Tafuta

Papa Leo XIV: Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu." Papa Leo XIV: Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu." 

Ujumbe wa Papa Leo XIV Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni Kwa Mwaka 2026

Maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, tarehe 17 Mei 2026, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni: Kauli mbiu “Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu.” Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuhakikisha kwamba, uvumbuzi wa teknolojia, hasa matumizi ya teknolojia ya akili unde, inamhudumia binadamu badala ya kuchukua nafasi au kupunguza utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, Kristo Yesu baada ya kusema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Mwili wa Kristo ulitukuzwa wakati ule ule alipofufuka kama zinavyoshuhudia hali mpya na za kimungu ambazo tokea hapo umebaki nazo daima. Lakini kile kipindi cha siku arobaini ambako alizoea kula na kunywa pamoja na wafuasi wake, na kuwafundisha juu ya Ufalme wa mbinguni, utukufu wake bado ulifunikwa na alama za ubinadamu wa kawaida. Tokeo la mwisho la Yesu linakamilika na kuingia bila kurudi kwa ubinadamu wake katika utukufu wa Mungu uliojionesha katika sura ya wingu na mbingu (Lk 24:51) ambako tangu hapo ameketi kuume kwa Mungu. Kwa namna moja tofauti kabisa na ya pekee atajionesha kwa Paulo “kama mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake” katika tokeo la mwisho lililomfanya kuwa Mtume. Hali iliyofunikwa ya utukufu wa Kristo Mfufuka kipindi hiki inaonekana katika maneno yake ya fumbo kwa Mariamu Magdalena: “Sijapata kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ninapaa kwenda kwa Baba yangu, naye ni Baba yenu.” Yn 20:17 Hii inaonesha tofauti ya kujidhihirisha kati ya utukufu wa Kristo Mfufuka na ule wa Kristo aliyetukuzwa kuume kwa Baba. Tukio ambalo kwa upande mmoja ni la kihistoria na bora sana linaloonesha kupita toka upande mmoja kwenda upande mwingine. Lakini yote yanabaki yakiwa yameungana kabisa na lile la kwanza yaani kushuka kutoka mbinguni kulikotekelezwa katika Fumbo la Umwilisho. Ubinadamu ukiachiwa katika nguvu zake za maumbile hauwezi kufika kwenye nyumba ya Baba wa milele. Kristo Yesu peke yake ameweza kumfungulia mwanadamu njia hii “ili tukae tukiamini kwamba sisi tulio viungo vyake ametutangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shina letu na kwamba, akiisha inuliwa juu ya nchi atawavuta wote kwake.” Huku ni kuinuliwa juu ya Msalaba ambako huonesha na kutangaza kuinuliwa kwa kupaa mbinguni. Huo ndio mwanzo wake.

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Ushuhuda wa imani
Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Ushuhuda wa imani   (Vatican Media)

Mbinguni Kristo Yesu anatekeleza Ukuhani wake daima, Yeye ni kiini na mtendaji mkuu wa Liturujia inayomheshimu Baba wa mbinguni. Kristo Yesu ameketi kuume kwa Baba, maana yake: ameketi katika utukufu na heshima ya Kimungu, ambaye Yeye aliyekuwako kama Mwana wa Mungu kabla ya nyakati zote, kama Mungu, na mwenye uwamo mmoja na Baba, anaketi kimwili, baada ya kumwilishwa na baada ya mwili wake kutukuzwa. Kuanzia hapo Mitume wamekuwa ni mashuhuda wa Ufalme usiokuwa na mwisho. Rej. KKK 659-664. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, tarehe 17 Mei 2026, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu.” Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuhakikisha kwamba, uvumbuzi wa teknolojia, hasa matumizi ya teknolojia ya akili unde, inamhudumia binadamu badala ya kuchukua nafasi au kupunguza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake anasema, nyuso na sauti za binadamu ni za kipekee, sifa bainifu za kila mtu; zinafichua utambulisho wa mtu mwenyewe usioweza kurudiwa na ni vipengele vinavyobainisha vya kila kukutana na wengine. Wahenga walielewa hili vizuri. Ili kufafanua mtu wa kibinadamu, Wagiriki wa kale walitumia neno "uso" (prósōpon), kwa sababu linaoneesha asili yake ni kile kilicho mbele ya macho ya mtu, mahali pa kuwepo na uhusiano. Neno la Kilatini "mtu" kwa upande mwingine, husababisha wazo la sauti: sio sauti yoyote, lakini sauti isiyojulikana ya sauti ya mtu. Nyuso na sauti ni mambo matakatifu. Mwenyezi Mungu aliye muumba mwanadamu kwa sura na mafano wake, aliwakirimia binadamu hawa kuweza kuishi kwa njia ya Neno wake aliyewaelezea. Neno hili limesikika kwa karne nyingi kupitia sauti za manabii, kisha likafanyika Mwili katika utimilifu wa nyakati, watu wakalisikia na kuliona. Rej. 1Yn 1: 1-3.

