Papa Leo XIV: Huduma Kwa Wagonjwa Mshikamano wa Huruma na Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ugonjwa wa “Amyotrophic Lateral Sclerosis” (ALS), au ugonjwa wa Lou Gehrig, ni ugonjwa unaoendelea na kuukumba mfumo wa neva ambao husababisha kifo cha nyuroni za mwendo zinazodhibiti misuli ya hiari na hivyo kusababisha udhaifu wa misuli polepole, kudhoofika, na hatimaye kupooza, kwa kawaida kusababisha kushindwa kupumua ndani ya miaka 3 hadi 5. Ingawa hakuna tiba maalum, lakini matibabu yanalenga kudhibiti dalili na maendeleo ya polepole kwa wagonjwa. Ni katika muktadha huu, Chama cha Italia cha “Amyotrophic Lateral Sclerosis, AISLA” kilianzishwa kunako mwaka wa 1983 kwa lengo la kuwa ni chombo cha rejea cha kitaifa cha ulinzi, usaidizi, na utunzaji wa wagonjwa wa ALS, ili hatimaye kukuza ufahamu kuhusu ugonjwa huo na kuhimiza taasisi zinazofaa kutoa huduma inayofaa kwa wagonjwa hawa.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 9 Mei 2026 alikutana na kuzungumza na wanachama wa Chama cha Italia cha “Amyotrophic Lateral Sclerosis, AISLA” na kuwakumbusha kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto za kiafya ni fursa makini ya kutoa na kupokea huruma na upendo; kwa kuonesha ukaribu kwa wagonjwa, kwani hakuna mtu awaye yote anayepaswa kuachwa peke yake katika shida na mahangaiko ya maisha. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wanachama wa Chama hiki kwa kuendelea kusimama kidete: ili kulinda, kusaidia na kutibu ugonjwa huu unaosababisha mateso makubwa kwa waathirika. Hiki ni Chama kinachowaunganisha wagonjwa, familia na wale wanaopata tiba na hivyo kutengeneza mtandao wa ujirani mwema, kielelezo makini cha huduma iliyokuwa inatolewa na Kristo Yesu mwenyewe kwa wagonjwa: Rej Lk 4:38-39.
Huu ni mkataba unaosimikwa katika imani, ujasiri na ushuhuda unaoonesha kwamba, maisha ni zawadi kubwa inayozidi hata ugonjwa na kwamba, changamoto za magonjwa zinaweza kukabiliwa kwa pamoja na hivyo kugeuka kuwa ni fursa makini ya kutoa na kupokea huruma na upendo. Baba Mtakatifu Leo XIV anawashukuru na kuwapongeza wanachama hawa, kwa kuendelea kuwa ni Manabii na mashuhuda wa tunu msingi za maisha; wanaojitaabisha kufanya tafiti za kisayansi, kuragibisha habari kuhusu ugonjwa huu pamoja na huduma kwa wagonjwa na kwamba, ulimwengu mambo leo unahitaji ushuhuda kama huu, dhidi ya utamaduni wa kifo. Hiki ni chama kinachoendelea kuragibisha umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za wagonjwa. Ujenzi wa ujirani mwema, unawataka kuwa karibu na makazi ya wagonjwa pamoja na waathirika, kwani huduma hii inawataka kuonesha uwepo wao wa karibu katika mahitahi yao msingi ya kibaiolojia, kimwili na hata kiroho.
Mama Kanisa anawapongeza kwa ushuhuda wa uwepo wao wa karibu kwa kuwasindikiza na kuwasaidia hata katika maisha yao ya kiroho, huku wakijitahidi kujibu maswali msingi juu ya mateso na mahangaiko ya maisha. Katika shida, mahangaiko na mateso, anasema Baba Mtakatifu Leo XIV, hakuna mtu anayepaswa kuachwa ili “apambane na hali yake”, huu ni mwaliko wa kukataa kumezwa na utamaduni wa kifo. Rej. Evangelii gaudium, 53. Kristo Yesu katika maisha na utume wake alikuwa akifundisha, kuhubiri Habari Njema ya Wokovu na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Rej. Mt 9:35. Ni kwa njia hii, Kristo Yesu aliweza kumwilisha mateso na hatimaye, kumwilisha ndani mwake ile “Via Crucis” yaani “Njia ya Msalaba” kama kipindi cha majaribu, mateso: kiroho na kimwili, akaonesha upendo na mshikamano wake na binadamu wote, kwani mateso yake yalikuwa ni Ufunuo wa: Nguvu, huruma na upendo wa Mungu Baba kwa wanadamu. Rej. Flp 2: 5-11. Ni katika muktadha wa Fumbo la Pasaka kwamba, wabatizwa wote ni watoto wa Fumbo la Pasaka, watu wa Injili ya matumaini; wanaojenga na kusimika maisha yao katika nguzo ya mshikamano na ujasiri, changamoto na mwaliko kwa waamini kutembea katika ujasiri na matumaini ya Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu amewahakikishia wajumbe hawa sala na maombi yake na kwamba, Bikira Maria sanjari na Watakatifu mashuhuda wa Injili ya upendo, wawasindikize katika maisha yao na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.
