Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi usiku, tarehe 30 Mei 2026 amewaongoza mahujaji kutoka katika madhabahu 200 yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufunga Mwezi wa Rozari Takatifu Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi usiku, tarehe 30 Mei 2026 amewaongoza mahujaji kutoka katika madhabahu 200 yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufunga Mwezi wa Rozari Takatifu   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Ibada ya Rozari Takatifu! Mashuhuda Kutoka Tanzania

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi usiku, tarehe 30 Mei 2026 amewaongoza mahujaji kutoka katika madhabahu 200 yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufunga Mwezi wa Rozari Takatifu na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia watu wa Mataifa zawadi ya imani, kwa njia ya Tafakari ya Rozari Takatifu ambayo kimsingi ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Kuna Ushuhuda kutoka kwa Mahujaji wa Tanzania! Rozari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi usiku, tarehe 30 Mei 2026 amewaongoza mahujaji kutoka katika madhabahu 200 yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufunga rasmi mwezi Mei uliotengwa kwa heshima na ibada kwa Bikira Maria sanjari kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia watu wa Mataifa zawadi ya imani, kwa njia ya Tafakari ya Rozari Takatifu ambayo kimsingi ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Baba Mtakatifu pamoja na waamini wametafakari kuhusu matendo ya furaha yaliyoongozwa na waamini kutoka: Lebanon, Nicaragua, Ukraine, Siria na Tanzania kwa nafsi ya Padre John Mlay, C.PP.S. Itakumbukwa kwamba, Madhabahu kimsingi ni mahali pa: Sala na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, anayetoa machozi ya faraja kwa wale wanaoteseka na kuhuzunika huku Bondeni kwenye machozi. Ni mwombezi wa watu waliovunjika na kupondeka moyo; watu waliokata tamaa na kwamba, Bikira Maria anajaribu kujibu sala ya kila mwamini anayekimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za: imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Madhabahu ni mahali pa ukimya unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: baraka, neema na rehema pamoja na kudumisha upendo kwa Mungu na jirani! Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Bikira Maria Mama wa Mungu ni Faraja kwa wagonjwa
Bikira Maria Mama wa Mungu ni Faraja kwa wagonjwa   (@Vatican Media)

Sala ya Rozari ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani wenye shida na mahangaiko mbalimbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu. Kwa njia ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kila mtu ajitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mchakato wa kuganga na kuponya ulimwengu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, wamekusanyika, mwshoni mwa Mwezi Mei, kuomba kwa bidii zaidi zawadi ya amani, ili mioyo ya watu ifunguke kwa toba na wongofu wa ndani, na watu wote waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, maridhiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Sala ya Rozari Takatifu iwe dhamira ya kila mwamini kama mjenzi na chombo cha amani. Mzaburi anasema, “Na nisikie atakavyosema Mungu BWANA, Maana atawaambia watu wake amani, Naam, na watauwa wake pia, Bali wasiurudie upumbavu tena.” Zab 85.8. Hii ni Zaburi ambayo imewasindikiza waamini katika tafakari ya Rozari Takatifu kwani ndani mwake mna chemchemi ya matumaini, mintarafu hali ngumu ya maisha, vita na kinzani sehemu mbalimbali za dunia. Bikira Maria ni kielelezo cha mwamini msikivu, anayetega sikio lake ili kumsikiliza Mwenyezi Mungu, ni mfano wa utii ambao umemwezesha kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Tafakari ya Mafumbo ya Rozari Takatifu, yanawawezesha waamini kumfahamu Kristo Yesu, Neno wa Mungu na ni Neno la amani kwa wale wote wanaomrudia kwa moyo uliovunjika na kupondeka; anayekuja kutafuta huruma na upendo wa Mungu na kwamba, kwa hakika ataweza kukirimiwa amani na yeye mwenyewe atakuwa ni shuhuda na chombo cha amani.