Kristo Yesu Ameinuliwa Juu ya Msalaba
Kristo Yesu Ameinuliwa Juu ya Msalaba   (Vatican Media)

Mwenyezi Mungu anajitambulisha kwa sababu amefunuliwa mbele ya mwanadamu kwa Sauti na Uso wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu. Tangu mwanzo wa Uumbaji Mwenyezi Mungu aliweka chapa kwenye nyuso za mwanadamu, kielelezo cha ufunuo wa upendo wa Mungu na hatimaye, binadamu aweze kuishi kikamilifu ubinadamu wake kwa njia ya upendo. Kumbe, kuhifadhi nyuso na sauti za binadamu kuna maanisha kuhifadhi alama isiyofutika ya upendo wa Mungu kwa binadamu na kwamba, kila mtu ana wito usioweza kubadilishwa na usiokuwa na kifani unaopata chimbuko lake kutokana na tajiriba inayojidhihirisha kupitia mwingiliano na wengine.Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, mwanadamu akishindwa katika kazi hii ya kuhifadhi, teknolojia ya kidijitali inatishia kubadilisha kwa kiasi kikubwa baadhi ya nguzo za msingi za ustaarabu wa binadamu ambazo nyakati fulani huchukuliwa kuwa ni za kawaida. Kwa kuiga sauti na nyuso za binadamu, hekima na maarifa, fahamu na uwajibikaji, huruma na urafiki, mifumo inayojulikana kama akili mnemba haiingiliani tu na mifumo ya ikolojia ya habari, lakini pia huingilia kiwango cha ndani zaidi cha mawasiliano, kile kinachogusa uhusiano wa kibinadamu. Changamoto, kwa hiyo, si ya maendeleo ya kiteknolojia tu, bali ya “kianthropolojia.” Kulinda nyuso na sauti hatimaye kunamaanisha kujilinda. Kukumbatia fursa zinazotolewa na teknolojia ya kidijitali na akili mnemba kwa ujasiri; uamuzi na utambuzi huu haimaanishi kufumbia macho masuala msingi, magumu na hatari.

Papa Leo XIV: Matumizi sahihi ya Teknolojia ya Akili unde
Papa Leo XIV: Matumizi sahihi ya Teknolojia ya Akili unde

Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka watu wa Mungu kamwe wasikatae uwezo wao wa kufikiri. Kwa muda mrefu kumekuwa na ushahidi mwingi kwamba “algoriti” iliyoundwa ili kuongeza ushiriki kwenye mitandao ya kijamii, ambayo ni faida kwa majukwaa hulipa hisia za haraka na kuadhibu majibu zaidi ya wanadamu yanayotumia wakati kama vile juhudi zinazohitajika kuelewa na kutafakari. Kwa kuwaweka watu katika vikundi vya maelewano rahisi na hasira kirahisi, kanuni hizi hupunguza uwezo wa binadamu wa kusikiliza na kufikiria kwa umakini, na matokeo yake ni kuongeza ubaguzi wa kijamii. Kutokana na utegemezi mkubwa wa akili mnemba amegeuka na kuwa ni "rafiki" anayejua yote, chanzo cha maarifa yote, na kumbukumbu ya ushauri wote. Haya yote yanaweza kuharibu zaidi uwezo wa binadamu wa kufikiri kiuchambuzi na kiubunifu, kuelewa maana na kutofautisha kati ya Sintaksia na Semantiki; haya ni matawi mawili makuu ya isimu yanayohusika na muundo na maana katika lugha. Sintaksia huchunguza mpangilio na muundo wa maneno ya kuunda sentensi, huku Semantiki (sarufi maana) ikichambua maana ya maneno, tungo, na sentensi. Kwa pamoja, husaidia kuelewa jinsi lugha inavyopangwa na kueleweka.

