni Mungu wao. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kumwomba, Kristo Yesu, Mfufuka awakirimia karama ya kuishi kwa umoja, ili kupokea na kulifanyia kazi Neno la Mungu, kama sehemu ya Mahujaji hapa duniani, kuelelekea katika maisha ya umilele.
Kwa upande wake Askofu Antonio Di Donna wa Jimbo la Acerra, Kusini mwa Italia katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV aweze kuzungumza na watu wa Mungu amesema, hotuba yake ni kama kumbukumbu ya toba na wongofu wa ndani; ya kuomba huruma na msamaha kutoka kwa Mungu, ili kuanza upya na yale yaliyotokea kamwe yasijirudie tena! "Terra dei Fuochi" yaani “Ardhi ya moto” eneo ambalo limeathiriwa sana na taka maalum na hatari zilizotupwa eneo hili kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za nchi, tafiti zinaonesha kwamba, ni uzembe uliofanywa na makampuni pamoja na wafanya biashara waliokuwa wanatupa, kuchoma taka za sumu katika eneo hili, kiasi kwamba eneo la Acerra limegeuka kuwa ni sehemu iliyotelekezwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, inayosadaka maisha yake kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa maeneo mengine. Uchafuzi wa mazingira ni chanzo cha vifo, magonjwa ya kudumu pamoja na ukosefu wa maendeleo endelevu. Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, takwimu zinaonesha kwamba, vijana 150 wamepoteza maisha na wengine wengi wanaendelea na matibabu ya muda mrefu. Hizi ni familia zinazopaswa kuambiwa ukweli mchungu. Mwaka 2025 Mahakama ya Haki Msingi za Binadamu Jumuiya ya Ulaya, iliishutumu Italia kwa kushindwa kuwalinda raia wake kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira na matokeo yake kuna ongezeko kubwa la umaskini, magonjwa na ujinga. Ni katika muktadha huu, Kanisa daima limekuwa ni sauti ya kinabii kwa waathirika hawa, ili kutafuta na kutangaza ukweli, Kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kama sehemu ya amana na utajiri wake wa imani. Kumbe, ombi lao kwa Baba Mtakatifu ni kuwaimarisha katika imani, ulinzi wa mazingira nyumba ya wote pamoja na faraja kwa waathirika na kwamba, ujumbe kwa wahusika wa vitendo hivi ni toba na wongofu wa ndani.
Baba Mtakatifu Leo XIV baada ya kusalimiana na baadhi ya viongozi wa Kanisa na familia zilizoathirika na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, alikwenda kwenye Uwanja wa “Calipari” hapa akakutana na Mameya wa miji tisini inayounda eneo la "Terra dei Fuochi" pamoja na watu wa Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewaambia kwamba, yuko kati yao kuwakumbusha kwamba, hakuna ukosefu wowote wa haki msingi za binadamu unaoweza kufutilia mbali uzuri wa Acerra na kwamba, yuko kati yao ili kukazia umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kuwajibika, ili hatimaye kuondokana na utamaduni wa kifo. Anawashukuru watu wa Mungu kwa kupokea na hatimaye kumwilisha katika maisha na vipaumbele vyao ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kutoka katika Waraka wake wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Hii ni changamoto kwa Kanisa kuhakikisha kwamba, linatoka nje, kwa kujenga na kudumisha dhana ya kimisionari na kisinodi, kwa kutembea na kusikilizana kwa pamoja, ili kuondokana na dhana ya upendeleo; kwa kuchagua Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kujikita katika utawala wa sheria na haki; kwa kuwajibika katika kukuza na kudumisha haki inayomwilishwa katika huduma ya Injili ya uhai na kwamba, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbe cha kwanza kwa wote na kwamba, kuna haja ya kuwa na mashuhuda wa mkataba mpya unaosimikwa katika kanuni maadili na utu wema na uwajibikaji. Uchafuzi na uharibifu wa mazingira unahitaji kwa namna ya pekee kuwa na mtazamo, namna ya kufikiri na kutenda; sera makini, mpango wa elimu, mtindo wa maisha ya kiroho ambavyo kwa pamoja vinapinga uvamizi wa mfumo wa teknokrasia.
