Tafuta

Papa Leo XIV anamwalika mwanafunzi huyu kushiriki kikamilifu katika: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu; Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti nyingine za Kanisa. Papa Leo XIV anamwalika mwanafunzi huyu kushiriki kikamilifu katika: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu; Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti nyingine za Kanisa.  (ANSA)

Papa Leo XIV: Jengeni Urafiki na Yesu: Katika: Sala, Neno na Sakramenti!

Baba Mtakatifu anamwalika mwanafunzi huyu kushiriki kikamilifu katika: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu; Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti nyingine za Kanisa, ili kutambua mahusiano na kukuza moyo wa utulivu wa ndani bila kuhukumu. Kijana huyu alimwambia Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, ndani mwake alihisi hali ya kukosa amani na utulivu na hivyo kuanza kuchanganyikiwa mintarafu mahusiano aliyokuwa nayo na msichana wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jarida la kila Mwezi lijulikanalo kama “Piazza San Pietro” ni mradi wa ubunifu wa uhariri ulioanzishwa na Hayati Papa Francisko tarehe 25 Novemba 2024 ambao sasa unaendelezwa chini ya uongozi na usimamizi wa Baba Mtakatifu Leo XIV. Jarida hili lina safu ya pekee iliyoratibiwa kibinafsi na Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye kila mwezi anajibu barua kutoka kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kama njia ya kujenga na kudumisha majadiliano ya moja kwa moja, ya kina na jumuishi na wasomaji. Jarida hili la kila mwezi linahaririwa na Padre Enzo Fortunato na kuratibiwa na Kardinali Mauro Gambetti, O.F.M, CONV., Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.  Jarida la "Piazza San Pietro"  ni daraja la kudumu la majadiliano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na moyo wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kukuza na kudumisha tunu msingi za amani, ushirikishwaji; utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitaka Jarida hili liwe ni chombo cha mawasiliano ya kweli yanayoshirikisha, tayari kugawana amana na utajiri wa maisha ya kiroho, ili kukuza na kudumisha ubinadamu wa kweli. Jarida hili huchapishwa kwa lugha ya Kiitalia, Kiingereza na Kihispania. Lengo ni kuwafikia watu wengi zaidi kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, ili kujenga utamaduni wa kusikilizana na watu mbalimbali!

Familia ni Kanisa Dogo la Nyumbani, shule ya sala na utakatifu
Familia ni Kanisa Dogo la Nyumbani, shule ya sala na utakatifu   (@VATICAN MEDIA)

Kwa mwezi Mei 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kumjibu mwanafunzi Pietro kutoka Reggio Calabria kwa kumwambia kwamba, hasiwe mwepesi kukimbilia kuelewa kila jambo kwa mara moja, kwani muda ni mwalimu mvumilivu tena anao uwezo wa kuganga na kuponya madonda kutoka katika undani wa maisha ya mwanadamu. Anamwalika kijana huyu mdogo kukita maisha yake katika Sala za kila siku, kwa kumwambia Mwenyezi Mungu maneno rahisi na machache; Kwa kusoma, Kusikiliza, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele na maisha ya kila siku. Baba Mtakatifu anamwalika mwanafunzi huyu kushiriki kikamilifu katika: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu; Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti nyingine za Kanisa, ili kutambua mahusiano na kukuza moyo wa utulivu wa ndani bila kuhukumu. Kijana huyu alimwambia Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, ndani mwake alihisi hali ya kukosa amani na utulivu na hivyo kuanza kuchanganyikiwa mintarafu mahusiano aliyokuwa nayo na msichana wake.

Jengeni Urafiki na Yesu Kwa njia ya Sala, Neno na Sakramenti
Jengeni Urafiki na Yesu Kwa njia ya Sala, Neno na Sakramenti   (@Vatican Media)

Pietro kutoka Reggio Carabria katika Jarida la Mwezi Mei, 2026 anaandika kwamba, anapoteza urafiki wote ambao umeipamba sura ya maisha ya ujana wake, si tu akiwa shuleni au parokiani bali hata katika uhalisia wa maisha yake ya kila siku. Baba Mtakatifu Leo XIV ana mhakikishia kwamba, kwa hakika anapendwa na Kristo Yesu katika hali yake na jinsi alivyo; maswali na ndoto za maisha yake; hofu na matamanio halali ya maisha na kwamba, upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, utamtangulia na kufuatana naye daima na kwamba hautegemei uchaguzi wa maisha yake au usafiri anaoutumia. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alikuwa pia na marafiki kama Lazaro, Martha na Maria. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kumhakikishia Petro kwamba, Kristo Yesu ni mtu wa kwanza kufahamu hofu na uchungu wa kupoteza urafiki ambao umejengeka katika kipindi cha miaka hii yote ni kweli kutakuwa na mabadiliko katika maisha yake, lakini kile cha kweli hakitapunguka na kitaendelea kubaki miaka yote, katika ukweli wake, upendo wa kweli kamwe haupungui thamani yake na unabaki jinsi ulivyo milele yote, hata kama utabadili sura. Petro anaonesha nia yake ya kutembea katika upendo wa Kristo Yesu, lakini anashindwa kufahamu ni vielelezo vipi anapaswa kuvihifadhi na kuviendeleza ili kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake!

Familia ni Kanisa Dogo la Nyumbani, Shule ya Upendo, huruma na haki
Familia ni Kanisa Dogo la Nyumbani, Shule ya Upendo, huruma na haki   (@Vatican Media)

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, familia inayokita mizizi yake katika upendo wa Kristo Yesu, hiyo inadumu na kwamba, hii ni zawadi adhimu sana kwa Kanisa, kumbe familia inapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Baba Mtakatifu amemhakikishia kijana Petro sala na sadaka yake, ili Mungu mwenyezi,  mwingi wa huruma na mapendo, aweze kumsaidia kutimiza matamanio yake halali katika maisha. Anamkabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria ambaye katika maisha yake alijifunza kutumaini, ingawa katika sakafu ya moyo wake kulikuwa na maswali mazito kuliko hata Yeye mwenyewe.

Papa Leo XIV Jengeni Urafiki na Yesu
26 Mei 2026, 14:41