Tafuta

Hii ni nafasi ya kujenga na kupanua Jumuiya za Kikatoliki zenye ari na mwamko wa kimisionari; Jumuiya zinazokita mizizi yake katika imani inayogeuka na kuwa ni chemchemi ya furaha na maisha mapya katika Kristo Yesu. Hii ni nafasi ya kujenga na kupanua Jumuiya za Kikatoliki zenye ari na mwamko wa kimisionari; Jumuiya zinazokita mizizi yake katika imani inayogeuka na kuwa ni chemchemi ya furaha na maisha mapya katika Kristo Yesu.   (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV Jumuiya ya Kipapa ya Ugani ya Kikatoliki: Injili ya Upendo Kwa Maskini

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, upendo kwa maskini unaweza kueleweka kama “alama ya Kiinjili ya Kanisa aminifu kwa moyo wa Mungu” na hivyo kuwa ni fursa ya kufungua malango kwa ajili ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili na hivyo hii inakuwa ni fursa kwa wale wanaohudumiwa kumfahamu Kristo Yesu, kama kielelezo makini cha ushuhuda kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Jumuiya hii ilianzishwa na Padre Francis Clement Kelley.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bodi ya Wakurugenzi wa Jumuiya ya Kipapa ya Ugani ya Kikatoliki: “The Catholic Extension Society” inafanya kazi kwa ushirikiano na mshikamano na watu wa Mungu ili kujenga na kudumisha Jumuiya za imani ya kikatoliki zenye uchangamfu na zinazopania kufanya mageuzi miongoni mwa watu maskini katika maeneo ya maskini zaidi nchini Marekani. Bodi hii ya Wakuregenzi, Jumatatu tarehe 18 Mei 2026 imekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kudumisha vifungo vya umoja na upendo na Khalifa wa Mtakatifu Petro, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Sherehe ya Pentekoste, Mama Kanisa anapoitwa na kutumwa kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, chemchemi ya maisha mapya katika Kristo Yesu.

Mashuhuda wa Injili ya upendo kwa Maskini
Mashuhuda wa Injili ya upendo kwa Maskini   (@VATICAN MEDIA)

Tangu wakati wa Pentekoste, Habari Njema, ilianza kuenea tangu Yerusalemu na baadaye katika maeneo yaliyouzunguka mji huu. Jumuiya ya kwanza ya waamini ilikuwa ikidumu katika mafundisho ya Mitume wakakuza na kudumisha ushirika na katika kuumega mkate. Watu walioamini walizidi kuongezeka na walikuwa wakiweka mali za ona vitu vyao vyote shirika. Hii ndiyo ari na moyo vilivyomsukuma Padre Francis Clement Kelley, miaka 120 iliyopita kuanzisha Jumuiya ya Kipapa ya Ugani ya Kikatoliki: “The Catholic Extension Society”, ili kuwahudumia maskini waliokuwa pembezoni mwa nchi ya Marekani, kwa kuwapelekea Sakramenti za Kanisa pamoja na huduma makini kwa watu wa Mungu katika ujumla wao.

Huduma kwa Maskini ni kielelezo cha upendo kwa Mungu
Huduma kwa Maskini ni kielelezo cha upendo kwa Mungu   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ari na mwamko wa kimisionari bado unatakiwa katika ulimwengu mamboleo na kwamba, huduma hii ya kichungaji kwa maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” bado ni muhimu sana ndani na nje ya nchi ya Marekani. Baba Mtakatifu amewaomba wakuregenzi hawa kuelekeza misaada yao huko Cuba na Puerto Rico, kama kielelezo cha upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Leo XIV amewapongeza kwa huduma makini wanayotoa kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji, kielelezo cha uwepo endelevu na angavu kwa watu wanaoteseka kutokana na hali mbalimbali za maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, upendo kwa maskini unaweza kueleweka kama “alama ya Kiinjili ya Kanisa aminifu kwa moyo wa Mungu” na hivyo kuwa ni fursa ya kufungua malango kwa ajili ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili na hivyo hii inakuwa ni fursa kwa wale wanaohudumiwa kumfahamu Kristo Yesu, kama kielelezo makini cha ushuhuda kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Injili ya upendo kwa Maskini ni ushuhuda wa imani katika matendo
Injili ya upendo kwa Maskini ni ushuhuda wa imani katika matendo   (@VATICAN MEDIA)

Hii ni nafasi ya kujenga na kupanua Jumuiya za Kikatoliki zenye ari na mwamko wa kimisionari; Jumuiya zinazokita mizizi yake katika imani inayogeuka na kuwa ni chemchemi ya furaha na maisha mapya katika Kristo Yesu. Mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Jumuiya hizi ni udongo mzuri wa kuchipusha na kuchanua miito mitakatifu ya Upadre na Maisha ya kuwekwa wakfu inaweza kuanza kukita mizizi yake na hatimaye, kuanza kukua na hatimaye kutoa wachungaji wapya kwa siku za usoni. Rej. Mt 13: 8. Huu ni mwaliko kwa waamini kukabiliana na changamoto za kiimani, kwa kuendelea kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa furaha na ukarimu, huku wakiendelea kuchochewa na upendo kwa Mungu na jirani na kwa uhakika kwamba, Baba “aonaye sirini atakujazi” (Mt 6:4). Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewakabidhi wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume, waendelee kutunza dhamana ya amani na furaha inayopata chimbuko lake kwa Kristo Yesu Mfufuka.

Ushuhuda wa Imani
18 Mei 2026, 14:26