Vita, kinzani na migogoro mbalimbali ni matokeo ya watu wachache kutaka kukwapua rasilimali na utajiri wa nchi; teknolojia inayopania kupata faida kubwa kwa mafao na ustawi wa watu wachache katika jamii na matokeo yake ni ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Kuna haja ya kuleta mabadiliko kwa kuwa na mtazamo mpya anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV. Ili kuweza kukiachia kizazi kijacho urithi mzuri, Jamii haina budi kuwekeza katika elimu makini kwa watu mbalimbali wa Taifa la Mungu kwa watu wote kuendelea kujifunza kwa pamoja; kwa kutoa na kupokea na hivyo kuthubutu kutembea pamoja na Kristo Yesu kwa kuwa ni mfuasi wake bora zaidi. Kunahitajika mabadiliko makubwa ya mtazamo wa kiuchumi, kiraia hata katika maisha ya kiroho, ili eneo hili liweze kuchanua upya, jambo la msingi ni mshikamano wa udugu wa binadamu, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha kazi ya uumbaji. Watu watafute utajiri wa halali kwa kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea: utu, heshima, haki msingi za binadamu, maendeleo na ustawi wa wengi. Ni muda wa toba na wongo wa ndani kwa kuzima kiu na njaa ya haki; kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano; kwa kuondokana na maamuzi mbele, ili kuanza kujikita katika utamaduni wa watu kukutana na kuanza kutembea kwa umoja. "Terra dei Fuochi" ni kiashiria cha ukosefu wa ulinzi na usalama; ugumu wa maisha; watu kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbe vya jamii.
Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mlinzi na Mwombezi wa Italia. Mtakatifu Francisko wa Assisi aliishi kati ya Mwaka 1181 hadi tarehe 3 Oktoba 1226. Maadhimisho ya Jubilei hii yalizinduliwa rasmi tarehe 29 Novemba 2021 na kilele chake ni tarehe 3 Oktoba 2026, kwa kuwashirikisha kikamilifu waamini walei na watawa kuweza kutembea kwa pamoja. Mtakatifu Francisko anatambulikana sana kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Maskini, Amani na Mazingira nyumba ya wote; chimbuko la yote haya ni upendo kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiasi cha kumzawadia Madonda Matakatifu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha: unyenyekevu, huruma na upendo kwa Mungu na jirani. Huu ni mwaliko wa kumfuasa Kristo Yesu, kwa kusoma, kutafakari hatimaye, kumwilisha Habari Njema ya Wokovu katika uhalisia wa maisha ya waamini kwa kushuhudia upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa njia ya ufukara wa Kiinjili, Wafranciskani, wanahimizwa kupyaisha sura ya Mama Kanisa katika maisha na huduma zao. Mtakatifu Francisko wa Assisi anasema, amani ya kweli inasimikwa katika huduma makini kwa jirani kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa binadanu; kwa kujitahidi kuishi kwa pamoja, kwa kutatua matatizo, changamoto na kutumia kwa umakini fursa zilizopo, ili kuona mapambazuko mapya. Baba Mtakatifu Leo XIV, mwishoni mwa hotuba yake amewaambia watu wa Mungu kwamba, hija hii ya kichungaji ni muhimu sana kwa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro; anaendelea kuwabeba na kuwakumbatia katika sala na sadaka yake na kwamba, anawakabidhi kwa Bikira Maria, Nyota ya Asubuhi kwa ajili ya mustakabali wa maisha yao ya leo na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi.
Kwa upande wake Askofu Antonio Di Donna wa Jimbo la Acerra, Kusini mwa Italia anasema, umefika wakati wa kumwilisha kwa matendo Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ili uweze kuwa ni dira na mwongozo katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili eneo hili badala ya kuendelea kuwa ni “Terra dei Fuochi” libadilike na kuwa ni “Bustani ya Campania na Bara la Ulaya” katika ujumla wake. Naye Dr. Tito d’Errico Mstahiki Meya wa Mji wa Acerra, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuwatembelea wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha kumbukizi ya Miaka kumi na moja, tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Waraka wake wa kitume wa: “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”unaotoa kipaumbele cha pekee kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu; afya na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu kwa uwepo na ushuhuda wake amegusa undani wa madonda ya Acerra yanayohitaji: Ukweli, Haki na Utunzaji Bora wa mazingira nyumba ya wote. Huduma yao kama Mameya wastahiki inasimikwa katika wimbo wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, Laudato si na kwamba, wanapenda kuhimiza utawala wa sheria, uaminifu pamoja na kuendelea kukuza uchumi endelevu; kwa kuheshimu na kudumisha sheria, taratibu na kanuni za kazi kwa kulinda kazi kama utimilifu wa heshima, utu na utambulisho wa mwanadamu. Amempongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuendelea kuwa ni chombo na shuhuda wa haki, amani na maridhiano; kwa kulinda kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kwa hakika hii imekuwa ni siku ya baraka kwa watu wa Mungu mjini Acerra, unaopania kuwa ni chimbuko la matumaini na umoja katika tofauti zake msingi.