Amani ni zawadi kutoka kwa Mungu! Inawezekana timiza wajibu wako
Amani ni zawadi kutoka kwa Mungu! Inawezekana timiza wajibu wako

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, amani ni zawadi inayopaswa kutafutwa kwa moyo wa toba, wongofu wa ndani na unyenyekevu na kwamba, hii ni dhamana na wajibu wa kila siku na kwamba, amani ya kweli inapata chimbuko lake katika: Haki, upendo na utulivu unaowaunganisha watu, familia, jumuiya pamoja na watu wa Mataifa. Hata katika ulimwengu mamboleo unaoendelea kusheheni vita, kinzani na migogoro kila kukicha, bado amani ya kweli inawezekana kwa kusikiliza na kujibu kilio cha watu wasiokuwa na sauti: Hawa ni watoto wasiokuwa na hatia, wazazi waliokata tamaa, wafungwa wanaoteswa, kudhulumiwa na kunyanyaswa, wakimbizi na wahamiaji, watu wanaoteseka; wote hawa wanatamani kusikia neno la amani. Amani ni jambo linalowezekana kwani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, Kristo Yesu ni amani ya waja wake, kwani ni kwa njia ya Kristo Yesu kuta za utengano na uadui zinavunjiliwa mbali na badala ya kujimwambafai, fadhila ya unyenyekevu inashika mkondo wake na kwamba, kwa njia ya Kristo Yesu, mwanadamu amekombolewa kutoka katika dhambi na mauti. Hii ni changamoto kwa wafuasi wake kutenda kama wafuasi amini kwa kujikita katika upendo na hapo Roho Mtakatifu ataweza kutenda hata kile ambacho kinaonekana kwamba, kwa nguvu za binadamu hakiwezekani lakini kwa njia ya Roho Mtakatifu yote yanawezekana, jambo la msingi ni kwa kila mtu kuwajibika barabara.

Waamini kutoka katika madhabahu 200 wameungana na Papa Kusali Rozari
Waamini kutoka katika madhabahu 200 wameungana na Papa Kusali Rozari   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ni kwa njia hii, sala za waamini zinageuka kuwa ni utume na unabii. Kumbe,  pasiwepo tena na machozi kwa watu wasio na hatia katika miji ; hakuna mtu atakayelazimika kukimbia nyumba yake kwa sababu ya tishio la mabomu; tamaa ya madaraka na jeuri ya maneno kwani hii itatoa nafasi kwa kiu ya haki na ukweli. Yote haya yanawezekana ikiwa kila mtu anatekeleza dhamana na wajibu wake, kwa kuanzia katika mambo madogo madogo, lakini muhimu; kwa kujiepusha na vurugu zote za matusi katika maisha ya kila siku na kwenye mitandao ya kijamii. Amani ya kweli huanzia katika moyo wenye upendo; inashuhudiwa na midomo inayosema maneno ya upatanisho; inaonekana katika macho yanayotazama ulimwengu kwa upole na hekima. Hii ni nguvu ya kweli na upendo. Mwenyezi Mungu anatafuta vyombo na wajenzi wa amani, Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awasaidie waamini kila siku kuweza kujibu: “Mimi hapa” si kwa maneno matupu, bali kwa vitendo.

Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia ya ukombozi
Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia ya ukombozi   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha wa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, hivi karibuni Kundi la Pili la Mahujaji 35 kutoka Tanzania limetembelea; Ureno, Ufaransa na Roma katika madhabahu ya Bikira Maria. Hili ni kundi lililoandaliwa na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S katika nafsi ya Padre John Greyson C.PP.S., Dekano wa Dekania ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Jimbo Kuu la Dodoma, Tanzania. Hili ni kundi linalowahusisha watu wa Mungu kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jimbo kuu la Dodoma, Jimbo la Moshi, Iringa, Bukoba na Kayanga. Wamesali na kumwomba Bikira Maria awaongoze na kuwaombea ili hatimaye, waweze kuwa ni wafuasi amini wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini wanahimizwa kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani sanjari na kuombea amani. Ni katika muktadha huu, Familia ya Bwana na Bibi Richard Donatian Toba Njau kutoka Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi, Jimbo kuu la Dar Es Salaam wanawaalika waamini kujibidiisha kusali Rozari Takatifu, kuwafundisha na kuwarithisha tunu msingi za Kiinjili watoto na vijana, ili wote kwa pamoja waweze kujikita katika kuutafuta Uso wa Mungu katika hija ya maisha yao ha duniani. Wanandoa waendelee kupendana, kuvumiliana, kusamehena pamoja na kujikita katika maisha ya sala, ili haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu viweze kutawala nyoyo zao. Kwa hakika, Bikira Maria ni mfabo bora wa kuigwa katika malezi na makuzi ya watoto. Kuna haja kwa wazazi kuangalia uwezekano wa vijana wao kufanya hija kwenye maeneo matakatifu ili waweze kujifunza mengi.

Papa Leo XIV Rozari Takatifu
31 Mei 2026, 15:28