Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 9 Mei 2026 alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa “Edith Haberland-Wagner Foundation and Augustiner-Bräu” Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 9 Mei 2026 alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa “Edith Haberland-Wagner Foundation and Augustiner-Bräu”   (ANSA)

Papa Leo XIV: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote

Baba Mtakatifu Leo XIV mwenyewe amewashukuru sana kwa kumzawadia kazi ya mikono ya Mfuko huu ambao kwa namna ya pekee unagusa maisha na utume wake kama Mtoto wa Mtakatifu Augostino anayewakumbusha watu wa Mungu kwamba, karama na talanta walizopewa na Mwenyezi Mungu ili ziweze kuwafaidia, zinapata utimilifu na furaha kubwa zinapomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na katika huduma kwa jirani. Utunzaji wa Mazingira!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 9 Mei 2026 alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa “Edith Haberland-Wagner Foundation and Augustiner-Bräu” wenye Makao yake makuu mjini Munich, nchini Ujerumani. Hii ikawa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kutafakari mapokeo ya huduma ya Kiagostiani na umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia kwa busara na kwa haki kazi ya uumbaji kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ilikuwa ni tarehe 8 Mei 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV alipokabidhiwa dhamana ya: Kuongoza, Kufundisha na Kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Siku ya Sala maalum kwa ajili ya Bikira Maria wa Pompei. Kumbe, hija hii ya kitume ilipania pamoja na mambo mengine, kuiweka huduma na utume wa kichungaji unaotekelezwa naye kama Khalifa wa Mtakatifu Petro chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Pompei na kwamba, katika maisha na utume wake, anaendelea kufuata nyayo za Papa Leo XIII, ambaye pamoja na mambo mengine, ni Kiongozi wa Kanisa aliyejibidiisha kuweka msingi wa Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kuhusu Rozari Takatifu pamoja na yeye mwenyewe kumtangaza Mwenyeheri Bartolo Longo, Mtume wa Rozari Takatifu kuwa ni Mtakatifu.

Kumbukizi ya Mwaka Mmoja Tangu Papa Leo XIV achaguliwe kuliongoza Kanisa
Kumbukizi ya Mwaka Mmoja Tangu Papa Leo XIV achaguliwe kuliongoza Kanisa   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha wa kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Leo XIV alipochaguliwa kuliongoza Kanisa: Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume; wajumbe wa Mfuko wa “Edith Haberland-Wagner Foundation and Augustiner-Bräu” waliamua kumtembelea Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican na yeye mwenyewe amewashukuru sana kwa kumzawadia kazi ya mikono ya Mfuko huu ambao kwa namna ya pekee unagusa maisha na utume wake kama Mtoto wa Mtakatifu Augostino anayewakumbusha watu wa Mungu kwamba, karama na talanta walizopewa na Mwenyezi Mungu ili ziweze kuwafaidia, zinapata utimilifu na furaha kubwa zinapomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na katika huduma kwa jirani.

Zawadi ni kazi ya mikono ya Mfuko huu
Zawadi ni kazi ya mikono ya Mfuko huu   (@Vatican Media)

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, mahujaji hawa wataimarika kiimani na hivyo kutiwa nguvu ya kusonga mbele katika kuwahudumia jirani zao na hasa wale wanaohitaji msaada zaidi. Hivi karibuni, Mama Kanisa amekumbuka Mwaka mmoja, tangu Papa Francisko alipofariki dunia. Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anasema, utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu na umegawanyika katika sura kuu sita: Mambo yanayoendelea kujiri katika mazingira; Injili ya Kazi ya Uumbaji na Amani Duniani; Vyanzo vya mgogoro wa Ikolojia na jinsi vinavyohusiana na watu; Ikolojia ya mazingira, uchumi na jamii. Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni kuhusu umuhimu wa elimu ya ikolojia inayojikita katika wongofu wa ndani, furaha na amani, Sakramenti za Kanisa pamoja na sala.

Papa Leo XIV: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote
Papa Leo XIV: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote   (@Vatican Media)

Katika Waraka huu muhimu Baba Mtakatifu Francisko alitoa ujumbe wa kila kiumbe katika kuleta amani ya kazi ya uumbaji kwa kutambua madhumuni ya kila kiumbe na kwamba, Ulimwengu mzima unaonekana kuuzunguka: ukuu na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Rej. Laudato si n. 84. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, rasilimali za dunia hii zinatumiwa kwa busara kwa kuzingatia haki ambalo ni sharti la amani. Kumbe, wanaporejea majumbani mwao waendelee kukuza bna kudumisha haki kama sehemu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kitaaluma na kibinafsi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV akawakabidhi wajumbe hawa kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.

Papa Leo XIV Mazingira
12 Mei 2026, 14:07