"Nenda kawaambie ndugu zangu nina paa kwenda kwa Baba!
"Nenda kawaambie ndugu zangu nina paa kwenda kwa Baba!   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anakiri kwamba, teknolojia ya akili mnemba inaweza kuwa ni msaada mkubwa katika mawasiliano na hivyo kukwepa juhudi za kufikiria wenyewe na hatimaye kusuluhisha mkusanyiko wa takwimu bandia hali ambayo kimsingi inatishia ujuzi, utambuzi, kihisia na katika mawasiliano. Katika miaka ya hivi karibuni, mifumo ya akili mnemba imezidi kuchukua udhibiti wa utengenezaji wa maandishi, muziki na video. Hii inaweka sehemu kubwa ya tasnia ya ubunifu wa binadamu katika hatari ya kubomolewa na kuandikwa kwamba, “inaendeshwa na teknlojia ya akili unde” na hivyo kuwageuza watu kuwa watumiaji wa kawaida wa mawazo yasiyofikiriwa na bidhaa zisizojulikana bila umiliki au upendo. Wakati huo huo, kazi bora za ustadi wa mwanadamu katika nyanja za muziki, sanaa na fasihi zinapunguzwa kwa kujielekeza na matumaini katika maendeleo ya sayansi na teknolojia. Binadamu anaweza kufikia, kwa kukua katika ubinadamu na ujuzi kwa kupitia matumizi ya hekima na busara ya zana zenye nguvu katika huduma ya binadamu kwa njia ya tafiti bora na makini sanjari na uwajibikaji wa mtu binafsi. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kuwekeza katika ubunifu, ili kukuza na kudumisha karama na talanta ambazo mwanadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kujenga na kudumisha uhusiano na mafungamano na watu wengine; maana yake ingekuwa ni kwa mwanadamu kuficha nyuso na kunyamazisha sauti zao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kuwa au kujifanya kuwa: kuiga uhusiano na ukweli kwani kuna uingiliaji kati usio na uwazi unaojiendesha kiasi cha kuathiri mijadala ya umma na chaguo za watu; kutokana na ufanisi wa kushangaza, ushawishi wa siri kupitia uboreshaji unaoendelea wa mwingiliano uliobinafsishwa, hali inayoonesha udanganyifu mkubwa kwa kuiga hisia za binadamu na uhusiano wake na matokeo yake ni hatari sana kwa kuficha hisia za binadamu na hivyo kujitahidi kuiga uhusiano na urafiki wa kijamii. Teknolojia inayotumia vibaya hitaji la uhusiano wa kibinadamu, linaweza kusababisha athari kubwa katika maisha ya binadamu; katika mifumo ya kijamii na kisiasa kwani matumizi ya akili unde yanafanya kila kitu kutengenezwa kwa sura na mfano wa binadamu; lakini bila kuwakumbatia na kuwaambata wengine, hakuna uhusiano au urafiki wa kijamii.

Papa Leo XIV: Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu
Papa Leo XIV: Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, changamoto nyingine kubwa inayoletwa na mifumo hii inayoendelea kuibuka ni ile ya upendeleo, ambayo inasababisha kupata na kusambaza mtazamo uliobadilisha ukweli sababu mifumo ya teknolojia ya akili unde inatengenezwa na wale walioiunda hivyo kwa upande wake, zinaweza kuzalisha chuki, uwasilishaji duni wa kijamii wa data na huwaweka wanadamu katika mtego ya mitandao ambayo inadhibiti mawazo ya binadamu, kuongeza muda na kuzidisha ukosefu wa haki msingi za kijamii pamoja na ukosefu wa usawa kiasi cha binadamu kushindwa kupambanua ukweli na kutoka katika wazo la kufikirika, hali inayojenga tabia ya kutoaminiana, kuchanganyikiwa pamoja na ukosefu wa usalama. Matumizi ya teknolojia ya akili unde yanapaswa kuratibiwa, kwa kutambua asili yake, kwa kusimama kidete kulinda na kuwendweleza mwanadamu, ili awe na uwezo wa kutumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kwa kuzingatia kwanza kabisa: Uwajibikaji, ushirikiano na elimu. Hii ina maana ya kujikita katika uaminifu, ukweli na uwazi; ujasiri, kuwa na maono ya mbali na kwamba huu ni msingi wa ujenzi wa leo na kesho yenye matumaini inayosimikwa katika: Usawa, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watengenezaji wa teknolojia ya akili unde wanahimizwa kutekeleza dhamana na wajibu wao katika misingi ya ukweli na uwazi; ili kulinda, kuheshimu na kudumisha utu na heshima ya binadamu; watu wanapaswa kuwajibika kijamii, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao.

