Tafuta

2026.05.15:Washiriki katika Mkutano wa Mabunge kuhusu Kupambana na Uhalifu wa Kupangwa katika Kanda ya OSCE. 2026.05.15:Washiriki katika Mkutano wa Mabunge kuhusu Kupambana na Uhalifu wa Kupangwa katika Kanda ya OSCE.  (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV:Mitandao ya kijamii katika kupotosha hatari za matumizi ya dawa za kulevya

Papa akikutana na Washiriki wa Mkutano wa Mabunge Kimataifa kuhusu Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu wa Kupangwa katika Kanda ya OSCE,Mei 15 mjini Vatican:"Vatican inaunga mkono kwa moyo wote kila mpango unaolenga kuanzisha mfumo wa haki za jinai wenye ufanisi,haki,kibinadamu na unaoaminika unaoweza kuzuia na kukabiliana na uzalishaji na biashara haramu ya dawa za kulevya."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana na Wawakilishi wa Mataifa yanayoshiriki Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya(OSCE)wakiwa katika Mkutano wa II wa Kimataifa kuhusu "Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu wa Kupangwa" wa Kanda hiyo tarehe 15 Mei 2026 mjini Vatican. Papa alielezea matumaini na wasi wasi wa  kichungaji katika kupambana na haraka dhidi ya janga haramu  la dawa za kulevya.

Mkutano wa kimataifa wa OSCE
Mkutano wa kimataifa wa OSCE   (@VATICAN MEDIA)

Kuzuia uhalifu na haki ya jinai

Papa Leo XIV alisema kuwa uwepo waoumetokana na Mataifa mengi yanayoshiriki Shirika hili la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya(OSCE) kuanzia Vancouver hadi Vladivostok,  "wanasimama kidete kama ushuhuda wa azimio la pamoja la kukabiliana na jambo linalodumisha mitandao ya uhalifu na kuhatarisha mustakabali wa jamii zetu.” Papa aliongeza “Kiti Kitakatifu kinaamini kabisa kwamba utawala wa sheria, kuzuia uhalifu na haki ya jinai lazima zisonge mbele pamoja kwa umoja. Hakika, utekelezaji halisi wa utawala wa sheria unabaki kuwa muhimu kwa maendeleo fungamani ya binadamu."

Hakuna jamii yenye haki ya kweli inayoweza kudumu isipokuwa sheria na si mapenzi ya watu binafsi,  ibaki kuwa huru (taz. Muhtasari wa Mafundisho ya Kijamii ya Kanisa, 408), huku hakuna mtu au kikundi, bila kujali mamlaka au hadhi, kinachoweza kudai haki ya kukiuka utu na haki za wengine au za jamii zao,” Papa alieleza. Papa Leo XIV alisema,  “kuzuia na kujibu shughuli za uhalifu kuna uhusiano wa karibu na heshima na ulinzi wa haki za binadamu kwa wote. Hii haihitaji juhudi za mamlaka za kutekeleza sheria tu,  bali pia ushiriki wa jamii kwa ujumla, katika ngazi za Kitaifa na Kimataifa.” Katika suala hilo, Vatican inaunga mkono kwa moyo wote kila mpango unaolenga kuanzisha mfumo wa haki za jinai wenye ufanisi, wa haki, wa kibinadamu na unaoaminika unaoweza kuzuia na kukabiliana na uzalishaji na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Washiriki wa Mkutano uliandaliwa na OSCE
Washiriki wa Mkutano uliandaliwa na OSCE   (@Vatican Media)

Programu kamili zinahitajika kuwafikia wanaotumia madawa ya kulevya

Kwa kutambua kwamba haki ya kweli haiwezi kuridhika na adhabu pekee, juhudi hizo lazima pia zikumbatie mbinu zinazoashiriwa na uvumilivu na huruma, zinazolenga kuelimisha upya na kuwaunganisha tena wahalifu katika mfumo wa jamii. Heshima ile ile kwa utu wa asili wa kila mtu, ikiwa ni pamoja na wale waliofanya uhalifu, huzuia matumizi ya adhabu ya kifo, mateso, na kila aina ya adhabu ya kikatili au ya kudhalilisha. Programu kamili zinahitajika ili kuwafikia wale walio watumwa wa uraibu, kuwapa matibabu ya kimatibabu, msaada wa kisaikolojia na ukarabati endelevu. Mbinu kama hiyo ya taaluma mbalimbali lazima imzingatie mwanadamu kwa ukamilifu wake, ikizidi hatua za ukandamizaji na suluhisho za kuruhusu, ambazo zote mbili hushindwa kuwakomboa watu kutoka kwa minyororo ya utegemezi.

Elimu lazima ianzie ndani ya familia

Kwa njia hiyo, wanaweza kugundua upya na kuishi upya utimilifu wa utu wao waliopewa na Mungu. Zaidi ya hayo, Papa Leo XIV alipenda kusisitiza kwamba, “elimu ni muhimu kwa kuzuia. Inaunda msingi wa maendeleo fungamani ya binadamu na kuwaandaa watoto na vijana kutambua uharibifu mkubwa unaosababishwa na dawa za kulevya.” Katika wakati wetu, ambapo mitandao ya kijamii mara nyingi husambaza taarifa potofu hatari zinazopunguza hatari hizi, Papa aliongeza “ elimu lazima ianzie ndani ya familia na kuimarishwa shuleni, ikitoa maarifa sahihi ya kisayansi kuhusu athari mbaya za dawa za kulevya kwenye ubongo, mwili, tabia binafsi na manufaa ya jamii.”

Mkutano uzae matunda ya kudumu katika mikakati ya ushirikiano wa Kimataifa

Papa Leo XIV alisema kuwa “kuzuia na kukabiliana na uhalifu uliopangwa ni muhimu kwa kujenga jamii salama, za haki na imara. Kwa mtazamo huo, Papa alipenda pia  kuwashukuru "maafisa wote wa kutekeleza sheria na wanachama wa mahakama ambao wamejitolea maisha yao au kupata majeraha katika utendaji wao wa ujasiri. Ushuhuda wao unapaswa kuchochea ndani yetu hisia za shukrani, uwajibikaji na azimio jipya.” Kwa kuongezea zaidi Papa alisema "Kanisa Katoliki, kupitia taasisi zake nyingi ulimwenguni  kote, na kwa kutumia uzoefu wake wa muda mrefu katika kuwasindikiza wale walioathiriwa na uraibu, liko tayari kuimarisha zaidi uhusiano wake wa ushirikiano wenye matunda na asasi za kiraia."

Papa Leo XIV akiwabariki
Papa Leo XIV akiwabariki   (@Vatican Media)

Kwa pamoja, "katika roho ya kuheshimiana na uwajibikaji wa pamoja, Papa aliongeza "tunaweza kuhamasisha sera zinazohudumia kweli manufaa ya wote na utu usioweza kuondolewa wa kila mwanadamu." Mkutano huo " uzae matunda tele na ya kudumu katika mikakati ya ushirikiano wa kimataifa, kinga madhubuti na matumaini ya kweli." Kwa kuhitimisha Papa alisema "Kwa nyote, kwa majadiliano yenu na kwa watu mnaowawakilisha, nawaombea baraka nyingi za Mungu za hekima, ujasiri na amani ya kudumu," aliwapatia Baraka yake ya Kitume.

PAPA KWA OSCE

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

 

15 Mei 2026, 10:58