Papa Leo XIV kwa Tawadros II:Wakristo washuhudie umoja katika ulimwenye wa vita
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alituma ujumbe wake kwa Papa wa Kanisa Kiorthodox la Kikoptiki katika fursa ya Siku ya Urafiki kati ya Kikoptiki na Wakatoliki, ulioanzishwa mwaka 2013 ili kusherehekea uhusiano kati ya Kiti cha Mtume Petro na Kiti cha Mtakatifu Marko. Papa anaelezea ufahamu wa jukumu la pamoja la kutangaza Injili na kukuza amani na upatanisho ulioneshwa. Katika barua hiyo, anawahimiza Wakoptiki na Wakatoliki kuendelea na hija yao katika ukweli na upendo ili kuelekea ushirika kamili. Baba Mtakatifu anaanza kusema kuwa Mpendwa katika Kristo , Kristo amefufuka! Al-Messih qam!
“Hakuna aliye na upendo mkuu kuliko huu...”
Katika mwanga wa furaha ya Pasaka, Papa alifurahi kuwasalimu “katika hafla ya furaha ya Siku ya Urafiki kati ya Wakoptiki na Wakatoliki, “hivyo kuendeleza utamaduni mzuri wa mtangulizi wake, Papa Francisko. “Siku hii ya Urafiki, ambayo wazo lake lilitoka kwake, Patriaki inaadhimisha uhusiano kati ya Kiti cha Petro na Kiti cha Marko na, kiukweli, ni mpango muhimu. “Kwetu Wakristo, urafiki si hisia isiyoeleweka; ni kiini cha maisha yetu na imani yetu. Hakika, Bwana wetu mwenyewe anatuita kuwa marafiki zake (taz. Yn 15:15) na anatufundisha kwamba "Hakuna aliye na upendo mkuu kuliko huu, wa kutoa uhai wake kwa ajili ya marafiki zake" (Yn 15:13).
"Kuimarisha urafiki kati yetu na makanisa yetu"
Baba Mtakatifu Leo XIV alisema kuwa: “Kwa hivyo, ni kwa kutumia urafiki wa Kristo kwa ajili yetu kwamba tutaweza kuimarisha urafiki kati yetu na kati ya Makanisa yetu, tunapoendelea kushuhudia pamoja upendo wa kimungu kwa wanadamu wote! Hija hii ya urafiki imeruhusu Makanisa yetu, yaliyotenganishwa na karne nyingi za kutoelewana, kushiriki katika mazungumzo ya Kitaalimungu yenye matunda mengi yaliyoanzishwa zaidi ya miaka hamsini iliyopita na Mtakatifu Paulo VI na Patriaki Shenouda III, ya kumbukumbu ya shukrani.” Mazungumzo haya, ambayo mwanzoni yalikuwa ya pande mbili, yamefanyika tangu 2003 ndani ya mfumo wa Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Mazungumzo ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki, ambayo hati zake Tatu za msingi zinaonesha uelewa unaokua wa kitaalimungu. Ni matumaini yangu kwamba Tume hii, ambayo Kamati yake ya Uratibu inakutana hivi sasa Roma, hivi karibuni itaanza tena kazi yake na Makanisa yote ya familia ya Kiorthodox ya Mashariki, ili kujibu sala ya Kristo "ili wote wawe kitu kimoja" (Yn 17:21).”
Papa atoa shukrani kwa Kanisa la Kiorthodox la kikoptiki kwa ukarimu
Baba Mtakatifu alituma fursa hiyo “kutoa shukrani zangu za dhati kwa kwake Yeye Patriaki, na kwa Kanisa la Kiorthodox la Koptiki kwa ukarimu wa kidugu uliotolewa kwa washiriki katika Mkutano wa Sita wa Dunia wa Tume ya Imani na Utaratibu, ikiwa ni pamoja na ujumbe mkubwa wa Wakatoliki, uliofanyika Oktoba 2025 katika Monasteri ya Mtakatifu Peshoy huko Wadi El Natrun.” Papa anaamini kwamba “tafakari kuhusu tukio la maadhimisho ya miaka 1700 ya Mtaguso wa Kwanza wa Kiekumeni zitaamsha tena hamu yetu ya kufikia umoja unaoonekana wa Kanisa, umoja unaotokana na ubatizo mmoja tunaosadiki katika Imani ya Nicaea ambayo, ni maombi yangu ya dhati, tutaufikia." Katika wakati ambapo ulimwengu wetu umeathiriwa na migogoro mingi, hasa katika Mashariki ya Kati, Wakristo lazima, zaidi ya hapo awali, watafute umoja kamili ili kwa pamoja tuweze kumshuhudia Mfalme wa Amani.”
Kwa kufanya hivyo, Papa Leo XIV aiongeza kusema: "tunaweza kuweka tumaini letu katika maombezi yenye nguvu na mfano wa mashahidi wengi wasiohesabika walioteseka kwa ajili ya jina la Kristo." Papa akimwelekea Patriaki huyo alisema "Makanisa yetu yanapojiandaa kwa ajili ya sherehe ya Pentekoste, ninaomba kwamba Roho Mtakatifu, chanzo na mbebaji wa vipaji vyote, awaongoze Wakoptiki na Wakatoliki katika hija yao ya pamoja katika ukweli na upendo kuelekea ushirika kamili." Hatimaye kwa kutarajia furaha ya kukutana naye kibinafsi, Baba Mtakatifu Leo XIV alimwakikishia, maombi yake wakati akimtumia mkumbatio wa kidugu wa “amani katika Kristo, Bwana wetu Mfufuka.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.