Papa Leo XIV: Teknolojia iwe ni kwa ajili ya binadamu!
Papa Leo XIV: Teknolojia iwe ni kwa ajili ya binadamu!   (@Vatican Media)

Ni wajibu wa makampuni ya vyombo vya habari na mawasiliano ya jamii kujikita katika kukuza na kudumisha kanuni maadili na utu wema, ili kwamba, maudhui yanayozalishwa na akili mnemba yawekewe alama, ili yatambulikane kwa urahisi na hivyo kutofautishwa na yale yanayotengezwa au kuundwa na binadamu. Uandishi na umiliki kamili wa kazi ya wanahabari na waundaji wengine wa maudhui lazima ulindwe kwa kutambua kwamba, habari ni kwa ajili ya faida ya umma. Utumishi wa umma unaojenga na wa maana hautokani na uwazi, bali juu ya uwazi wa vyanzo, ushirikishwaji wa wale wanaohusika na viwango vya juu vya ubora. Ushirikiano ni jambo la msingi, ulinzi na usalama lazima udumishwe na kwamba, wadau wote kutoka kwenye tasnia ya teknolojia hadi kwa wabunge, kutoka katika kampuni za wabunifu hadi wasomi; kutoka kwa wasanii hadi kwa waandishi wa habari na waelimishaji; wote hawa wanapaswa kuelimishwa katika kujenga na kutekekeza uraia wa kidigitali unaowajibisha. Ni katika muktadha huu Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, elimu, haina budi ijikite katika mchakato wa kuongeza uwezo wa mtu binafsi wa kufikiri kwa kina; kutathmini kama vyanzo vya habari ni vya kuthaminiwa na kuaminika na maslahi yanayoweza kutokea baada ya kuchagua maelezo tunayoweza kufikia; kuelewa taratibu za kisaikolojia zinazohusika; na kuwezesha familia, jumuiya na vyama mbalimbali kuunda vigezo vya kiutendaji kwa kujikita katika utamaduni bora na wa kuwajibika zaidi katika tasnia ya mawasiliano ya jamii.

Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni
Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni

Ni katika muktadha huu, kuna haja kwa jamii kuingiza katika mfumo wa elimu kuhusu mawasiliano na matumizi ya akili mnemba na kwamba, Kanisa kwa upande wake, linapania pia kuchangia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mkazo ni kwa vijana wa kizazi kipya ambao wanaweza kupata ujuzi wa kufikiri kuhusu muhimu na kukua katika uhuru wa roho. Ujuzi huu wa kusoma na kuandika unapaswa pia kuunganishwa katika sera na mikakati ya kujifunza maisha yote ili kuwafikia watu wengi; wale wanaohisi kutengwa na kutokuwa na uwezo mintarafu mabadiliko haya makubwa na ya haraka ya sayansi na teknolojia. Kwa njia hii vyombo vya habari na mawasiliano ya jamii vinapaswa kuwa na ujuzi wa kusoma na kuandika kwa njia ya akili mnemba. Kujua kusoma na kuandika pia kutaruhusu ulinzi bora wa faragha na data kupitia ufahamu ulioongezeka wa vigezo vya usalama na chaguo za malalamiko.Ni muhimu watu wakajielimisha na kuwaelimisha wengine jinsi ya kutumia maendeleo makubwa ya sayansi ya akili mnemba, ili watu waweze kuitikia na kuambata maendeleo mapya kwa kuwa na ujuzi na matumizi ya kidigitali; elimu ya binadamu na kitamaduni ili kutengeneza mtazamo wa ukweli, jinsi maendeleo ya teknolojia ya akili unde yanayovyofanya kazi zake, mbinu inazotumiwa katika kuamua maudhui gani yanaweza kuwepo; kanuni maadili, utu wema na uchumi; miundo mbalimbali ya akili mnemba na jinsi inavyo weza kubadilishwa. Baba Mtakatifu Leo XIV anakazia kwa kusema, binadamu anahitaji nyuso na sauti ili kuwasemea watu tena. Wanahitaji kuthamini zawadi ya mawasiliano kama ukweli wa ndani kabisa wa ubinadamu, ambao uvumbuzi wote wa kiteknolojia unapaswa kuelekezwa. Katika kuelezea tafakari hizi, Baba Mtakatifu Leo XIV anawashukuru na kuwapongneza wale wote wanaofanya kazi kufikia malengo yaliyoelezwa hapo juu, na hatimaye akatoa baraka zake za kitume kwa wale wote wanaofanya kazi kwa manufaa ya wote kupitia vyombo vya habari na vile vya mawasiliano ya kijamii.

Papa Leo XIV Ujumbe Upashanaji Habari
14 Mei 2026, 15:10